Friday, 12 February 2016

#YALIYOJIRI>>>TAKUKURU Yawafikisha Mahakamani Vigogo 11 wa Kampuni ya Reli (TRL).Fahamu zaidi hapa.

Hatimaye vigogo 11 wa Kampuni ya Reli (TRL) waliosimamishwa kazi hapo awali wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakishtakiwa na makosa tisa yakiwemo matumizi mabaya ya madaraka yaliyopelekea manunuzi ya mabehewa mabovu 25 kinyume na utaratibu.

Washtakiwa hao ni pamoja na  Kipallo Aman Kisamfu  (Mtendaji Mkuu), Jasper Hurbert Kisiraga (Mkurugenzi Mkuu wa Ndani), Ngoso Joseph Ngosomwiles (Mhandisi Mkuu wa Mitambo), na Mathias Andrew Massae.

Wengine ni pamoja na Muungano Kaupunda, Paschal Mafikiri, Kedmon Mapunda, Felix Kashaigili, Lowland Simtengu, Joseph Syaizyagi, na Charles Ndege.

Akiwasomea mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Emillius Mchauru, Mwendesha mashtaka wa TAKUKURU, Maxilmillian Ari amesema washtakiwa walitenda makosa hayoa kati Januari 1, 2013 na Mei 31, 2014.

Maximillian alisema mshtakiwa wa kwanza Kipallo Kisamfu akiwa kama Mtendaji Mkuu alitumia vibaya madaraka yake kwa makusudi kwa kushindwa kuhakikisha mkataba wa tenda no. PA/113/2012-13/ME/G/OE/013 unatekelezwa kwa mujibu vigezo na masharti ya utoaji tenda na kukiuka kifungu cha 33(k) na 44(1) na (3) cha Sheria ya Manunuzi na kusababisha Kampuni ya M/S Hindustan Engineering and Industries Ltd kujinufaisha kutokana na mkataba huo.

Ilidawa pia kuwa mshtakiwa namba 6, Paschal Mafikiri akiwa kama Injinia Mkuu alitumia vibaya nafasi yake kwa kupitisha michoro na dizaini za mabehewa aina ya Ballast Hopper Bogie Wagons (BHB) iliyoandaliwa na Kampuni ya M/S Hindustan Ltd ambazo zilikuwa kinyume na vigezo na masharti ya mkataba katika tenda tajwa.

Mwendesha mashtaka wa TAKUKURU aliiambia mahakama kuwa washtakiwa wa pili na wa tatu (Jasper Kisanga na Mathias Massae), wakiwa kama Mhasibu Mkuu na Mhandisi Mkuu wa TRL, walitumia vibaya nafasi zao kwa makusudi kwa kuidhinisha malipo ya kiasi cha Dola za Marekani 1,280,593.75 kwenda Kampuni ya M/S Hindustan Ltd bila ya kuthibitisha ufanisi wa mabehewa 25 aina ya Ballast Hopper Bogie Wagons ndani ya muda wa uangalizi (warranty period), kinyume na Sheria ya Manunuzi.

Vilevile mshtakiwa wa 4, Muungano Kaupunda, akiwa kama Fundi Mkuu wa TRL alitumia vibaya nafasi yake kwa kuruhusu Kampuni ya M/S Hindustan Ltd kuanza utengenezaji wa mabehewa hayo 25 bila ya kujiridhisha kama vigezo na masharti vya utolewaji wa tenda hiyo vilifatwa kama inavyoainishwa na Sheria.

Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka, washtakiwa wa 4,7,8,9 na 10 kama wajumbe wa kamati ya uthibitisho na huku wakijua wanatenda kosa walitumia vibaya nafasi zao kwa kushauri na kupendekeza Kampuni ya M/S Hindustan Ltd kushinda tenda tajwa kinyume na Sheria ya Manunuzi.

Washtakiwa wote walikana mashtaka yao na mshtakiwa 3, 4, na 11 walifanikiwa kupata dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wa kuaminika watatu watakaosaini dhamana ya Shilingi Milioni Kumi kila mmoja ikiwa ni pamoja na kuwasilisha hati zao za kusafiria mahakamani.

Washtakiwa wengine 8 walirudishwa rumande kwa kushindwa masharti ya dhamana huku wengine wakiwa hawana wadhamini kabisa hadi hapo kesi yao itakapotajwa tena Februari 25, mwaka huu.

Machi 21, 2013, TRL iliingia mkataba wa kununua mabehewa hayo aina ya Ballista Hopper Bogie (BHB) kutoka Kampuni ya M/S Hingustan Engineering and Industrial Limited ya nchini India kwa ajili ya kutumika katika uimarishaji wa njia za Reli ya Kati na yaliwasili Julai, 2014.

Hata hivyo, baada ya kuanza kazi yalilalamikiwa kuwa hayakuwa na ubora unaotakiwa na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe aliunda kamati kwa ajili ya kuchunguza tuhuma hizo na kamati hiyo ilikabidhi ripoti yake Desemba 1, 2014 na Waziri huyo kuahidi kuishughulikia bodi ya zabuni ya TRL.

0 comments:

Post a Comment