Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akizungumza na Waganga, Wauguzi na wafanyakazi wa Hospitali ya Mkoa wa Mtwara wakati alipoitembelea Februari 29, 2016.
- Ni baada ya kudai rushwa ya sh. 100,000/- kumfanyia upasuaji mgonjwa.
- Mama alilazimika kuuza shamba ili apate fedha za kumtibia baba yake
- Aagiza maduka ya dawa nje ya hospitali hiyo yafungwe leo hii
- Amwagiza RAS aitishe kikao cha watumishi wote leo saa 9 alasiri
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameagiza kusimamishwa kazi kwa Dk. Fortunatus
Namahala wa kitengo cha upasuaji katika hospitali ya Ligula ambayo ni
hospitali mkoa wa Mtwara kutokana na tuhuma za kumdai mgonjwa rushwa ya
sh. 100,000/-.
Pia
ametoa agizo la kufungwa kwa maduka yote ya dawa yaliyo nje ya
hospitali hiyo kuanzia leo na kumtaka Katibu Tawala wa Mkoa huo, Bw.
Alfred Luanda asimamie zoezi hilo mara moja.
Waziri
Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Februari 29, 2016) kwenye kikao cha
watumishi wa hospitali hiyo alichokiitisha baada ya kutembelea maeneo
kadhaa ya hospitali hiyo na kupokea malalamiko kutoka kwa wagonjwa na
ndugu wenye wagonjwa waliolazwa.
Mara
baada ya kuwasili, Waziri Mkuu aliamua kwenda mojamoja mapokezi badala
ya wodini kama alivyopangiwa na kuuliza maswali ni kwa nini wana dirisha
moja la kupokelea wagonjwa wote. "Dirisha la wazee lipo?" akajibiwa
hakuna. "Dirisha wa watu wa Bima ya Afya (NHIF) lipo" nalo pia akajibiwa
halipo. "Je wazee wana daktari wao", hakupata jibu.
"Mganga
Mkuu ni kwa nini hujatenga dirisha la wazee wakati haya maelekezo
yalishatolewa siku nyingi? Tengeni dirisha la wazee na uhakikishe wana
daktari wao. Siyo kuwaleta huku ili waje kusukumana na wagonjwa
vijana," alisema wakati akimwagiza Mgaga Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Shaibu
Maarifa.
Akiwa
njiani kuelekea wodi aliyopangiwa kuiona, Waziri Mkuu alikutana na
kundi la wagonjwa waliokuwa wakiimba "tuna jambo, tuna jambo"
wakiashiria kutaka kusikilizwa. Kati ya wauguzaji watatu aliowasikiliza,
Waziri Mkuu alipokea kero za kuuziwa dawa kwa bei za juu kwenye maduka
ya dawa binafsi, lugha mbaya za madaktari na wauguzi, uchafu wa vyoo na
uhaba wa maji.
Lakini
kero ya Bi. Tatu Abdallah aliyelazimika kuuza shamba la baba yake ekari
2.5 ili apate fedha za kulipa gharama za kufanya upasuaji kwenye
hospitali binafsi baada ya baba huyo kutimuliwa kutoka hospitali ya
Ligula ndiyo ilimgusa zaidi Waziri Mkuu.
"Februari
mosi nilimleta baba yangu hapa nikaambiwa anatakiwa kufanyiwa upasuaji.
Nikaandikiwa ninunuue dawa za sh. 85,000/- hapo nje (pharmacy
haikumbuki jina) pia uzi wa kushonea kwa sh. 25,000/-. Lakini pia
daktari akasema anataka sh. 100,000/- ya kwake. Lakini hadi Februari 7
hakufanyiwa huo upasuaji."
"Tarehe
12 Februari baba alitolewa wodini na kuambiwa arudi tarehe 16
Februari. Niliumia sababu kijiji tunachotoka ni mbali na hali ya baba
ilizidi kuzorota. Ndipo baba akaniambia nirudi kijijini kwetu Kilomba
nikauze ekari 2.5 za shamba lake ili tulipie matibabu. Niliuza na
kumpeleka baba katika zahanati ya Sajora. Huko nililipa sh. 560,000/- na
baba akafanyiwa upasuaji sasa hivi yuko nyumbani".
"Leo
nataka huyu daktari aje achukue boksi hili la dawa alizoniandikia na
pia anirudishie hela yangu iliyopotea bure. Mie sijazitumia, ni kwa nini
aliniandikia wakati baba hajampa huduma yoyote?" Alipoulizwa kama
anaweza kumtambua akimuona, mama huyo alikiri kuwa anaweza.
Waziri
Mkuu alitembelea pia wodi ya akinamama waliojifungua na kukuta wakiwa
wametandikiwa shuka moja na wagonjwa kulazimika kuweka khanga juu ya
mipira wanayolalia wodini ambayo pia wanaambiwa wajinunulie kabla ya
kwenda hospitali kujifungua.
Akiwa
njiani kuelekea theatre, Waziri Mkuu alipata kilio cha wagonjwa wengine
ambao walisema hospitali hiyo haina maji, choo kinachotumika ni kimoja
na kwamba usafi umefanyika leo waliposikia kuwa atatembelea hospitali
hiyo.
Akiwa
katika kikao na watumishi hao, Waziri Mkuu aliwainua madaktari wote ili
wajitambulishe ndipo akamuomba mama aliyedaiwa rushwa aende kumshika
mkono daktari mhusika.
"Gwaride
la utambuzi ni jambo la kawaida. RPC hakikisha huyu mama hasumbuliwi.
Lakini leo nitaanza na huyu Daktari kwa sababu rushwa haivumiliki. RAS
simamia suala lake lakini pia shirikiana na TAKUKURU na Polisi kufanya
uchunguzi wa jambo hili hadi mwisho," alisema.
Kuhusu
madai na stahili za watumishi, Waziri Mkuu amemwagiza RAS, RMO na Afisa
Utumishi wa mkoa wafanye kikao na watumishi wote wa hospitali hiyo leo
saa 9 alasiri na kisha wamletee taarifa.
Kabla
ya kufikia uamuzi wa kumsimamisha Dk. Namahala, Waziri Mkuu alitumia
muda mwingi kuwaelezea watumishi hao jinsi walivyo na umuhimu katika
huduma zao na kwamba nafasi yao ni nyeti kwa maisha ya binadamu hivyo
wanapaswa kuwa na huruma na siyo kuwaumiza wananchi wa kipato cha chini
ambao hawana uwezo wa kumudu gharama za matibabu.
Aliwataka
waache tabia ya kuwatoza fedha watoto wanaolazwa hospitalini hapo na
wanawake wanaojifungua kwani wanapaswa kutibiwa bure kwa mujibu wa sera
ya Serikali.
Sakata
la hospitali ya Ligula lilianza juzi (Jumamosi, Februari 27, 2016)
wakati Waziri Mkuu akiwahutubia mamia ya wakazi wa Mtwara kwenye mkutano
wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa mashujaa ambapo baadhi yao
walikuwa wakichomekea kuwa aende hospitalini hapo kwa kuwa kuna majipu
ya kutumbua.
Waziri
Mkuu aliwajibu kuwa amesikia ujumbe wao na ataenda huko lakini
alishindwa kutokana na ratiba za siku hiyo kumalizika jioni sana.
Waziri Mkuu amerejea Jijini Dar es Salaam mchana huu.
0 comments:
Post a Comment