Sunday, 14 February 2016

#YALIYOJIRI>>>ACT-Wazalendo Wapinga Uchaguzi wa Marudio Zanzibar,Wamtaka Rais Magufuli Afute Posho za Makalio Na Matumizi Ya Magari Ya Anasa.Fahamu zaidi hapa.

Maazimio Ya Kamati Kuu Ya ACT-Wazalendo Kufuatia Kikao Chake Kilichofanyika Jumamosi 13 Februari 2016 Katika Hoteli Ya Kagame Jijini Dar Es Salaam

Kamati Kuu ya Chama cha Wazalendo (ACT-Wazalendo) ilifanya kikao chake cha kawaida siku ya Jumamosi tarehe 13 Februari 2016 katika Ukumbi wa Hoteli ya Kagame Jijini Dar es Salaam. 

Pamoja na mambo mengine, Kamati Kuu ilijadili, kutolea maoni na kuazimia mambo yafuatayo yanayohusu chama na Taifa kwa ujumla.

1. Kamati Kuu ilijadili na kuzingatia hali ya kisiasa nchini na kutolea maoni mambo yafuatayo:

a. Kamati Kuu iliwapongeza wananchi na Tume ya Taifa Uchaguzi (NEC) kwa kufanikisha uchaguzi mkuu kwa amani kwa upande wa Jamhuri Muungano wa Tanzania. Hata hivyo, Kamati Kuu inalaani kitendo cha Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar za kuvuruga zoezi la kukamilisha kujumlisha matokeo ya kura zilizopigwa katika uchaguzi huo.

b. Kamati Kuu ilipokea na kujadili utendaji wa serikali ya awamu ya tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais John Pombe Joseph Magufuli na kuzingatia yafuatayo:

i. Kamati Kuu imetambua jitihada za serikali ya Dk Magufuli katika kupambana na rushwa na ufisadi nchini kupitia dhana ya kile anachokiita ‘kutumbua majipu’. Hata hivyo, Kamati Kuu imezingatia kuwa bado hali ya maisha ya wananchi imeendelea kuwa ngumu kama inavyothibitishwa na kuendelea kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu kwa maisha ya binadamu kama vile sukari, mchele, na mafuta ya kula. Aidha, pamoja na bei ya mafuta kuendelea kushuka kwa kasi katika soko la mafuta duniani, bei ya mafuta hapa nchini imeshuka kwa kiwango kidogo kisicholingana na kiwango cha kushuka katika soko la dunia.

ii. Pamoja na kwamba chama chetu kinaunga mkono juhudi za kuwachukukia hatua za kinidhamu watumishi wa umma wenye tuhuma za rushwa na ubadhirifu wa mali za umma, tunasisitiza kwamba juhudi hizo lazima zifanywe kwa kuzingatia misingi ya utawala wa sheria, utawala bora na utu.

Aidha, serikali ya Rais Magufuli haijajikita katika kuleta mabadiliko ya kimfumo, ikiwemo: kubadili mikataba ya kinyonyaji ya raslimali kama vile madini na mafuta; kufuta posho za makalio katika mfumo wa utumishi wa umma ikiwemo Bunge; kuachana na matumizi ya magari ya anasa (mashangingi); tunaendelea kuagizi sukari nje; hakuna mpango wa kuifanyia mabadiliko TAKUKURU; na serikali haielekei kama itashughulikia suala la Katiba Mpya ambayo ndiyo ajenda kubwa kwa miaka mingi sasa.

2. Kamati Kuu imepokea na kujadili hali ya kisiasa katika visiwa vya Zanzibar na kuzingatia na kuazimia yafuatayo:

a. Kamati Kuu imeendelea kusisitiza kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Ndugu Jecha Salumu Jecha, hakuwa na uhalali wa kisiasa, kikatiba na kisheria kufuta zoezi lililokuwa linaendelea la kuhesabu kura mnamo tarehe 28 Oktoba 2015.

Dalili zote za kisiasa zinaonyesha kwamba Ndugu Jecha alichukua hatua alizochukua kwa shinikizo na/au mapenzi ya kisiasa kwa lengo la kuzuia ushindi wa chama kimojawapo ulioelekea kuwa dhahiri.

Kamati Kuu imezingatia pia kuwa, mbali na Chama cha Mapinduzi, waangalizi wote wa uchaguzi wa ndani na nje, pamoja na Jumuiya ya Kimataifa, ikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki, wametamka bayana kwamba uchaguzi wa Zanzibar ulifanyika katika mazingira ya haki, huru na demokrasia na matokeo ya uchaguzi huo yalizingatia utashi na matakwa ya wapiga kura wa Zanzibar.

Kwa kuzingatia haya, Kamati Kuu imeazimia yafuatayo:

i. Kupinga marudio ya uchaguzi uliopangwa kufanyika tarehe 20 Machi 2016 na kwamba Chama chetu cha ACT-Wazalendo hakitashiriki katika uchaguzi huo

ii. Kutoa wito maalumu kwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kuchukua hatua stahiki kwa mamlaka aliyepewa kikatiba kuhakikisha kwamba Umoja na Amani ya Taifa inaendelea kuimarika nchini kwa kuzingatia misingi ya demokrasia, utawala wa sheria na utawala bora.

iii. Kamati kuu ya ACT-Wazalendo,inataka madiwani na wawakilishi walioshinda na kutangazwa rasmi na ZEC katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 25/2015 watambuliwe na waanze kuwatumikia wananchi.
 
Kwa sababu wawakilishi na madiwani waliotangazwa na ZEC ni halali kwa mujibu wa katiba, sheria na kanuni za Uchaguzi wa Zanzibar

iv. Kamati Kuu inaamini kwamba suluhu ya mkwamo wa kisiasa Zanzibar ni kufanya mazungumzo yatakayojumuisha wadau wote muhimu katika mchakato wa uchaguzi wa Zanzibar. Hatuamini kwamba mkwamo huu utatuliwa kwa vitisho vya kidola.

3. Kamati Kuu imepokea, kujadili na kupitisha taarifa ya uchaguzi wa chama na kuzingatia yafuatayo:

a. Kamati Kuu imewapongeza na kuwashukuru wananchi waliojitokeza kupiga kura na kukiunga mkono chama na hata kufanikiwa kumpata mbunge mmoja, madiwani 41 katika mikoa mbalimbali, na kuongoza Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji

b. Kamati Kuu imepitisha taarifa ya mapato na matumizi katika uchaguzi mkuu ambapo chama kilipokea na kutumia shilingi 656,625,000/=.Taarifa hii inawekwa wazi kwa umma kama tulivyoahidi kwa kuzingatia tunu yetu ya uwazi

c. Kamati Kuu imevipongeza vyombo vya habari kwa kazi kubwa waliofanya katika kuwaelimisha wananchi kuhusu uchaguzi mkuu na kwa kufanya kazi kwa weledi na bila ubaguzi

4. Kamati Kuu imejadili na kupitisha Mkakati wa Chama kwa kipindi cha miaka mitano 2016-2020.

Mkakati huu unalenga kukiimarisha chama katika maeneo matano yafuatayo:

i) Kuimarisha safu ya uongozi na watendaji katika ngazi zote
ii) Kuimarisha mfumo wa mawasiliano ya ndani na kwa umma
iii) Kuibua na kushiriki katika miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi kwa kuwashirikishi wananchi
iv) Kuimarisha mahusiano na vyombo vya habari
v) Kujiandaa kikamilifu na kimkakati kwa chaguzi za serikali za mitaa wa mwaka 2019 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, na chaguzi ndogo zitakazojitokeza.

5. Ili kutekeleza kikamilifu Mkakati wa Chama, pamoja na hatua zingine, Kamati Kuu imeziunda upya Kamati za chama makao makuu kama ifuatavyo:

i) Kamati ya Fedha na Miradi ya Kujetegemea
ii) Kamati ya Utafiti, Sera na Mipango
iii) Kamati ya Uadilifu, Ulinzi na Usalama wa Chama
iv) Kamati ya Katiba, Sheria na Mambo ya Nje
v) Kamati ya Itikadi, Mawasiliano na Uenezi
vi) Kamati ya Maendeleo ya Jamii
vii) Kamati ya Mafunzo na Chaguzi
viii) Kamati ya Wabunge na Uendeshaji wa Serikali za Mitaa

Kamati kuu imeiagiza sekretariet ya chama kuanza utekelezaji wa mpango mkakati, ili kukiandaa chama kwa Uchaguzi ujao na uchaguzi mbali mbali

Pia kamati kuu inawahimiza wanachama waendelee na juhudi za ujenzi wa Chama na kutunza amani ya nchi.

Zitto Ruyagwa Kabwe
Kiongozi wa Chama
14/02/2016

0 comments:

Post a Comment