Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob na Mkuu wa
wilaya hiyo, Paul Makonda wameingia kwenye mvutano kuhusu kuvuka mipaka
ya utendaji wa halmashauri hiyo.
Mvutano huo umekuja baada ya
Jacob kumtuhumu Makonda kuwa ametoa taarifa za kikao cha kamati za fedha
ya halmashauri hiyo kilichofanyika wiki iliyopita kinyume na taratibu.
“…Tena
hata kwenye kikao hakuwepo, lakini nashangaa kuona ameenda kutangaza
kwenye vyombo vya habari kuwa Wilaya ya Kinondoni inatarajia kupata dola
300 milioni za Marekani sawa na Sh600 bilioni kutoka Benki ya Dunia kwa
ajili ya miradi ya maendeleo,” alisema Jacob jana kwenye mkutano na
waandishi wa habari.
“Vikao vyote vya halmashauri ni siri… huo ni upotoshaji na Makonda anaingilia mamlaka zisizokuwa za kwake, ” alisema.
Jacob alisema halmashauri hiyo imeshindwa kufumbia macho jambo hilo kwani linaweza kuleta mvutano baadaye.
“Mimi
nalalamikiwa na wajumbe wa kamati, wanasema kwa nini taarifa za kikao
ambazo ni za siri zinatangazwa wakati bado michakato yake inaendelea?”
alihoji Jacob.
Meya huyo alisema Makonda ambaye alipewa taarifa
hizo na maofisa tarafa waliohudhuria kikao hicho, alitakiwa kuuliza
uongozi wa halmashauri kabla ya kutangaza kwa umma.
“Sasa leo ikitokea wajumbe wamegoma kupitisha maazimio kuhusu mchakato huo hizo hela atatoa wapi?” aliendelea kuhoji.
Alisema
endapo Makonda ataendelea na tabia hiyo, maofisa tarafa watazuiliwa
kuhudhuria kwenye vikao vya kamati za fedha za halmashauri hiyo.
Hata
hivyo, Jacob alisema si mara ya kwanza kwa mkuu huyo wa wilaya kuvuka
mipaka na kuingilia shughuli za halmashauri, ambazo kimsingi zinapaswa
kufanywa na meya, mkurugenzi au msemaji wa halmashauri.
Meya
huyo alisema mara ya kwanza Makonda alisema halmashauri itajenga
machinjio ya kisasa, wakati anafahamu hana uwezo wa kupata fedha za
kufanikisha mradi huo.
Jacob alisema halmashauri ndiyo yenye dhamana na kuidhinisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo.
Pili,
aliwahi kuwaita wenyeviti wa Kinondoni Leaders Club kwa ajili ya
kuzungumzia mchakato wa kuvunja maeneo ya wazi yaliyojengwa.
Alipotafutwa Makonda kueleza kuhusu madai hayo, alisema Jacob bado ni
mwanafunzi hivyo hawezi kuzungumza chochote juu ya madai hayo.
“Amechaguliwa
kuwa meya juzi tu bado mwanafunzi, hafahamu mipaka ya mamlaka yangu.
Akijifunza na kuelewa hizo kelele hamtazisikia tena,” alisema Makonda
0 comments:
Post a Comment