Baada ya kuahirishwa mara tatu, hatimaye Mkutano wa 18 wa wakuu wa nchi
zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), leo unaanza kwa kujadili
ajenda tano kubwa, ikiwamo inayosababisha nyufa mpya katika ujenzi wa
jumuiya hiyo.
Ni mwelekeo gani jumuiya hiyo inapaswa kuchukua, hasa baada ya
kushuhudia kusuasua kwa miradi mikubwa katika umoja huo, ni moja ya
masuala makubwa yatakayoibua mijadala mizito katika mkutano huo.
Kuna minong’ono kuwa suala la mwelekeo mpya ambao jumuiya inapaswa
kuchukua, limesababisha mvutano kiasi cha kutoelewana kwa baadhi ya
wakuu wa nchi wanachama wa EAC, ambayo miaka ya hivi karibuni imekuwa
ikishindwa kutosheleza bajeti yake.
Mkutano huo unafanyika wakati nchi wanachama zikiwa zimegawanyika kuhusu
Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Umoja wa Nchi za Ulaya (Epa).
Wakati Kenya na Uganda, kwa upande mmoja, zinasukuma kwa nguvu zote
jitihada za kuridhiwa kwa mkataba wa Epa, Tanzania inaongoza kundi
linalopinga mkataba huo.
Tanzania imeshatamka rasmi kwamba haitasaini mkataba huo ambao
unaruhusu, pamoja na mambo mengine, bidhaa kutoka nchi za Afrika
Mashariki kuingia Ulaya bila kodi.
Katika utaratibu huo pia, baadhi ya bidhaa kutoka Tanzania zitaweza
kuingia katika ukanda huo bila kutozwa kodi huku baadhi ya bidhaa kodi
ikiondolewa taratibu kwa muda wa miaka 25.
Tanzania inauona mkataba huo kuwa unaigawa jumuiya kwa ukoloni mamboleo
na kwamba utaua kabisa ubunifu, viwanda vya ndani na kugeuza ukanda huu
kuwa wa kuzalishaji malighafi. Tanzania inaamini kwa sasa hakuna
mwanachama wa EAC aliye tayari kushindana kiuchumi na nchi za Ulaya.
Septemba mwaka jana, wakuu wa EAC walikutana wakati Tanzania ikionyesha
upinzani mkali kwa mkataba huo. Ni katika mkutano huo wa 17 ndipo
walikubaliana kuwapa wataalamu wa uchumi kutoka serikali za nchi
wanachama muda zaidi wa kuwasiliana ili kuangalia upya misimamo yao na
kukutana tena Januari.
Hadi sasa hakuna dalili kwamba nchi hizo zitafikia makubaliano ya
pamoja, na tayari Bunge la Tanzania, ambalo kiutaratibu ndilo
linaloridhia mikataba yote ya kimataifa, limeshapiga kura kuizuia
Serikali kusaini mkataba huo.
Habari kutoka ndani ya vikao vya matayarisho ya mkutano huo wa 18,
zinadai kuwa suala la Epa halitarajiwi kupewa kipaumbele. Tanzania
imeendelea kusisitiza kwamba nchi za EAC zisisaini Epa mpaka faida na
hasara zake zitakapowekwa wazi.
Sudan Kusini
Suala jingine linalotarajiwa kuibua mjadala ni taarifa ya maendeleo
yaliyofikiwa katika kuiingiza Sudan Kusini katika EAC. Wakuu hao
wataamua kama wakati mwafaka umefika wa kuikubali moja kwa moja nchi
hiyo ifikapo Julai mwaka huu.
Tayari Sudan Kusini imeteua wanachama wake wa kujiunga na Bunge la
Afrika Mashariki (Eala) na Mahakama ya Afrika Mashariki kama
inavyoelekezwa katika mchakato wa kuikubali nchi hiyo.
Marais hao wanatakiwa kutoa mwelekeo kama nchi hiyo inaweza ikateua
makamishna wa EAC na kutoa majina ya watakaoiwakilisha katika nafasi za
kiutendaji ndani ya sekretarieti na jumuiya.
Bajeti ya Jumuiya
Jambo jingine muhimu ni mfumo mahususi wa ugharamiaji bajeti ya Jumuiya.
Mawaziri wa jumuiya, isipokuwa Burundi, wamekubaliana kuendelea kwa
mfumo wa sasa wa uchangiaji sawa na kuweka vikwazo kwa watakaoshindwa
kulipa.
Nguo na viatu vya mitumba
Pia, katika meza ya mkutano wa leo utajadili suala la uzuiaji kwa awamu
wa uagizaji wa nguo na viatu vya mitumba, ambao unafanyika kwa miaka
mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2016.
Marais pia wanatarajiwa kuipitisha kuwa sheria miswaada mbalimbali
iliyojadiliwa na kupitishwa na Bunge la Afrika Mashariki kama wa Mfumo
wa Usimamizi wa Forodha, wa Sheria ya Matumizi ya EAC na wa Sheria ya
Matumizi ya Ziada ya EAC.
Soko la Pamoja
Wakuu hao wa nchi pia wanatarajiwa kujadili ripoti ya hatua iliyofikiwa
katika utekelezaji wa Soko la Pamoja, moja kati ya hayo ni kuzitambua
kwa pamoja hati za biashara kutoka kila nchi na suala la kuzuia kabisa
utozaji kodi mara mbili kwa kampuni zinazofanya biashara kati ya nchi
hizo.
Katika mkutano wa hivi karibuni wa Baraza la Mawaziri wa EAC liliiomba
Tanzania kuharakisha mchakato wa kupitia upya mfumo wake wa kisheria na
kumaliza mawasiliano ya ndani kuhusu ulinganishaji wa ada za vibali vya
kazi ifikapo Septemba.
Ombi hilo limekuja kufuatia uamuzi wa hivi karibuni wa Serikali ya
Tanzania kupunguza ada ya vibali vya ukaazi hadi dola 500 za Kimarekani
kutoka dola 2,000 kwa raia wa Afrika Mashariki wanaotaka kukaa na
kufanyakazi nchini.
Kenya, Uganda na Rwanda wamefuta kabisa ada ya vibali vya kazi, lakini Tanzania na Burundi hawajaridhia suala hilo.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment