Umoja wa Wazalishaji Vinywaji laini umetoa msaada wa vifaatiba vyenye
thamani ya Sh10 bilioni vilivyopokelewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Vifaatiba
vilivyopokelewa jana ni pamoja na mashine za aina mbalimbali kama utra
sound, mashine za kustulia moyo, vitanda vya watoto njiti, vitanda vya
kujifungulia, vitanda 80 vya kawaida na magodoro yake, ambavyo viliwekwa
kwenye makontena 20.
“Haijapata kutokea msaada mkubwa kama
huu,” alisema Majaliwa kwenye hafla hiyo iliyofanyika kwenye ghala la
Bohari Kuu ya Dawa (MSD) iliyoko Mabibo, Ubungo jijini Dar es Salaam.
“Natoa wito kwa makampuni mengine binafsi kuunga mkono jitihada za
Serikali.”
Msaada huo wa vifaa tiba unawalenga zaidi watoto na
wajawazito, ikiwa ni jitihada za kuunga mkono juhudi za Rais John
Magufuli katika kuboresha huduma za afya.
Msemaji wa umoja huo,
Erastus Mtui kutoka Coca Cola Kwanza alisema msaada huo umelenga
kusaidia watoto na wajawazito pamoja na wagonjwa wengine kama wa moyo.
“Tumelenga
hasa vifaa vya watoto na wajawazito. Hii yote ni katika kuunga mkono
jitihada za Rais Magufuli kwani anaboresha afya na kutokomeza rushwa,
hii inayaokoa zaidi makampuni ya uzalishaji nchini,” alisema Mtui.
Akizungumza
kwenye hafla hiyo, Majaliwa alizipongeza sekta binafsi kwa kushirikiana
na Serikali kukabiliana na changamoto katika sekta ya afya.
Alisema vifaa hivyo vimekuja wakati mwafaka kwa kuwa vitawezesha vituo kutoa huduma bora za afya.
“Mtakumbuka
kwamba hivi karibuni Rais Magufuli alihamasisha maboresho ya Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili na hasa wodi ya wazazi, hatua hii mliyoichukua ya
kutoa msaada wa vifaa hivi ni sehemu ya kumuunga mkono,” alisema Waziri
Mkuu.
Alisema Serikali kupitia MSD itahakikisha vifaa hivyo
vinasam bazwa kwenye vituo husika kwa umakini mkubwa, hasa maeneo yenye
mahitaji makubwa.
Alisema tayari kuna orodha ya awali katika mikoa ya Dodoma, Geita, Katavi, Lindi, Kilimanjaro, Mara, Mbeya, Shinyanga na Tanga.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu alisema bohari imedhamiria
kusambaza dawa na vifaa tiba vya kutosha kwenye kanda nane za nchi,
lakini changamoto kubwa ni jinsi ya kuzihifadhi.
“Ukubwa wa
ghala hili la vifaa tiba ni mita za mraba 19,650 na hapa panatugharimu
kiasi cha Sh2.5 bilioni. Na iwapo tutaendelea kuhifadhi hapa,
itatulazimu kulipia Sh4 bilioni,” alisema Bwanakunu na kuongeza kuwa:
“Kwa
hiyo changamoto ni kupata eneo la kujenga ghala. Wizara ya Ardhi
ikitupatia eneo, tunategemea kuanza ujenzi mara moja.”
Wafanyakazi PSI
wasimamisha ziara
Wafanyakazi wa kampuni ya PSI walisimamisha msafara wa
Waziri Mkuu kwa kuziba barabara wakati akiondoka, wakitaka wamuambie
kero wanazokumbana nazo kazini.
Wafanyakazi hao walitoa kero zao
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kulipwa malipo kiduchu kiasi cha Sh5,750
kwa siku, huku wakinyimwa kushiriki kuchangia mfuko wa hifadhi ya jamii
wa PPF.
“Shida yetu kubwa ni mshahara. Tangu mwaka 2013
tunalipwa Sh5,750 mpaka leo na kwa miaka yote hiyo watu hawashiriki
PPF,” alisema Amini Athuman ambaye ni mfanyakazi wa PSI.
“Wote
ni vibarua, hakuna aliyeajiriwa hapa. Pia kinamama wajawazito hawalipwi
chochote wakienda kujifungua, mtu anafukuzwa kazi bila kosa lolote bosi
akiamua.”
Akijibu malalamiko hayo, Waziri Mkuu alisema
ameyapokea na kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ilishajipa kazi ya
kusikiliza kero za wananchi na wafanyakazi, lazima tatizo hilo
litatuliwe.
“Nawasihi kesho (leo) mje kazini asubuhi saa 2:00
asubuhi na Waziri ya Kazi, Jenister Mhagama atakuwa hapa kwa kuwa
mmelalamika kwamba hata makato ya PPF hayakatwi. Namsihi kiongozi
ayaandike vizuri malalamiko ili akija asome kwa umakini na utatuzi
utapatikana kesho hiyohiyo. Nawasihi msigome kufanya kazi,” alisema.
0 comments:
Post a Comment