ZIMEBAKI saa 72 kuanzia leo zenye umuhimu mkubwa kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Hali hiyo inatokana na taarifa kuwa kiongozi huyo ataripoti polisi siku ya Alhamisi ambako huko itajulikana kama ataendelea kuhojiwa na jeshi hilo kuhusiana na tuhuma za kutoa kauli ya uchochezi, kuachiwa huru au kufikishwa mahakamani. Siku moja ina saa 24, hivyo jumla ya saa 72 ndizo zinazokadiriwa kubaki kuanzia leo hadi kufikia Alhamisi.
Awali, Lowassa ambaye sasa ni mmoja wa makada muhimu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), aliripoti polisi Juni 27 mwaka huu kwa amri ya jeshi hilo kutokana na madai ya kutoa kauli ya uchochezi.
Akizungumza na Nipashe jana, Wakili wa Chadema), Peter Kibatala, alisema hatima ya Lowassa ya kuachiwa huru au kufikishwa mahakamani inatarajiwa kujulikana atakaporipoti tena makao makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam Alhamisi wiki hii.
Hiyo itakuwa ni mara ya tatu kwa mwanasiasa huyo aliyekuwa Waziri Mkuu wakati wa utawala wa awamu ya nne wa Rais Jakaya Kikwete kufika kwenye ofisi za jeshi hilo kuhusiana na madai hayo ya uchochezi.
Awali, Lowassa aliyehama Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati wa mchakato wa kumsaka mgombea urais wa chama hicho tawala katika uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2015, aliripoti kwa mara ya pili Juni 29, mwaka huu.
Lowassa ambaye alijiunga na Chadema Julai 28, 2015 na kupewa nafasi ya kupeperusha bendera ya chama hicho kuwania urais katika uchaguzi mkuu uliopita na kuungwa mkono na muungano wa vyama vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NCCR-Mageuzi, NLD na Chama cha Wananchi (CUF), anadaiwa kutoa maneno ya uchochezi wakati wa hafla ya futari iliyoandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Ukonga jijini Dar es Salaam, Mwita Waitara (Chadema).
Katika hafla hiyo, Lowassa anadaiwa kutoa kauli ya kumshauri Rais Magufuli kutafakari upya hatima ya masheikh wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu, maarufu Uamsho, wanaoshikiliwa mahabusu kwa zaidi ya miaka minne wakikabiliwa na mashtaka ya tuhuma za ugaidi.
Kwenye hafla hiyo, Lowassa anadaiwa kutamka kuwa ni jambo la fedheha kwa nchi illiyopata uhuru zaidi ya miaka 50 kuwaweka mahabusu viongozi wa dini bila kesi kusikilizwa mahakamani. Kutokana na kauli hiyo, Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai (DCI) ilimwandikia barua ya kumhitaji katika ofisi za makao makuu ya Jeshi la Polisi jijini Juni 27, mwaka huu ambako alihojiwa kwa saa nne kisha kuachiwa na kuhitajika kuripoti tena kituoni hapo siku mbili baadaye, lakini siku hiyo alipangiwa tena siku ya kuripoti ambayo ni Alhamisi ya wiki hii kwa madai kuwa upelelezi ulikuwa bado haujakamilika.
Katika mazungumzo yake na Nipashe jana, Wakili Kibatala alisema tarehe ya kuripoti kwa Lowassa kituoni hapo haijabadilika na ataitikia wito huo kama alivyoambiwa awali. Julai 2, mwaka huu, ikiwa ni siku chache baada ya Lowassa kutoa kauli hiyo, Rais Magufuli alilitaka Jeshi la Polisi kuwaweka mahabusu watu wote wanaowatetea masheikh hao ili wasaidie upelelezi.
Wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi katika mradi wa uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam wiki iliyopita, Rais Magufuli aliwaonya wanasiasa wanaowatetea masheikh hao na kuwataka kukaa kimya.
“Wanaoropoka wote wakamateni wawekeni ndani wasaidie polisi, nataka polisi mfanye kazi yenu, wajifunze kufunga mdomo wao, wataumia.
Wengine wanajitokeza hadharani kupinga, nasema wakamateni hata kama wanatembea taratibu,” alisema Rais Magufuli.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment