Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) limeufungia rasmi wimbo wa ‘Shika Adabu
Yako’ ulioimbwa na Msanii Nay wa Mitego kutokana na ukiukwaji mkubwa wa
maadili, kashfa, uchochezi, kudhalilisha watu na kuhatarisha amani na
utengamano miongoni mwa wasanii na jamii kwa ujumla.
Sambamba
na kuufungia wimbo huo, BASATA litampa karipio kali Msanii huyo na
kumwagiza kuacha mara moja kujihusisha kwa namna yoyote na tabia ya
kuutangaza wimbo au kuusemea katika vyombo vya habari vinginevyo hatua
kali zaidi na za kisheria zitachukuliwa.
Ieleweke
kwamba kwa mujibu wa kifungu cha 4 (1) (j) cha sheria ya BASATA namba
23 ya mwaka 1984, Baraza limepwa mamlaka ya kuratibu na kufuatilia
mienendo ya mtu yeyote anayehusika na kazi za Sanaa na kuhakikisha
linalinda maadili ya kitaifa miongoni mwa Wasanii wanapokuwa jukwaani au
wanapobuni kazi yoyote ya Sanaa.
Aidha,
kifungu cha 4 (2) cha sheria hii kinalipa Baraza nguvu ya kisheria
kufanya jambo lolote lile kuliwezesha kufanya majukumu yake kwa faida na
ustawi wataifa.Baraza la Sanaa la Taifa limekuwa likipokea simu za
maswali na malalamiko kadhaa kutoka kwa waandishi wa habari na wadau wa
Sanaa ambao kwa njia moja ama nyingine wameguswa na kuchukizwa na kazi
hiyo ambayo si tu inadhalilisha tasnia ya Sanaa bali inawafanya watu
makini kuanza kuhoji hadhi ya msanii, weledi na taaluma ya Sanaa kwa
ujumla.
BASATA
mara kadhaa limekuwa likikemea na kuchukua hatua kadhaa dhidi ya tabia
hii chafu ambayo ilianza kujitokeza kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa
mwaka jana wa 2015. Kukemea huku ni kwa msingi mmoja kwamba asili ya
tasnia hii ya Sanaa ni kuelimisha jamii, kukosoa pale kunapokuwa na
tatizo, kuburudisha na kujenga jamii yenye staha, umoja wa kitaifa,
mshikamano na amani.
Ni
wazi wasanii wengi wanafanya kazi zao vizuri, kwa kubuni kazi zenye
ubora, zenye kujenga jamii na zaidi zinazoburudisha rika zote kiasi cha
kuzifanya zililetee heshima taifa. Kati ya hawa wengi, kuna wachache
ambao wanaipaka matope tasnia ya Sanaa na kwa kiasi kikubwa wanaonesha
wazi kutokuwa na nia njema.
Kwa
mantiki hii BASATA halitavumilia hawa ‘wasanii’ wachache ambao wanataka
kuigeuza tasnia ya Sanaa na wasanii genge la wahuni, wasio na staha, wa
kudharaulika na waliojipanga kuibomoa jamii na kuharibu amani na
utulivu uliopo nchini.
BASATA linapenda kueleza yafuatayo:
1.Vyombo
vya habari viwe vya kwanza kuchuja maudhui ya kazi yoyote ya Sanaa
kabla ya kuingia kwenye mtego wa kuwa mawakala wa uharibifu wa jamii
kupitia kucheza kazi chafu za Sanaa. BASATA lilishaziandikia radio zote
kuzishauri kuwa na kamati za maudhui ya kazi za Sanaa lakini inashangaza
baadhi ya vyombo vya habari vinakuwa vya kwanza kushabikia nyimbo hizo
chafu na kuwapa muda mrefu wa mahojiano wasanii hao na baadaye kurudi
BASATA kuhoji uhalali wa nyimbo husika. Hii si sawa hata kidogo.
2.Serikali
ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli imejipanga
kuwajengea mazingira bora ya utendaji Wasanii wote nchini kupitia
kuboresha miundombinu ya Sera, Sheria na Kanuni. Hata hivyo, uwepo wa
Wasanii kama hawa unafanya jamii kuhoji hadhi ya wasanii, nafasi yao
katika jamii na kwa maana hiyo kukatisha tamaa juhudi za kuipa msukumo
sekta hii maana wadau wakuu ambao ni wasanii wanaanza kuoneasha kuwa
mawakala wa uharibifu wa jamii.
3.BASATA
linawataka wasanii kujiuliza mara mbili kabla ya kubuni kazi zao za
Sanaa. Wafikirie wazazi, ndugu, jamaa na marafiki zao watazipokeaje?
Wavae nafasi ya wale wanaowatukana na kuwadhalilisha, Waelewe kwamba
Sanaa si uwanja wa kutusi na kudhalilisha watu hata kidogo. Ikitokea
wale wanaotukanwa na kudhalilishwa kughafilika Sanaa itakuwa uwanja wa
vita. Hili halikubaliki.
4.Tunafahamu
kuna wasanii wamekuwa wakifanya hivyo makusudi kutafuta ‘umaarufu
uchwara’ ambao wanadhani utakuja kutokana na kuzungumziwa sana.
Tunapenda kusema wazi kwamba umaarufu hauji kwa upuuzi wa namna hiyo
unakuja kwa msanii mwenyewe kujiheshimu, kujituma, kubuni kazi bora na
zenye kulifahamu vema soko la ndani na la kimataifa.
SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI
Godfrey L. Mngereza
KATIBU MTENDAJI, BASATA
0 comments:
Post a Comment