Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya wanafunzi
32 wa darasa la saba, walimu 2 na dereva wa gari la shule ya msingi
iitwayo Lucky Vicent ya Arusha vilivyotokea leo saa 3 asubuhi baada ya
gari walilokuwa wakisafiria kupata ajali katika eneo Rhotia Marera,
Wilaya ya Karatu Mkoani Arusha.
Wanafunzi
na walimu hao walikuwa wakitoka shuleni kwao kwenda shule ya msingi
iitwayo Tumaini kwa ajili ya kufanya mtihani wa ujirani mwema na
walipofika katika eneo la Rhotia Marera basi walilopanda liliacha njia
na kisha kutumbukia korongoni ambako limesababisha vifo hivyo na
majeruhi watatu.
Kufuatia
ajali hii, Mhe. Rais Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa
Mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo na kueleza kuwa ajali hiyo imezima ndoto
za watoto waliokuwa wakijiandaa kulitumikia Taifa na imesababisha
uchungu, huzuni na masikitiko makubwa kwa familia za marehemu na Taifa
kwa ujumla.
“Ndg
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo naomba unifikishie pole nyingi
kwa wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wote wa wanafunzi, walimu na dereva
waliopoteza maisha, hiki ni kipindi kigumu kwetu sote, na uwaambie
naungana nao katika majonzi na maombi.
“Muhimu
kwa sasa tuwaombee marehemu wote wapumzishwe mahali pema, majeruhi
wapone haraka na wote walioguswa na msiba huu wawe na moyo wa subira,
ustahimilivu na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu” Amesema Mhe. Rais
Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Mei, 2017
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment