1. Utangulizi
Mnamo mwezi Februari mwaka 2015, serikali ya Tanzania ilizindua sera
mpya ya Elimu na Mafunzo.
Sera hii imepanua wigo wa elimu ya msingi kwa kuiunganisha na elimu ya sekondari (hii ilikuwa ikitolewa bure na kwa lazima tangu mwaka 2001 baada ya kuanzishwa kwa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi {MMEM}).
Sera hii imepanua wigo wa elimu ya msingi kwa kuiunganisha na elimu ya sekondari (hii ilikuwa ikitolewa bure na kwa lazima tangu mwaka 2001 baada ya kuanzishwa kwa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi {MMEM}).
Tangu kuchaguliwa kwa Rais John Pombe Magufuli mwezi Octoba mwaka 2015,
utekelezaji kikamilifu wa sera hii imekuwa moja ya ahadi kuu za serikali
yake.
Rais Magufuli aliwahakikishia wazazi wenye watoto wanaosoma
katika shule za msingi na sekondari katika hotuba yake ya ufunguzi wa
bunge la kumi na moja kuwa hawatapaswa kutoa michango yoyote kuanzia mwezi
Januari mwaka 2016.
Rais Magufuli pia alibainisha kuwa fedha zote
zitakuwa zikipelekwa moja kwa moja shuleni, na kuongeza kuwa “Nina
uhakika fedha hizo zitatumika vizuri, ole wao watakao zitumia vibaya.”
Japokuwa dhamira hii ya kutoa elimu bure mpaka kiwango cha sekondari
(kidato cha nne) kwa kila mtoto wa Kitanzania ni hatua kubwa katika
historia ya nchi, lakini upatikanaji fursa za elimu siyo changamoto
pekee inayoukabili mfumo wa elimu nchini Tanzania. Juhudi zote zitakuwa
hazina maana kwa wananchi na taifa kwa ujumla iwapo watoto wanaenda
shule lakini hawajifunzi.
Hivyo basi ubora wa elimu inayotolewa ni suala muhimu pia. Ripoti ya
Uwezo ya mwaka 2014 inaonesha kuwa asilimia 19 pekee ya wanafunzi wa
darasa la 3 ndiyo walioweza kusoma hadithi ya Kiingereza ya kiwango cha
darasa la pili 4 .
Tukiangalia ufaulu wa darasa la 7 mwaka 2015, takribani asilimia 68 ya
wanafunzi waliofanya mitihani walifaulu 5 . Japokuwa hii ni ongezeko la
ufaulu kwa karibu asilimia 11, bado ni idadi kubwa ya wanafunzi
wasiofaulu ipasavyo.
Kutokana na umuhimu wa elimu katika maendeleo, na ukizingatia mabadiliko
katika sekta ya elimu yanayoendelea nchini hivi sasa, ni vyema kufahamu
mitazamo ya wananchi kuhusu mfumo wa elimu ya umma.
Wananchi wana mtazamo gani juu ya hali ya elimu iliyopo hivi sasa? Wana
maoni gani juu ya walimu wa shule za umma na ubora wa elimu wanayopatiwa
watoto wao? Je wana matarajio yapi kuwa elimu ya bure itaboresha elimu?
Je wazazi wamekuwa wakichangia fedha kiasi gani huko mashuleni, na nini
athari za kupigwa marufuku kwa michango yote ya wazazi katika elimu? Na
je fedha hizo zimetumikaje?
Muhtasari huu umebeba maoni na uzoefu wa wananchi juu ya utolewaji wa
elimu ya msingi ya umma. Tunatumaini matokeo haya yatakuwa mwanzo mzuri
wa kupima mafanikio ya utekelezaji wa sera hii mpya kwa siku za usoni.
Takwimu kutoka muhtasari huu zimekusanywa na Twaweza kupitia mpango wake
wa Sauti za Wananchi. Sauti za Wananchi ni utafiti unaofanywa kwa njia
ya simu za mkononi, wenye uwakilishi wa kitaifa. Utafiti huu
unawakilisha Tanzania Bara.
Mambo muhimu kuhusu matokeo haya:
• Asilimia 76 ya wananchi wanaamini kuwa utoaji wa elimu bure utaboresha elimu.
• Asilimia 89 ya wazazi wanasema wanatoa michango ya fedha kugharamia elimu ya watoto wao waliopo shule za umma.
• Asilimia 66 ya michango ya wazazi hulipia ulinzi, asilimia 57 majaribio na asilimia 34 madawati.
• Karibu nusu ya wananchi wanaamini michango inayokusanywa shuleni haitumiki kwenye malengo husika.
• Wananchi 8 kati ya 10 wanaamini kuwa walimu hawapendi taaluma yao.
• Nusu ya wananchi wote wanaona kuwa ubora wa elimu ya msingi umezorota
ama kubaki pale pale wakati nusu nyingine wanaona kuwa imeboreshwa. Hii
ni ndani ya miaka 10 iliyopita.
2. Mambo sita kuhusu elimu nchini Tanzania
Jambo la 1: Wananchi wana matumaini na ahadi ya elimu bure
Asilimia 97 ya wananchi wanafahamu kuhusu ahadi ya Rais Magufuli ya
kutoa elimu bure ya sekondari (kidato nne) kuanzia Januari 2016, kama
ilivyoainishwa kwenye sera mpya na ilani ya chama tawala. Vilevile,
asilimia 88 wana imani kuwa ahadi hii itatekelezwa kama ilivyopangwa.
Asilimia 76 ya wananchi wanaamini kuwa utolewaji wa elimu bure utaongeza
ubora wa elimu kwa kuboresha mazingira ya kufundishia (asilimia 55).
Pamoja na imani hiyo, asilimia 15 ya wananchi walisema elimu ya bure
haitaboresha elimu, kwa kuwa kuongezeka kwa uandikishwaji wa wanafunzi
kutatumia rasilimali (fedha) nyingi 8.
Asilimia 49 walisema wanafunzi hawatafanya vizuri kutokana na kukatazwa
kwa masomo ya ziada ambayo walimu waliyatumia kuwasaidia wanafunzi
wasiofanya vizuri huku wakijipatia kipato cha ziada. Pamoja na hayo
asilimia 22 wana hofu na upatikanaji wa vifaa vya kutosha vya
kufundishia 9 .
Jambo la 2: Asilimia 89 ya wazazi huchangia elimu ya umma
Michango imekuwa ni sehemu ya mfumo wa elimu baada ya upanuzi wa Elimu
ya Msingi kwa Wote. Asilimia 89 ya wazazi waliohojiwa walikiri kuchangia
fedha kwenye shule za umma.
Wazazi walipoulizwa kuhusu kiwango cha fedha walichochangia, asilimia 80
walisema wamechangia TZS 50,000 ama pungufu kwa mwaka, huku asilimia 8
wakichangia zaidi ya TZS 100,000 .
Michango inayotolewa kwenye shule za umma hutumika kugharamia ulinzi
(asilimia 66), majaribio (asilimia 57) na madawati (asilimia 34).
Kiwango kidogo hutumika kwenye mahafali (asilimia 4) na safari za
kishule (asilimia 4).
Utaratibu wa ugawaji wa fedha za ruzuku ni: asilimia 40 vitabu na nyenzo
nyingine za kusomea; asilimia 20 kwa ajili ya vifaa vya kuandikia
(kalamu, madaftari, penseli n.k.); asilimia 10 kwa shughuli za kiutawala
na asilimia 10 kwa ajili ya makaratasi ya mitihani na uchapishaji.
Hivyo basi, maamuzi ya kuwa ruzuku itumike vipi yanakuwa changamoto kwa
upande wa shule zenyewe, na hata hivyo, inaonekana wazi kuwa michango
hulipia vitu vingi zaidi kuliko ruzuku.
Jambo la 3: Asilimia 49 ya wazazi wanaamini michango ya wazazi haitumiki ipasavyo
Japokuwa wazazi wengi wamekuwa wakitoa michango ya ziada, asilimia 49 ya
wazazi wanaamini kuwa fedha hizo hazitumiki ipasavyo. Wazazi wa mjini
wana mashaka zaidi ambapo asilimia 57 wanasema hivyo ukilinganisha na
asilimia 44 ya wazazi wa vijijini.
Vilevile asilimia 58 ya wananchi wanaamini kuwa michango hii
haijaidhinishwa na serikali. Asilimia 89 wanaamini kuwa walimu wa shule
za umma huchangisha fedha hizo kama chanzo cha kujipatia kipato cha
ziada 11 .
Jambo la 4: Wananchi wanahusisha mafanikio ya ujifunzaji na juhudi za mwalimu
Wananchi walipoulizwa kuwa ni nini ambacho wanadhani kinachangia matokeo
ya darasa la saba kwenye jamii yao (kuwa mazuri ama mabaya), nusu yao
walihusisha matokeo na juhudi za mwalimu 12 . Asilimia 7 pekee ndio
waliotaja changamoto zinazohusiana na wazazi au wanafunzi wenyewe 13 .
Cha kushangaza ni kwamba mwananchi 1 kati ya 3 hajui nini kinachangia
matokeo ya kujifunza pindi watoto wanapohitimu elimu ya msingi.
Jambo la 5: Wananchi wanaamini kuwa walimu wanaona fahari juu ya taaluma yao lakini hawapendi kazi yao
Asilimia 93 ya wananchi wanaamini kuwa ualimu ni taaluma ambayo ndiyo
msingi wa taifa. Japokuwa asilimia 79 ya wananchi wanaamini kuwa walimu
wanaona fahari ya kile wanachokifanya, asilimia 80 wanaona kuwa walimu
hawapendi kazi zao na hufanya tu kwa ajili ya kujipatia kipato. Je ni
kwanini walimu wanaona fahari ya taaluma yao lakini hawapendi kazi yao?
Kwa mujibu wa baadhi ya wananchi, ni kutokana na mishahara pamoja na
mazingira ya kufanyia kazi. Kwa ujumla asilimia 42 ya wananchi wanaamini
kuwa walimu hawalipwi vizuri, na asilimia 34 wanaamini mazingira ya
kazi ya walimu hayawapi motisha wa kufundisha.
Haya ni maoni ya wananchi wachache (wananchi wengi wanatoa kauli
zinazokinzana), lakini yanaweza kutoa mwanga kwanini wananchi wanadhani
walimu hawapendi kazi yao.
Wananchi walipoulizwa kuhusu vitu ambavyo vinaweza kuwaongezea walimu
motisha ili kutoa elimu bora kwa wanafunzi, asilimia 56 walisema
nyongeza ya mishahara na asilimia 19 walitaja uboreshaji wa mazingira ya
kazi.
Jambo la 6: Maoni ya wananchi yanatofautiana juu ya ubora wa elimu ya msingi.
Wananchi walipoulizwa kuhusu ubora wa elimu, nusu yao waliamini kuwa
ubora wa elimu ya msingi umezorota ama kubaki vilevile kwa kipindi cha
muongo mmoja uliopita, huku nusu nyingine wakisema elimu ya msingi
imeboreshwa.
Wananchi walio wengi wanaamini njia kuu ya kuboresha elimu ya msingi ni
kwa kuweka mkazo kwa walimu. Ili kuboresha elimu wananchi wametoa
ushauri ufuatao kwa serikali: kufuatilia utendaji wa walimu (asilimia
40), kuongeza mishahara ya walimu (asilimia 19), pamoja na kuongeza
idadi ya walimu (asilimia 10). Asilimia 7 pekee ndiyo waliotaja
ushirikiano kati ya
mwalimu na mzazi kama njia ya kuwawezesha watoto kujifunza.
3. Hitimisho
Serikali mpya imejikita kwenye utoaji wa elimu bure kwa shule za msingi
na sekondari na wananchi wamekuwa na imani kubwa juu ya suala hilo.
Wananchi wanaamini kuwa utoaji wa elimu bure utatekelezwa katika muda
ulianishwa, na ubora wa elimu utaongezeka.
Wasiwasi wa wananchi unaonekana kwenye uwajibikaji wa walimu katika
kufikia kiwango cha juu cha elimu. Walipoulizwa kuhusu namna ya
kuboresha elimu ya msingi, wananchi walitilia mkazo kwenye mishahara ya
walimu, kuongezeka kwa idadi ya walimu mashuleni na zaidi ya yote
uwajibikaji
wa walimu.
Siyo wananchi pekee wanaosisitiza uwajibikaji wa walimu. Kwa mujibu wa
Davidson, ukosefu wa motisha kwa walimu ni moja ya sababu kuu
inayoathiri ubora wa elimu nchini Tanzania 16 .
Utafiti usio rasmi uliofanywa na Twaweza kwa walimu 272 unaonesha kuwa
asilimia 96 ya walimu hao hawaridhishwi na kazi zao.
Pia, mwalimu 1 kati
ya walimu watatu alisema asingechagua tena kazi ya ualimu, huku
wakitaja mazingira magumu ya kazi (asilimia 34) na mishahara midogo
(asilimia 26) kama sababu kuu. Hii inadhihirisha kuwa walimu na wananchi
kwa ujumla wana mitazamo inayofanana.
Kwa kuwa uongozi mpya umeweka mkazo suala la elimu, ni vizuri pia
ukaanza kutatua matatizo ya walimu na kuboresha mazingira ya ufundishaji
Tanzania ili kwenda sambamba na kasi ya utoaji wa elimu.
Wakati utekelezaji wa sera mpya ya Elimu ukiendelea, ni vyema kufuatilia
mabadiliko yaliyofanyika na mafanikio yaliyopatikana.
Kumekuwa na
kusitasita kuhusu dhana hii ya ‘elimu bure’ ambapo viongozi wa shule
wana mashaka na jinsi ambavyo TZS 10,000 kwa kila mwanafunzi mmoja kwa
mwaka inaweza kutosha. Mfano mmoja ni kuhusu suala la ulinzi.
Kama ilivyoelezwa hapo juu, asilimia kubwa ya michango ya wazazi kwa
mwaka 2015 imekuwa ikitumika kwenye ulinzi (asilimia 66); wakati ruzuku
inayotumwa shuleni haihusishi suala la ulinzi.
Iwapo fedha zote
zilizotengwa zitapelekwa shuleni na kuwafikia wahusika kwa kiwango
kilichopangwa, je kiwango hicho kitatosha kuhakikisha watoto
wanajifunza?
Suala jingine la msingi ni kuhusu utunzwaji wa rasilimali. Ruzuku hapo
awali zilikuwa zinapelekwa moja kwa moja shuleni mpaka mwaka kufikia
mwaka 2002 zilipoanza kupelekwa kupitia kwa mamlaka zaHalmashauri za
Wilaya na Miji.
Kwa sasa mfumo umebadilika ambapo ruzuku zinapelekwa
moja kwa moja shuleni. Tunaamini uamuzi wa kupeleka ruzuku moja kwa moja
mashuleniumechangiwa na na kutokuwepo kwa ufanisi katika mfumo
uliopita.
Kwa mfano, kati ya 2010 na 2013, kwa wastani ni TZS 2,202 pekee ndizo zilizofika shuleni kwa kila mwanafunzi.
Sera mpya ya kupeleka pesa za ruzuku moja kwa moja mashuleni unaibua
maswali kadhaa. Tutahakikisha vipi upelekaji wa pesa moja kwa moja
kwenye shule utatupa matokeo tofauti?
Je shule zina uwezo wa kusimamia rasilimali hizo vizuri; kuzuia
ubadhirifu na upotevu na kuhakikisha zinaelekezwa kwenye matumizi ya
vitu muhimu zaidi? Kuna mfumo gani uliopo kwenye ngazi ya shule,
hususani katika kuhakiki maamuzi ya matumizi?
Ili kuhakikisha tunapata thamani halisi ya matumizi katika elimu, utoaji
na matumizi ya fedha vinapaswa kuhakikiwa katika ngazi ya shule.
Kwa kumalizia, na la muhimu zaidi, utawala mpya umeonekana kuwa kimya
kwenye suala la kuboresha matokeo ya ujifunzaji. Ongezeko la shule za
msingi kwa mamilioni ya watoto wa kitanzania ni mafanikio makubwa.
Hata hivyo, baada ya miaka kumi ya sera hii, tunatilia shaka anguko la
uandikishaji huo wa maelfu ya watoto pasipo kutoa fedha za kutosha, wala
kutilia mkazo suala la ubora. Je kutakuwa na walimu wa kutosha kwa
wanafunzi hawa? Tutahakiki vipi kama wanajifunza?
Kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita tumeshuhudia ongezeko kubwa la
shule za sekondari pamoja na wanafunzi huku ikiambatana na ongezeko
kubwa la idadi ya wanafunzi wanaofanya vibaya kwenye mitihani yao ya
kidato cha nne.
Je uongozi huu umejipanga kufanya nini cha tofauti
kuhakikisha kuwa Tanzania haiendelei kutengeneza wahitimu mbumbumbu?
Tutahakikisha vipi mfumo wa elimu unawapa watanzania fursa ya kuishi
maisha mazuri na kuchochea maendeleo ya nchi? Pamoja na nia njema na
maelezo mazuri ya Rais yanayotilia mkazo kwenye elimu na kutoa matumaini
mapya, ni muhimu kuzingatia kuwa ufanisi katika sekta hii muhimu
utafikiwa kwa kutumia ushirikiano na wadau wote.
Aidha, panahitaji marekebisho mapana zaidi katika mfumo wa elimu ili
kufikia malengo ya elimu bure na bora, na sio bora elimu bure!
0 comments:
Post a Comment