Waziri
wa Nishati na Madini wa zamani Ngeleja ni mmoja kati ya watu waliopokea
mgawo wa fedha zinazodaiwa kuwa zao la kashfa ya Tegeta Escrow, lakini
akatangaza kuzirejesha kwa TRA Jumatatu iliyopita.
Februari
2014, Ngeleja ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Sengerema (CCM) aligaiwa Sh.
milioni 40.4 na mfanyabiashara maarufu James Rugemalira ambaye mwanzoni
mwa mwezi alifikishwa mahakamani akikabiliwa na mashtaka 12, yakiwamo
ya kughushi na utakatishaji fedha.
Hata
hivyo, wakati Ngeleja akithibitisha kwa risiti mbele ya waandishi wa
habari kuziingiza fedha hizo katika akaunti ya TRA, mamlaka hiyo imesema
haizitambui. TRA imesema haina mpango wowote wa kufuatilia fedha hizo
kwa sababu shughuli yake ni kukusanya kodi.
Akizungumza
na Nipashe mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma wa TRA,
Richard Kayombo alisema mamlaka hiyo inahusika na kuhakikisha serikali
inakusanya kodi stahiki na siyo urejeshaji wa fedha za kashfa kama
Escrow.
Kayombo
alitoa ufafanuzi huo wakati alipoulizwa na Nipashe juu ya utaratibu
rasmi uliopo wa urejeshaji wa fedha hizo endapo wanufaika zaidi wa mgawo
wa Rugemalira watataka kufuata nyayo za Ngeleja.
Akifafanua
zaidi juu ya suala hilo, Kayombo alisema TRA haihusiki na fedha
zilizochotwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow kwa kuwa hazikuwa mali
yake.
Aidha,
Kayombo alisema TRA haiwezi kuzizungumzia fedha hizo kwa kuwa
hazijawahi kuwa mali yake na kuelekeza watafutwe wenye fedha hizo kwa
ufafanuzi zaidi.
“Fedha za Escrow zinaihusu vipi TRA? Tunawezaje kukaa na kuzungumzia fedha ambazo si zetu?” Alisema Kayombo. “Mimi nashauri watafutwe wenyewe wazungumze kama wanataka kurejesha… siyo sisi.”
Rais
wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu aliiambia Nipashe
wiki iliyopita kuwa uamuzi wa Ngeleja kupeleka fedha za hizo TRA unazua
maswali zaidi kwa kuwa alipewa na Rugemarila, na viongozi wa awamu ya
nne ya serikali walisema siyo za umma bali mtu binafsi.
Lakini
akizungumza jijini Jumatatu iliyopita Ngeleja alisema amerejesha mgawo
huo kwa TRA kwa kuwa pamoja na sababu nyingine, ili kujiweka kando na
kashfa.
Alisema aliyetoa mgawo huo ameshakamatwa na Takukuru na ana kesi inayoendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Huku akionyesha stakabadhi ya malipo ya Benki ya CRDB tawi la Tower, Ngeleja alisema pia “nimeamua
kurejesha fedha hizi hata kama aliyenipa msaada bado ni mtuhumiwa, kwa
vile hajathibitika kupatikana na hatia, kwa sababu sitaki kuwa sehemu ya
kashfa au tuhuma hizo.”
“Nimesononeshwa na kufadhaika sana kuona kuwa msaada niliopewa sasa unahusishwa na tuhuma.”
Alisema
alipokea mgawo huo Februari 12, 2014 na Januari 15, 2015 alilipa kodi
kwa TRA kiasi cha Sh. 13,138,125 ikiwa ni sawa na asilimia 30 ya msaada
huo aliopewa.
Hakusema ni kwa nini ulipita muda mrefu kati ya kupokea na malipo ya kodi.
MASHTAKA 12
Rugemalira
na mwenzake, mmiliki wa Kampuni ya Pan African Power (PAP), Harbinder
Singh Sethi walisomewa mashtaka 12 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu Julai 3.
Mashtaka
hayo ni pamoja na ya kugushi, utakatishaji fedha na kusababisha hasara
ya dola zaMarekani milioni 22.1 na Sh. bilioni 309.4 kwa serikali.
Novemba
26, 2014, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliwasilisha
mjini Dodoma ripoti ya uchunguzi wa kashfa Tegeta Escrow ambapo ilisema
Sh. bilioni 306 zilichotwa kutoka Benki Kuu kinyume cha sheria.
Mwenyekiti
wa kamati hiyo wakati huo, Zitto Kabwe alisoma ripoti na
kulithibitishia Bunge kwamba viongozi na wafanyakazi wa Serikali,
wafanyabiashara, viongozi na taasisi za dini, mabenki na watu binafsi
walihusika katika ufisadi.
Ripoti
ya PAC ilianika orodha ya waliopata mgawo huo kuwa mbali na Ngeleja ni
aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna
Tibaijuka na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa zamani, Andrew Chenge ambao
kila mmoja alipata Sh. bilioni 1.6.
Wengine
ni ofisa katika Ofisi ya Rais wakati huo, Shabani Ngurumo aliyepewa Sh.
milioni 80, Jaji wa Mahakama Kuu, Eudes Ruhangisa alipata Sh. milioni
404.25 na aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Shirika la Ugavi wa Umeme
(Tanesco), Dk. Enos Bukuku, aliyepewa Sh. milioni 161.7.
Katika
ripoti hiyo Waziri wa Nishati na Madini wa serikali ya awamu ya tatu,
Daniel Yona, Mbunge wa zamani wa Sumbawanga Mjini, Paul Kimiti,
aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Emmanuel Ole Naiko na
Jaji wa zamani wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Aloisius Mujulizi walitajwa
kupatiwa Sh. milioni 40.4 kila mmoja.
Wengine
ni ofisa wa TRA, Lucy Apollo Sh. milioni 80.8, aliyekuwa Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Usajili wa Vizazi na Vifo (Rita), Philip Saliboko Sh.
milioni 40.2, maaskofu Methodius Kilaini Sh. milioni 80.9 na Eusebius
Nzingirwa Sh. milioni 40.4, Padri Alphonce Twimannye Sh. milioni 40.4,
maofisa wa Rita Placidus Luoga Sh. milioni 121.2 na Theophil Rugozobwa
Sh. milioni 323.4.
BAJETI WIZARA
Mgawo
waliopata wabunge, maofisa wa serikali na viongozi wa dini kutoka kwa
Rugemalira unatosha bajeti ya mwaka mzima ya miradi ya maendeleo ya
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Nipashe imegundua.
Katika
miaka mitatu iliyopita ya bajeti (2014/15, 2015/16 na 2016/17), wizara
hiyo ambayo kwa sasa iko chini ya Waziri Dk. Harrison Mwakyembe,
ilitengewa bajeti ya Sh. bilioni tatu kila mwaka, ikiongoza wizara zote
18 kwa kuwa na bajeti ndogo zaidi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya
maendeleo.
Wakati
wizara hiyo ikiambulia Sh. bilioni moja (theluthi ya bajeti yake ya
maendeleo) hadi inapofika robo tatu ya mwaka wa bajeti katika miaka hiyo
mitatu, imebainika Sh. bilioni 4.77 zinazodaiwa zao la kashfa ya
uchotwaji wa fedha kwenye akaunti ya Tegeta Escrow walizopatiwa
waheshimiwa hao zingetosha kugharamia kikamilifu miradi ya maendeleo ya
wizara hiyo kwa mwaka mzima na ‘chenji’
ya Sh. bilioni 1.7 ikabaki.
Katika
mwaka uliopita wa fedha, kwa mfano, kati ya Sh. bilioni tatu
zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wizara
hiyo, ni Sh. bilioni 1.19 tu (asilimia 40) ndizo zilizokuwa zimetolewa
hadi Aprili 30, mwaka huu kwa mujibu wa Dk. Mwakyembe.
Chanzo: Nipashe
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment