Tuesday, 18 July 2017

Hii kali, anayedaiwa kufariki na kuzikwa aibuka msibani.

TAHARUKI imeibuka msibani baada ya kijana aliyedaiwa kufariki dunia na kuzikwa, Seif Ramadhan (33), kuibuka wakati ndugu na jamaa zake walipokuwa wakiomboleza msiba wake.

Tukio hilo lilitokea juzi katika Mtaa wa Relini, Kata ya Kizota, Manispaa ya Dodoma.

Akisimulia tukio hilo, mjomba wa Seif aliyejitambulisha kwa jina la Idd Salum, alisema walipokea taarifa ya kifo Jumanne ya wiki iliyopita kutoka kwa rafiki yake aitwaye Seleman Kipusa, maarufu kwa jina la Babeshi, mkazi wa Mtaa wa Kizota.

Alisema kwamba Kipusa alipata taarifa za kifo hicho kutoka kwa rafiki zake Seif waliopo mkoani Morogoro ambako alikuwa akiishi.

“Tulipopata taarifa hizo, tulikubaliana na dada yangu ambaye ni mama wa Seif aitwaye Sarah Michael na kukubaliana mimi niende Morogoro pamoja na rafiki yake aitwaye Mohammed Hamisi ili tukauchukue mwili.

“Tulipofika Morogoro, tulikwenda Kituo Kikuu cha Polisi Morogoro kwa sababu wakati tuko Dodoma, tuliambiwa mwili wa ndugu yetu uliokotwa Stendi ya Msamvu, baada ya kuuawa kwa kipigo.

“Polisi walitwambia twende Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kuangalia miili ya marehemu iliyohifadhiwa huko ambapo tuliukuta mwili wa marehemu ndugu yetu.

“Nilipofunua ule mwili, cha kwanza nilichoangalia ni kovu la kichwani kwani Seif ana kovu na nilipolikuta, nikaangalia urembo aliokuwa ameuweka mkononi, nao nikaukuta na nilipoangalia miguu na mikono, mimi na mwenzangu tukaamini ni mwili wa ndugu yetu.

“Kwa hiyo, niliamua kumpigia simu dada yangu nikamwambia ni kweli mwanae amefariki, hivyo nikamtaka atume fedha za kusafirisha mwili baada ya kuwa tumeufanyia usafi,” alisema Salum.

Kwa upande wake, Sarah, alisema Seif ni mtoto wake wa tano kati ya watoto watano aliozaa.

Pamoja na hayo, alisema kabla ya taarifa hizo, mwanae huyo aliondoka nyumbani Dodoma hivi karibuni na kwenda Dar es Salaam kwa kaka yake aitwaye Chilewa William.

“Imepita kama wiki moja hivi aliponiaga kwamba anakwenda kutafuta maisha Dar es Salaam kwa ndugu yake Chilewa.

“Kwa hiyo, mwili wa marehemu ulipoletwa, tuliukagua na kujiridhisha kuwa alikuwa ni mwanangu kwani alikuwa na alama zote ninazozifahamu.

“Jambo la ajabu ni kwamba baada ya mazishi kufanyika Alhamisi wiki iliyopita, nilipokea simu kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kwamba ni Seif na yupo Dar es Saalam.

“Nilishtuka, lakini mwishowe nikawaita baadhi ya ndugu zangu na tulimuuliza maswali mengi na alipotujibu, tulibaki tumeshangaa.

“Sasa basi, tulimtumia nauli na kumtaka arudi nyumbani haraka kwani tulikuwa na msiba wake, jambo ambalo alilifanya na kufika juzi usiku,” alisema Sarah.

MAREHEMU ATINGA NYUMBANI

Akisimulia mkasa huo, Seif alisema baada ya kufika Dar es Salaam, hakwenda kwa kaka yake moja kwa moja, bali alianza kuishi mitaani akitafuta namna ya kuanza maisha.

“Nilipofika Dar es Salaam, sikwenda kwa kaka, lakini baada ya maisha kuwa magumu, nilikwenda kwa ndugu yangu huyo, aneo la Kisanga, Wazo.

“Nilipofika kwa kaka, wanaonifahamu walikimbia kwa sababu walidhani mimi ni msukule kwani walijua nimeshafariki.

“Lakini, kuna dada mmoja anaitwa Chiku ni jirani yake kaka, huyo alikuwa mvumilivu kwa sababu alinifuata na kuniambia wana taarifa nimefariki na hata kaka yangu amekwenda kwenye msiba wangu Dodoma.

“Kauli ile ya Chiku ilinitisha sana, nikabaki nashangaa, lakini wakati naongea naye, alikuwa amejaa hofu ingawa nilimwambia asinikimbie kama wenzake,” alisema Seif.

Kutokana na hali hiyo, alisema alimuomba Chiku atumie simu yake kuwasiliana na mama yake Dodoma, jambo ambalo lilimtisha sana mama yake.

“Mama alishtuka, aliniuliza maswali mengi na baadaye akampa siku kaka yangu Chilewa, naye akashangaa, hapo hapo nikagundua ni kweli nimezushiwa kifo.

“Ili waridhike kwamba ni mimi, walinitumia nauli ya Sh. 40,000 ili nisafiri kurudi Dodoma, Jumapili. Nilipofika nyumbani majira ya saa tatu usiku, nilikuta watu wengi sana sijawahi kuona.

“Wengine walikuwa wakinipa pole, wengine walikuwa wakilia na wengine walikuwa wakinishikashika utadhani wameona kitu cha ajabu,” alisema Seif.



DIWANI AZUNGUMZA

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kizota, Jamal Yaled (Chadema), alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kusema limewashtua wananchi wa kata yake.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Relini Kizota, Omary Bangababu (Chadema), alisema tukio hilo ni kati ya matukio yaliyowahi kuwatisha wananchi.

Download  Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa

                            Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
                       Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
                       Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa

0 comments:

Post a Comment