Mbunge
wa Viti Maalumu, mkoani Singida Jesca Kishoa(CHADEMA), amesema
aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe na Katibu Mkuu
wake, wanapaswa kufikishwa mahakamani katika sakata la mabehewa mabovu.
Akizungumza
jana jijini Dar es Salaam, Kishoa alisema viongozi hao, pia aliyekuwa
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha wakati huo, naye afikishwe mahakamani kwa
sababu ndiye alikuwa mlipaji Mkuu wa Serikali.
Alisema
ni aibu Kiti cha Spika kumfukuza mbunge bungeni akidaiwa kuzungumza
uongo kabla ya kudai ripoti ya mabehewa ili kujua ukweli wa jambo hilo
ni upi.
Aliongeza
kuwa, Katibu Mkuu huyo alilipa fedha asilimia 100 kinyume cha sheria
wakati Dkt. Mwakyembe ambaye kwa sasa ni Waziri wa Katiba na Sheria,
aliruhusu mabehewa yanunuliwe.
"Aliyekuwa
Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi naye awajibishwe kwa kosa hilo kama
Mtendaji Mkuu wa Wizara...mabehewa hayo yalipokewa kwa mbwembwe lakini
kasoro zake zinatokana na zabuni ya utengenezaji wake kutozingatia
viwango.
"Kampuni ya Hindustan Engineering haikufanyiwa uchunguzi kuhusu rekodi na uwezo wake, malipo yalifanyika kwa asilimia
100 kabla ya mabehewa hayajawasili nchini," alisema.
Alisema
umma unashuhudia baadhi ya vigogo wa TRL wanafikishwa mahakamani
kutokana na sakata la mabehewa hayo na kusisitiza sheria ichukue mkondo
wake kwa wote waliohusika si kuwashtaki wachache wakati Mawaziri
wanaachwa.
Kishoa
ambaye ni Mke wa aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini David Kafulila
(NCCR-Mageuzi), alisema hakuna mtu mwenye uhakika kwamba mabehewa mabovu
ni 25 kati ya 275.
"Nani
ana uhakika kwamba waliokamatwa ndio wanahusika peke yao, haiwezekani
Serikali ikajichunguza yenyewe, kujishughulikia yenyewe kwa kuamua nani
imtoe kafara, nani imlinde wote, wote washtakiwe kama ilivyo kwa
wengine," alisema Kishoa.
Kishoa
alihoji kwanini ripoti ya mabehewa inaendelea kufichwa na haifikishwi
bungeni ili Bunge liweze kuisimamia Serikali jambo ambalo halitoi picha
kwa Bunge la 11.
0 comments:
Post a Comment