HAMZA TEMBA - WMU
Tanzania
imesisitiza uamuzi wake wa kuendelea na mpango wa kujenga mradi mkubwa
wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler's Gorge
Hydro Power Project) yaliyopo ndani ya Pori la Akiba la Selous mbele ya
wajumbe wa Kamati ya Urithi wa Dunia kutokana na umuhimu wake kwa
maendeleo ya Watanzania.
Akizungumza
mwishoni mwa wiki katika mkutano wa 41 wa wajumbe wa Kamati ya Urithi
wa Dunia unaoendeshwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja
wa Mataifa (UNESCO) ambao unaendelea katika Jiji la Krakov nchini
Poland, Kiongozi wa msafara huo ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya
Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi aliwaeleza wajumbe
wa mkutano huo kuwa mpango huo ulikuwepo katika ajenda ya Serikali ya
Tanzania tangu miaka ya 1960's na kwamba ukubwa wa eneo litakalotumika
kutekeleza mradi huo ni asilimia tatu tu ya eneo lote la pori hilo
ambalo lina ukubwa wa kilometa za mraba 50,000.
Aliongeza
kuwa, “Itakumbukwa kuwa mnamo mwaka 1982 wakati pori hili (Selous)
limewekwa katika orodha ya maeneo ya urithi wa dunia, Shirika la Umoja
wa Mataifa la Uhifadhi wa Asili (IUCN) liliutambua mradi huo wa
Stiegler's Gorge kutokuwa na madhara makubwa katika uharibifu wa
mazingira ukizingatia ukubwa wa pori hilo na eneo litakalotumika kujenga
mradi huo”.
Aliwaeleza
wajumbe hao kuwa, Serikali ya Tanzania inatekeleza sera ya kujenga
uchumi wa viwanda hali inayopelekea kuwa na mahitaji makubwa ya nishati
ya umeme hivyo kwa kuzingatia vyanzo vilivyopo imekuwa ni muhimu sasa
kufikiria tena ujenzi wa mradi huo kama chanzo kingine muhimu cha
nishati kuwezesha kufikia azma hiyo.
Alisema
mradi huo utaongeza uzalishaji wa umeme nchini kufikia asilimia 144.8
hivyo kuondoa upungufu wa nishati uliopo kwa sasa na pindi
utakapokamilika utawanufaisha watanzania wengi wanaoishi bila umeme
ikiwa ni pamoja na kukidhi mahitaji yake ya kuendesha viwanda.
Meja
Jenerali Milanzi alilazimika kutoa maelezo hayo kwa kamati hiyo ili
kuweka bayana dhamira ya dhati Serikali ya Tanzania ya kuendelea na
ujenzi wa mradi huo kwa ajili ya maendeleo endelevu huku akitoa rai kwao
kuwa Serikali bado ipo tayari kwa mazungumzo ya namna bora ya
kutekeleza mradi huo kwa faida ya jamii, uchumi na mustakbali bora wa
mazingira ya hifadhi ya Selous na taifa kwa ujumla.
“Kwa
kutumia teknolojia bora zilizopo, mipango imara na usimamizi thabiti,
mradi huu utakua na faida kubwa kwa taifa ikiwa na pamoja na kuboresha
maisha ya watu maskini na jamii kwa ujumla bila kuathiri mazingira
yanayotoa faida hizo”, alisema Milanzi.
Hapo
awali, kabla ya mkutano huo, ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Katibu
Mkuu huyo ulifanya mazungumzo na Maafisa Waandamizi wa Kituo cha Urithi
wa Dunia na Bodi za Ushauri ya kituo hicho na kuwasilisha kwa maandishi
msimamo wa Tanzania kuhusu ujenzi wa mradi huo.
Tanzania
ilipinga vikali rasimu ya azimio No. 41 COM 7 A.17 aya ya 7 ambalo
liliitaka kusitisha kabisa (to permanently abandon) ujenzi wa mradi wa
kuzalisha umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler's Gorge Hydro
Power Project).
Baada
ya tamko la Tanzania kupinga azimio hilo kipengele hicho kilifanyiwa
marekebisho ipasavyo na neno “to permanently abandon” (kusitisha kabisa)
liliondolewa katika azimio hilo kupisha majadiliano zaidi.
Tanzania
ni miongoni mwa nchi wanachama zilizosaini mkataba wa urithi wa Dunia
wa mwaka 1972 huku ikiwa na maeneo saba yaliyorodheshwa katika urithi
huo ikiwepo Pori la Akiba la Selous, Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro,
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Mji Mkongwe (Zanzibar), Hifadhi ya
Ngorongoro na Michoro ya kondoa na Kilwa Kisiwani. Aidha, ni mwanachama
wa Kamati ya Urithi wa Dunia kwa kipindi cha miaka minne hadi mwaka
2019.
Tokea
ijiunge na kamati hiyo mwaka 2015, Tanzania imekua na msimamo wa kuwa
na maendeleo endelevu katika ajenda za mikutano yake pamoja na miongozo
yake ili kuruhusu kuendeleza maeneo ya urithi wa dunia kuweza kufikia
maendeleo ya kijamii na kiuchumi bila kuwepo kwa athari kubwa katika
mazingira.
Mkutano
huo wa 41 wa wajumbe wa Kamati ya Urithi wa Dunia unaoendelea katika
jiji la Krakov nchini Poland umehudhuriwa na nchi wanachama 193 na
unajadili mambo mbalimbali muhimu kuhusu uhifadhi na ulinzi maeneo ya
urithi wa dunia pamoja na kutangaza maeneo mengine mapya ya urithi wa
dunia yaliyowasilishwa na nchi nyingine wanachama katika mkutano huo.
Muonekano wa mto Rufiji kutokea angani ambao maporomoko yake yatatumika kuzalisha umeme katika mradi unaotarajiwa kujengwa na Serikali wa Stiegler's Gorge
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment