Monday, 29 February 2016

#YALIYOJIRI>>>Kinara Uporaji Benki Mbagala Atiwa Mbaroni.Fahamu zaidi hapa.

Siku nne baada ya majambazi 12 kuvamia Benki ya Access tawi la Mbagala, jijini Dar es Salaam na kuiba Sh. milioni 20 na kusababisha vifo vya watu saba, mtu anayedaiwa kuwa kinara wa uhalifu huo ametiwa mbaroni baada ya kutajwa na washirika wake, akiwamo aliyekamatwa  akiwa anafunga ndoa.

Taarifa za uhakika  zinaeleza kuwa, kinara wa ujambazi huo alikamatiwa Sinza Mori, wilaya ya Kinondoni jana, saa 11:00 jioni.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, kikosi kinachoshirikisha askari wa majeshi mbalimbali ikiwamo, polisi na la wananchi wa Tanzania, kilinasa watu wanne kwenye sherehe ya harusi baada ya kufuatilia mawasiliano yao ya simu.

“Unajua sasa hivi hili suala linahusisha jeshi ambao wamefuatilia kwenye mtandao na kunasa simu za watu wanne ambao wamekamatwa huko Mbagala, akiwamo bwana harusi na watu wengine wanne,” kilisema chanzo cha habari hii.

Taarifa hizo zinasema baada ya watu hao kukamatwa wakiwa wanafunga ndoa msikitini, walisaidia kutoa taarifa ambazo hatimaye zilifanikisha kukamatwa kwa mtu huyo anayedaiwa kuwa ni kinara wa ujambazi huo.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alipoulizwa kuhusu tarifa hizo alisema bado hajazipata na kwamba yawezekana wasaidizi wake wamemkamata lakini bado hawajamfikishia taarifa.

Kinara huyo amekamatwa ikiwa imepita siku moja baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, kutangaza uwezekano wa kutumia Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kushirikiana na polisi kuwasaka wahalifu wote waliojificha kwenye misitu ya Bagamoyo na Pwani, ambako inadaiwa walikimbilia baada ya tukio la Mbagala.

Pia waziri huyo alisema katika operesheni hiyo, watakuwa wakiwasimamisha mara kwa mara watumia pikipiki kwa sababu vyombo hivyo vimekuwa vikitumiwa na majambazi katika kufanikisha matukio yao.

Friday, 26 February 2016

#YALIYOJIRI>>>WAZIRI NAPE AAHIDI UPATIKANAJI WA SERA YA FILAMU NCHINI.FAHAMU ZAIDI HAPA.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye (kulia) akiwasili eneo la tukio kushuhudia uchaguzi wa Rais, Makamu wa Rais pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) uliofanyika 25 Februari, 2016 Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu, Bi. Joyce Fissoo.
 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye (mwenye suti nyeusi) akihojiwa na na Wanahabari pamoja na baadhi ya Wasanii mara baada ya kuwasili eneo la tukio kushuhudia uchaguzi wa Rais, Makamu wa Rais pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) uliofanyika 25 Februari, 2016 Jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye (mwenye suti nyeusi) akiwahutubia Wasanii pamoja na wageni waalikwa wakati wa siku ya uchaguzi wa Rais, Makamu wa Rais pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) uliofanyika 25 Februari, 2016 Jijini Dar es Salaam.
 Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu, Bi. Joyce Fissoo (kushoto) akiwahutubia Wasanii pamoja na wageni waalikwa wakati wa siku ya uchaguzi wa Rais, Makamu wa Rais pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) uliofanyika 25 Februari, 2016 Jijini Dar es Salaam.
Viongozi wa Uchaguzi wakitoa maelekezo juu ya namna zoezi la upigaji kura kwa kiti cha Rais, Makamu wa Rais pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF).

#YALIYOJIRI>>>Waziri Mkuu Kassim Majaliwa apokea mchango wa vifaa vya bilioni 10/= vya mahospitalini kutoka Azam, Coke na Pepsi.Fahamu zaidi hapa.

Umoja wa Wazalishaji Vinywaji laini umetoa msaada wa vifaatiba vyenye thamani ya Sh10 bilioni vilivyopokelewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Vifaatiba vilivyopokelewa jana ni pamoja na mashine za aina mbalimbali kama utra sound, mashine za kustulia moyo, vitanda vya watoto njiti, vitanda vya kujifungulia, vitanda 80 vya kawaida na magodoro yake, ambavyo viliwekwa kwenye makontena 20.

“Haijapata kutokea msaada mkubwa kama huu,” alisema Majaliwa kwenye hafla hiyo iliyofanyika kwenye ghala la Bohari Kuu ya Dawa (MSD) iliyoko Mabibo, Ubungo jijini Dar es Salaam. 

 “Natoa wito kwa makampuni mengine binafsi kuunga mkono jitihada za Serikali.”

Msaada huo wa vifaa tiba unawalenga zaidi watoto na wajawazito, ikiwa ni jitihada za kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli katika kuboresha huduma za afya.

Msemaji wa umoja huo, Erastus Mtui kutoka Coca Cola Kwanza alisema msaada huo umelenga kusaidia watoto na wajawazito pamoja na wagonjwa wengine kama wa moyo.

“Tumelenga hasa vifaa vya watoto na wajawazito. Hii yote ni katika kuunga mkono jitihada za Rais Magufuli kwani anaboresha afya na kutokomeza rushwa, hii inayaokoa zaidi makampuni ya uzalishaji nchini,” alisema Mtui.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Majaliwa alizipongeza sekta binafsi kwa kushirikiana na Serikali kukabiliana na changamoto katika sekta ya afya.

Alisema vifaa hivyo vimekuja wakati mwafaka kwa kuwa vitawezesha vituo kutoa huduma bora za afya.

“Mtakumbuka kwamba hivi karibuni Rais Magufuli alihamasisha maboresho ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na hasa wodi ya wazazi, hatua hii mliyoichukua ya kutoa msaada wa vifaa hivi ni sehemu ya kumuunga mkono,” alisema Waziri Mkuu.

Alisema Serikali kupitia MSD itahakikisha vifaa hivyo vinasam bazwa kwenye vituo husika kwa umakini mkubwa, hasa maeneo yenye mahitaji makubwa.

Alisema tayari kuna orodha ya awali katika mikoa ya Dodoma, Geita, Katavi, Lindi, Kilimanjaro, Mara, Mbeya, Shinyanga na Tanga.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu alisema bohari imedhamiria kusambaza dawa na vifaa tiba vya kutosha kwenye kanda nane za nchi, lakini changamoto kubwa ni jinsi ya kuzihifadhi.

“Ukubwa wa ghala hili la vifaa tiba ni mita za mraba 19,650 na hapa panatugharimu kiasi cha Sh2.5 bilioni. Na iwapo tutaendelea kuhifadhi hapa, itatulazimu kulipia Sh4 bilioni,” alisema Bwanakunu na kuongeza kuwa:

“Kwa hiyo changamoto ni kupata eneo la kujenga ghala. Wizara ya Ardhi ikitupatia eneo, tunategemea kuanza ujenzi mara moja.” 

Wafanyakazi PSI wasimamisha ziara
 Wafanyakazi wa kampuni ya PSI walisimamisha msafara wa Waziri Mkuu kwa kuziba barabara wakati akiondoka, wakitaka wamuambie kero wanazokumbana nazo kazini.

Wafanyakazi hao walitoa kero zao mbalimbali ikiwa ni pamoja na kulipwa malipo kiduchu kiasi cha Sh5,750 kwa siku, huku wakinyimwa kushiriki kuchangia mfuko wa hifadhi ya jamii wa PPF.

“Shida yetu kubwa ni mshahara. Tangu mwaka 2013 tunalipwa Sh5,750 mpaka leo na kwa miaka yote hiyo watu hawashiriki PPF,” alisema Amini Athuman ambaye ni mfanyakazi wa PSI.

“Wote ni vibarua, hakuna aliyeajiriwa hapa. Pia kinamama wajawazito hawalipwi chochote wakienda kujifungua, mtu anafukuzwa kazi bila kosa lolote bosi akiamua.”

Akijibu malalamiko hayo, Waziri Mkuu alisema ameyapokea na kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ilishajipa kazi ya kusikiliza kero za wananchi na wafanyakazi, lazima tatizo hilo litatuliwe.

“Nawasihi kesho (leo) mje kazini asubuhi saa 2:00 asubuhi na Waziri ya Kazi, Jenister Mhagama atakuwa hapa kwa kuwa mmelalamika kwamba hata makato ya PPF hayakatwi. Namsihi kiongozi ayaandike vizuri malalamiko ili akija asome kwa umakini na utatuzi utapatikana kesho hiyohiyo. Nawasihi msigome kufanya kazi,” alisema.

#YALIYOJIRI>>>Wadaiwa 16 Waliotorosha Makontena Bandarini Waanza Kufilisiwa,Jana Zimekamatwa Kontena 9 za Mabati Ambazo Zitauzwa Kufidia Deni.Fahamu zaidi hapa.

MaliI zenye thamani ya Sh bilioni sita za baadhi ya wadaiwa 16, waliokwepa kulipa kodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), baada ya kutorosha kontena za mizigo yao kwenye Bandari Kavu (ICD) ya Azam mwishoni mwa mwaka jana, zimekamatwa jana na zinafilisiwa.

Aidha, mali nyingine za thamani ya Sh bilioni 7.4 zimebainishwa na muda wowote kuanzia leo zitakamatwa ili kufilisiwa kwa lengo la kulipa kodi inayodaiwa na TRA.

Hayo yalibainishwa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Udalali ya Yono, iliyopewa kazi ya kufuatilia wadaiwa hao, Yono Kevella alipokuwa akizungumzia kuanza kwa kazi ya kukamata mali za wadaiwa hao na kufilisiwa.

Kevela alisema baada ya kuisha muda wa siku 14, walioutoa kwa wadaiwa 24 kulipa madeni yao ya Sh bilioni 18.95, hadi juzi ni wadaiwa nane tu waliweza kulipa, hivyo hao 16 hawakulipa na mali zao ndio zimeanza kukamatwa na kufilisiwa.

Aliwataja wadaiwa ambao mali zao zimekamatwa na wamekubali wenyewe zifilisiwe kulipa deni hilo kuwa ni Tifo Global Trading Co Ltd wanaodaiwa Sh bilioni 1.57 na Lotai Steel Tanzania Ltd wanaodaiwa Sh bilioni 5.47.

Alisema wadaiwa hao ni wawekezaji kutoka China na wamekubali kwa hiari yao mali zao zifilisiwe kulipa deni wanalodaiwa. 

Mali zilizokamatwa na ziko tayari chini ya kampuni hiyo ya Yono ni kontena tisa za mabati, zenye thamani ya Sh bilioni sita.

"Nitumie fursa hii kuwaalika wananchi wote wanaohitaji mabati waje ofisi za kampuni yetu kununua mabati hayo, yako mengi ni kontena tisa, tunachofanya si kumuonea mtu, bali tunatekeleza wajibu wetu tuliopewa wa kuhakikisha kodi ya serikali inalipwa”, alisema Kevella.

Alisema kazi ya kukamata mali za wadaiwa wengine 14, zinaendelea na ndani ya wiki moja kazi hiyo itakuwa imekamilika na iwapo wahusika wote hawatapatikana, Kampuni ya SSB ambayo ndiyo mmiliki wa bandari kavu ya (Azam ICD) na kampuni ya wakala wa forodha ya Regional Cargo Services, watahusika kulipa deni linalobaki.

"Kwa wale tutakaoshindwa kuwapata au kukamata mali za kutosha kulipa deni wanalodaiwa, mmiliki wa bandari kavu ya Azam ICD, na kampuni ya wakala wa forodha ya Regional Cargo Services, watapaswa kulipa”, alisisitiza Kevella.

Kevella alisema jana jioni walitarajia kukamata mali nyingine za Sh bilioni 7.4 za mdaiwa Tuff Tyres General Co Ltd, ambaye amekimbilia kufungua ombi mahakamani lakini Mahakama haijatoa uamuzi.

Alisema wameshazibainisha mali za mdaiwa huyo, ikiwa ni pamoja na jengo la ghorofa, matairi na nyumba iliyopo Msasani, ambazo zote kwa pamoja zikifilisiwa zitalipa deni la Sh bilioni 7.4 anazodaiwa.

#YALIYOJIRI>>>Majina Ya Mawaziri MAJIPU Yakabidhiwa Kwa Waziri Mkuu,Ni Wale Waliogoma Kutangaza Mali Zao.Fahama zaidi hapa.

Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imemkabidhi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa majina ya baadhi ya mawaziri na naibu mawaziri ambao hawajajaza fomu za mali wanazozimiliki kama sheria inavyowataka.
 
Akizungumza jana kwenye semina ya mawaziri na naibu mawaziri, Kamishina wa Sekretarieti hiyo, Jaji mstaafu Salome Kaganda alisema viongozi hao wanajua umuhimu wake lakini wanapuuza.

“Sheria hii ya Maadili ya Viongozi wa Umma inajulikana, lakini jambo la kushangaza wapo baadhi ya mawaziri na manaibu ambao hawajajaza, kwa ruhusa yako nitakukabidhi majina yao, sisi tunafanya kazi kwa mujibu wa sheria, hivyo anayekiuka anapaswa kuadhibiwa,” alisema Jaji Kaganda bila kutaja majina hayo.
 
Kifungu cha 9 cha sheria hiyo kinataka katika kipindi cha siku 30 baada ya kupewa wadhifa, kila mwisho wa mwaka na mwisho wa kutumikia wadhifa wake kiongozi husika anatakiwa kupeleka tamko la maandishi la mali zake.
 
Sheria hiyo inafafanua kuwa mali hizo ni pamoja na rasilimali zake au mume au watoto wenye umri usiozidi miaka 18 ambao hawajaoa au kuolewa.

Alisema fomu hizo lazima zijazwe na viongozi na wananchi wanaruhusiwa kwenda kuzihakiki wakitoa sababu za msingi, lakini sheria hiyo hairuhusu waende kutangaza na wakifanya hivyo hatua zinachukuliwa dhidi yao.
 
“Hapo ndipo wananchi wengi huwa hawatuelewi kwa kuwa wanapenda kujua mali ambazo viongozi wao wanamiliki,” alisema. 

Alisema Sekretarieti kwa kutambua umuhimu wa viongozi hao kuzingatia sheria na maadili, ndiyo sababu imeandaa semina hiyo baada ya kupata ufadhili kutoka Shirika la Misaada ya Maendeleo la Marekani (USAID), wakiamini kuwa yatasaidia kuwakumbusha.

#YALIYOJIRI>>>Vigogo Watatu Wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Wafikishwa Mahakamani.Fahamu zaidi hapa.

Vigogo watatu wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), akiwemo Mtendaji Mkuu wa mradi huo, Asteria Mlambo, wamepandishwa kizimbani, kwa tuhuma za kuisababishia serikali hasara ya Sh milioni 83.5.

Mbali na Asteria, washitakiwa wengine wanaokabiliwa na mashitaka hayo ya uhujumu uchumi ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Evodius Katale, Mwanasheria Mkuu wa mradi huo, Francis Kugesha na Mkurugenzi wa kampuni ya Yukan, Yuda Mwakatobe.

Walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana na kusomewa mashitaka matatu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage.

Walisomewa mashitaka na wakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Jackline Nyantori akisaidiwa na Estazia Wilson na Stellah Mafuru.

Nyantori alidai kati ya Septemba Mosi na Oktoba Mosi 2013, Kinondoni Dar es Salaam, Asteria, Katale na Kugesha wakiwa wafanyakazi wa mradi huo, walishindwa kutekeleza majukumu yao vizuri na kuisababishia serikali hasara ya Sh milioni 83.5.

Katika mashitaka yanayomkabili Mwakatobe, inadaiwa Juni 29, 2005 katika ofisi za kodi Ilala, Dar es Salaam, alitoa taarifa za uongo kwa maofisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA), wakati akiwasilisha taarifa ya fedha ya mwaka 2004 na ya 2005 ya kampuni yake ya Yukan Business, jambo lililosababisha alipe kodi ndogo.

Awali, Wakili Nyantole alidai kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) amewasilisha hati ya kuruhusu mahakama hiyo, kusikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi hivyo washitakiwa wataruhusiwa kujibu mashitaka yao.

Washitakiwa walikana mashitaka na upande wa Takukuru ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, pia hawana pingamizi ya dhamana kwa washitakiwa.

Hakimu Mwijage alisema Asteria, Katale na Kugesha watapata dhamana endapo kila mmoja atakuwa na mdhamini mmoja anayefanyakazi serikalini au kwenye taasisi inayofahamika, atakayesaini hati ya Sh milioni 15. Pia kila mshitakiwa awasilishe Sh milioni 15 au hati isiyohamishika yenye thamani ya Sh milioni 15.

Kwa upande wa Mwakatobe, dhamana yake ipo wazi endapo atapata mdhamini mmoja mwenye barua kutoka taasisi inayofahamika, asaini hati ya Sh milioni tano.

Wote waliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti. Asteria na Katale wametakiwa kuwasilisha hati hizo Machi 3 mwaka huu. Kesi itatajwa tena Machi 9 mwaka huu.

#YALIYOJIRI>>>Basi La Mashimba Express La Kahama- Mwanza Lagongana Na Gari Ndogo Na Kuua Watu Wanne.Fahamu zaidi hapa.

Watu wanne wamefariki dunia katika ajali baada ya basi la Mashimba Express lililokuwa linasafiri kutoka Kahama kwenda jijini Mwanza kugongana na gari dogo  katika eneo la njia panda kuelekea wilayani Kishapu  Mkoani Shinyanga

Ajali hiyo imetokea jana jioni ambapo mashuhuda wa tukio hilo wamedai kuwa ilisababishwa  na  gari ndogo iliyokuwa katika mwendo kasi ambayo ilipoteza uelekeo na kisha kuligonga basi hilo.Watu  wawili  waliokuwa  katika  gari  hilo  akiwemo  dereva  walifariki  dunia  papo hapo

Mganga mfawidhi wa hospitali ya  rufaa ya mkoa wa Shinyanga Dkt Albert George Masigati amesema kati ya saa 12 na saa moja usiku wa kuamkia leo  walipokea miili ya marehemu wanne katika hospitali hiyo ,wote wakiwa ni wanaume na majeruhi wanane,kati yao wanawake wanne na wanaume wanne.

Hata hivyo Dkt Masigati amesema huenda idadi ya majeruhi ikaongezeka kutokana na taarifa kuwa baada ya ajali hiyo kutokea baadhi ya majeruhi walikimbizwa katika hospitali ya Kolandoto na Kishapu.

Dkt Masigati amesema hakuna majeruhi aliye katika hali mbaya na kwamba bado wanaendelea kuwafanyia uchunguzi .

Thursday, 25 February 2016

#YALIYOJIRI>>>Rais Magufuli Akutana Na Rais Mstaafu Wa Awamu Ya Tatu Benjamin Mkapa Pamoja Na Mjumbe Maalum Wa Rais Wa Guinea Bisau Februari 25,2016.Fahamu zaidi hapa.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia jambo wakati alipokuwa akizungumza na Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Mheshimiwa Benjamin Wiliam Mkapa Ikulu jijini Dar es Salaam Februari 25,2016
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Mheshimiwa Benjamin Wiliam Mkapa Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Genarali Omar Embalo mjumbe Maalum wa Rais wa Guinea Bissau Jose Mario Vaz Ikulu jijini Dar es Salaam. Pamoja na mambo mengine Mjumbe huyo alileta salamu za pongezi kutoka kwa Rais wa Guinea Bisau.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipokea barua kutoka Genarali Omar Embalo mjumbe Maalum wa Rais wa Guinea Bissau Jose Mario Vaz.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimshukuru Mjumbe Maalum wa Rais wa Guinea Bissau mara baada ya kupokea barua ya Salamu na pongezi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Genarali Omar Embalo mjumbe Maalum wa Rais wa Guinea Bissau Jose Mario Vaz Ikulu jijini Dar es Salaam