Inawezekana ilikuwa ni nia njema kwenda kumshuku Rais kwa kumpa msamaha
uliomuepusha na kifungo cha maisha, lakini kitendo hicho cha Nguza
Mbangu Viking na wanawe kimepokelewa kwa hisia tofauti.
Nguza, ambaye ni mtunzi wa wimbo maarufu wa “Seya” uliomfanya apachikwe
jina la Babu Seya katika kesi ya kubaka na kulawiti wanafunzi wenye umri
kati ya miaka sita na nane, na mwanae Johnson Nguza au Papii Kocha,
walisamehewa na Rais John Magufuli pamoja na wafungwa wengine 8,150 siku
ya Uhuru wa Tanganyika.
Alikuwa kitumikia kifungo cha maisha baada ya mahakama kumtia hatiani
kwa kubaka na kulawiti watoto hao, na juhudi za kupangua hukumu hiyo
Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufani na nyuingine za nje hazikuweza
kufanikiwa.
Lakini msamaha wa nadra kutokea kwa wafungwa wanaotumikia kifungo cha
maisha na wenye makosa ya kubaka na kulawiti, ulimuepusha nyota huyo
maarufu kwa kupiga gitaa la solo na mara tu alipotoka alisema angependa
kuonana na Rais kwa ajili ya kumshukuru na akapata nafasi hiyo juzi.
Lakini kupokelewa kwake kumeibua hoja tofauti.
Wako wanaowaangalia waliofanyiwa vitendo hivyo miaka 13 iliyopita, ambao
kwa sasa ni wasichana, na wengine wanaoangalia nafasi waliyoipata
tofauti na wengine walionufaika na msamaha huo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, watu waliohojiwa na gazeti hili
walisema tukio la kwenda Ikulu halikupaswa kupambwa, pamoja na ukweli
kwamba Katiba inampa Rais mamlaka ya kusamehe wafungwa wa aina yoyote.
“Sikuona haja ya Ikulu kulikuza suala la wanamuzi hao kwenda kuonana na
Rais. Baada ya kusamehewa kwa nini wanageuzwa kama mashujaa?,” alihoji
Wakili Onesmo Kyaule.
“Inawezekana kabisa hilo likawa na picha tofauti kwa watu waliofanya au watakaofanya makosa kama yao.”
Ikulu ilisambaza picha za Nguza na familia yake wakiwa wanatembea
kuelekea Ikulu na baadaye wakiwa kwenye mazungumzo na Rais na nyingine
zinazoonyesha wakisalimiana na baadaye wakitoka.
Dk Kyauke alisema licha ya sheria kumpa Rais mamlaka ya kusamehe, wanamuziki hao walipaswa kurejeshwa kwao baada ya kusamehewa.
Naye wakili mwingine wa kujitegemea, Alloyce Komba wa kampuni ya Haki
Kwanza, alipinga kitendo cha wanamuziki hao kwenda Ikulu kwa maelezo
kuwa licha ya kusamehewa kwao, bado wana hatia ya ubakaji.
Alisema lingekuwa jambo la maana kama wangeitisha mkutano na waandishi
wa habari na kumshukuru Rais kuliko kwenda Ikulu na suala lao
kutangazwa.
“Rais akisamehe wafungwa anakuwa na vigezo vyake ila katika hili la kina Babu Seya, nimeshtuka kidogo,” alisema.
Alibainisha kuwa Papii Kocha na Babu Seya walitiwa hatiani na hata walipokata rufaa walishindwa.
“Kwa kuwa tunaheshimu utawala wa sheria na Mahakama ndio yenye uamuzi wa
mwisho na wahusika wameshindwa kwenye hizo ngazi zote, tunatakiwa
tuheshimu,” alisema.
“Kwenda Ikulu kuna heshima, hawa heshima hii wameipata wapi? Aaah sisi
tunaomuamini Mungu tunasema sawa ila katika sheria, sheria ni sheria.”
Alisema msamaha huo unaweza ukawa kikwazo kwa vyombo vya Serikali vinavyopambana kudhibiti makosa ya ubakaji na mengineyo.
Naye Profesa Mwesiga Baregu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (Saut)
alisema: “Sikutegemea kama wangeenda Ikulu kwa sababu msamaha wa Rais
haufuti hukumu. Hauondoi jinai waliyofanya.
“Sijasikia kama wameomba radhi nasema hivi kwa sababu watoto
waliotendewa vitendo hivyo pamoja na wazazi wao bado wapo na wanaliona
suala hili.”
Alisema kama wanamuziki hao wangekaribishwa Ikulu sambamba na
waliotendewa vitendo viovu walau ingeeleweka, “hata Serikali kufikiria
fidia kwa waliotendewa vitendo vile nayo ingeweza kueleweka”.
Kwa upande wake, Dk James Jesse wa Shule Kuu ya Sheria Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) pia alisema msamaha haujafuta kosa.
“Unapopewa msahama sio kwamba kosa lako linafutwa. Rais ana mamlaka ya
Kikatiba kufanya alichokifanya na kama watu watawaza tofauti huwezi
kuwazuia,” alisema.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa