Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amesema hakuna
sababu za msingi za kurejewa kwa mazungumzo ya kutafuta muafaka wa
mkwamo wa uchaguzi mkuu wakati Zec tayari imetangaza kufanyika uchaguzi
wa marudio Machi 20, mwaka huu.
Balozi
Seif ametoa msimamo huo wa serikali alipokuwa akizungumza na waandishi
wa habari kwenye Uwanja wa Ndege wa Pemba baada ya kumalizika kwa ziara
yake ya siku tatu Kisiwani Pemba jana.
Alisema
mazungumzo ya pamoja kati ya Rais wa Zanzibar, Dk. Shein na Katibu Mkuu
wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad, kuhusu kufutwa
kwa uchaguzi mkuu yalifanyika kwa maombi ya Maalim Seif na kwamba
mwishowe yeye binafsi akaamua kujiondoka kwenye maendeleo ya vikao vya
mazungumzo hayo.
"Kinacholikabili
taifa kwa wakati huu ni suala la marejeo ya uchaguzi si njia nyingine,
walioamua kutoshiriki uchaguzi huo wa marudio ni vema wakabakia nyumbani
ili kutoa fursa kwa wenzao kushiriki kwa kutumia haki yao ya
kidemokrasia kuwachagua viongozi wanaowataka," alisema.
Balozi
Seif alisema hata kwa upande wake anaheshimu maamuzi ya Zec ambayo
hayawezi kuingiliwa na chombo chochote licha ya kwamba tayari alikuwa
ameshashinda Jimbo la Mohanda na kupewa cheti kinachothibitisha kuwa
mwakilishi wake.
“Tupo
tuliokwishashinda kwenye chaguzi zetu za majimbo na kupewa vyeti
vinavyotuthibitisha, lakini baadhi yetu kwa nini tuendelee kushutumu
maamuzi ya tume ambayo kutokana na sababu za msingi imeeleza
kulijitokeza dosari kadhaa kwenye zoezi zima na kulazimika kufuta
matokeo na uchaguzi wote,” alisema Balozi Seif.
Akizungumzia
uvumi uliojitokeza wa kuwapo kikundi cha vijana wanaopiga watu katika
badhi ya maeneo maarufu kama 'Mazombi', Balozi Seif alisema hana taarifa
yoyote iliyomfikia akiwa kama kiongozi wa juu wa serikali kuhusu shutma
hizo.
Hata
hivyo, alitoa agizo kwa vyombo vya ulinzi kufanya uchunguzi dhidi ya
shutuma hizo na pale itakapobainika kuwapo kwa vitendo hivyo, juhudi za
kuwakamata wahusika zichukuliwe na kuwafikisha mbele ya sheria.
0 comments:
Post a Comment