Friday, 29 January 2016

#YALIYOJIRI>>>>LHRC Yaitaka Serikali Kuheshimu Haki ya Watanzania Kupata Taarifa, Yalaani Wabunge Kudhalilishwa na Mbwa wa Polisi.Fahamu zaidi hapa.

Serikali imetakiwa kuheshimu haki ya kikatiba ya kuwapa wananchi habari na taarifa muhimu zinazowahusu bila ya kujali gharama za taarifa hizo kwa kuwa ni jukumu lake kufanya hivyo.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na kituo cha sheria na haki za binadamu kupitia kwa Kaimu Mkurugenzi wake Bi. Imelda Urio na kuongeza kuwa kusitishwa baadhi ya matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya bunge kwa kisingizio cha gharama ni kitendo cha makusudi kwa kuwanyima wananchi taarifa muhimu toka kwa wawakilishi wao ambao ni wabunge.

Bi Imelda Urio ameongeza kuwa muhimili wa bunge na viongozi wake lazima wafanye kazi kiueledi na kuzuia mianya ya kuingiliwa na mihimili mingine hususani serikali.

Aidha LHRC imelaani vikali kitengo cha kuzalilishwa kwa wabunge kwa kutolewa bungeni na mbwa wa jeshi la polisi,

Kwa upande wa kaimu mkurugenzi wa utetezi na maboresho Bi. Anna Henga yeye amesema kuwa haki yoyote haina gharama na ni jukumu la serikali kulipia gharama hizo za matangazo ya bunge.

#YALIYOJIRI>>>>Zitto Kabwe: "Serikali Imekurupuka, Kuongoza Nchi Sio Kutumbua Majipu Tu".Fahamu zaidi hapa.

Mbunge wa Kigoma mjini Zitto Kabwe amefunguka na kuonesha masikitiko yake kwa kitendo cha serikali kushindwa kuleta Bungeni mpango wake wa maendeleo wa miaka mitano.

Zitto Kabwe kupitia ukurasa wake wa Facebook ameweka wazi jambo ambalo serikali inapaswa kufanya baada ya uchaguzi na kusema ni kuwasilisha mpango wa maendeleo wa miaka mitano.

"Shughuli ya kwanza ya serikali baada ya uchaguzi ni kuwasilisha mpango wa maendeleo wa miaka mitano ( kutafsiri ilani yake kwenda kwenye mpango wa utekelezaji) . Bunge linapaswa kujadili na kuidhinisha Mpango wa Maendeleo wa miaka 5 na kisha Mpango wa mwaka mmoja kuanza kutekeleza Mpango huo wa miaka 5. Kwa mujibu wa Katiba ya JMT Ibara ya 63(3)(c), Mpango wa Maendeleo wa miaka 5 hutungiwa sheria kwa ajili ya utekelezaji." Alisema Zitto Kabwe

"Leo Serikali ya Rais John Magufuli ilipangiwa kuwasilisha Mpango huo wa Maendeleo wa miaka 5. Imeshindwa. Imeleta mwelekeo wa Mpango. Haikuleta sheria na Kamati ya Bajeti Imeleta maelezo yake kuhusu Mpango wa Maendeleo wa mwaka mmoja ilhali hakuna Mpango wa Miaka 5. 

"Mwenyekiti Chenge alitaka wabunge wajadili kwa mujibu wa kanuni ya 94 ambayo kimsingi ni Kanuni inayohusu Mpango wa mwaka mmoja. Serikali imejichanganya. Uongozi wa Bunge umechanganyikiwa." Aliongeza Zitto Kabwe

Zitto Kabwe alimaliza kwa kusema kuwa ni aibu kubwa kwa serikali inayojinasibu kwa kauli ya "Hapa kazi tu"

"Bunge linapaswa kuagiza Serikali ikalete Mpango wa Maendeleo wa miaka 5 ili uidhinishwe na utungiwe Sheria kabla ya kuanza kujadili mipango ya mwaka mmoja mmoja.

"Ni aibu kubwa kwa Serikali ya ‪#‎HapaKaziTu‬ kushindwa kuleta Bungeni Mpango wake wa Maendeleo wa miaka 5 na hata ule wa mwaka wake wa kwanza. Itapangaje bajeti zake? Itatekeleza vipi ilani yake? Kuongoza nchi sio kutumbua majipu tu, ni kuendesha nchi." Alimaliza Zitto Kabwe.

Thursday, 28 January 2016

#YALIYOJIRI>>>January Makamba Atetea Uchaguzi Wa Marudio Zanzibar,Asema Watakaoleta Vurugu Damu Za Wazanzibar Zitawalilia.Fahamu zaidi hapa.

Serikali  imesema uamuzi wa kurudia uchaguzi wa urais Zanzibar ni halali na wa kisheria na kwamba wanaotafuta suluhu nje ya Katiba, wanakosea.

 Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, January Makamba alipokuwa akihitimisha majadiliano ya kuchangia hotuba ya Rais John Magufuli.

Alisema uchaguzi ulifutwa kisheria na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa Tangazo la Serikali Namba 6587. Makamba alisema Katiba ya Zanzibar, imeeleza wazi kuwa hakuna mamlaka ambayo itahoji uamuzi wa tume, hata kama ni Mahakama. Alisema akidi ilitimia wakati tume inafikia hatua hiyo.

Waziri huyo alisema wanaotaka kutumia suala hilo kuleta vurugu Zanzibar, damu za Watanzania zitawalilia. Alisema viongozi wakuu wa nchi, wamefanya kazi kubwa katika kulitafutia ufumbuzi suala hilo na hivyo ieleweke kuwa ZEC na NEC ni tume zinazojitegemea.

Alisisitiza NEC haiwezi kuingilia uamuzi wa ZEC, kwani uchaguzi wa rais uliofanyika kwa siku moja Tanzania Bara na Zanzibar, umekuwa ukiendeshwa na Tume mbili tofauti. Alisema uchaguzi huo, ulifanywa na tume tofauti na hata wino uliotumika katika chaguzi hizo ni tofauti .

Alisema wajibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kuhakikisha kuwa amani na utulivu, vinalindwa Zanzibar katika marudio ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Machi 20 mwaka huu.

Oktoba 28 mwaka jana, Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, alitoa “Taarifa Kwa Umma ya Kufuta Uchaguzi wa Zanzibar”.

Katika taarifa hiyo, Jecha Salim Jecha alisema “Mimi nikiwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, nimeridhika kwamba uchaguzi huu haukuwa wa haki na kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu za uchaguzi. Hivyo, kwa uwezo nilionao natangaza rasmi kwamba uchaguzi huu na matokeo yake yote yamefutwa na kwamba kuna haja ya kurudia uchaguzi huu”.

MAGAZETI YA LEO IJUMAA JANUARY 29 YAKO HAPA


MICHEZO YA WEEK HII MSIMAMO LIGI KUU TANZANIA BARA HIKO HAPA JIONEE.

MSIMAMO WA LIGI KUU TANZANIA BARA HUU KABLA YA MICHEZO YA HAPO JUU.

#YALIYOJIRI>>>Chadema Waungana na ACT -Wazalendo,Wadai Serikali ya Magufuli ni ya kidikteta.Fahamu zaidi hapa.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimekosa imani na serikali ya awamu ya tano kwa kuwa na matendo ya kidikteta na kwenda kinyume na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 kwa kuminya uhuru wa wananchi wa kupata habari.

Hayo yameelezwa leo Jijini Dar es Salaam, na Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu alipokuwa akizungumza na wandishi wa habari ambapo amesema kuwa serikali imekuwa ikijinadi kwa kauli mbiu ya hapa kazi huku ikiwa mstari wa mbele kwa kuwanyima haki ya msingi wananchi ya kupata habari.

Amesema kuwa matendo hayo ni pamoja na kuzuia Shirikia la Utangazaji la Tanzania(TBC), kurusha matangazo ya moja kwa moja ya mikutano ya bunge inayoendelea ,kufutwa kwa Gazeti la Mawio pasi na sababu za msingi,kuzuia vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara, na kuunda kamati dhaifu bungeni.

Amesema kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Mnauye ametoa sababu zisizokuwa za msingi ambapo alidai kuwa serikali inaepuka gharama za kurusha matangazo hayo moja kwa moja na baadala yake kurekodi vikao hivyo vya bunge kwa  kurushwa saa nne usiku.

Amesema inaonekana Waziri huyo hajafanya utafiti na kwamba ikiwa  tatizo lipo kwenye gharama alizotaja chadema ipo tayari kuchangia gharama hizo kwa kuanzisha harambee maalumu pamoja kuwataka chama cha wamiliki wa vyombo vya Habari (Moat) na Baraza la Vyombo vya Habari (MCT) kulisimamia suala hilo.

“Nape ataje gharama hizo tutachangishana ......mwenye mia moja mia mbili ili wananchi wajue mambo muhimu yanayoendela kwa wakilishi wake”,amesema Mwalimu.

Amesema Nape alikuwa anayumba kwa kuwa na ndimi mbili kwa kuongeza sababu nyingine ya kuzuia kurusha kwa matangazo hayo ni kuwa muda huo ni wa kazi na kwamba watu watakuwa hawafanyi kazi kutokana na kuangalia bunge.

Amesema kuwa hoja ya watu kutofanya kazi haina mashiko kutokana na watu huwa wanafanya kazi ilhali bunge linaendelea ambapo kama kuna hoja muhimu watu huzisikia bila kuathiri shuguli zao lakini kuna wengine muda huo sio wa kazi kwao.

Amesema kuwa serikali imekusudia kuminya uhuru wa habari kutokana na matukio yaliyofuatana ya kushugulikia vyombo vya habari.

Amesema kuwa serikali imezuia mikutano ya siasa ambapo Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa na Nape Mnauye walitoa kauli hizo walipokuwa Mkoani Lindi na baadaye Jeshi la Polisi kuweka mkazo wa suala hilo.

Amesema suala hilo hawawezi kulikubali kutokana na chama kuwa na mikutano yao kila baada ya muda na kwamba muda wa kuratibu mikutano hiyo watafanya vikao vyao.

Amesema serikali imeunda kamati dhaifu bungeni  kwa nia ya kudhoofisha shughuli za utendaji bungeni na maendeleo ya nchi kwa kuwaweka wabunge wageni kwenye kamati muhimu ilhali hawana uwezo kuzisimamia ambapo kamati ambazo hazina umuhimu kupangiwa watu wenye uwezo.

#YALIYOJIRI>>>Rais Dkt Magufuli Afanya Uteuzi Wa Naibu Gavana Wa Benki Kuu Ya Tanzania.Fahamu zaidi hapa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, amemteua Ndugu Julian Banzi  RAPHAEL, kuwa Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.

Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue imeeleza kuwa uteuzi huo umeanzia tarehe 26 Januari, 2016.

Kabla ya uteuzi huu Ndugu Julian Banzi RAPHAEL alikuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Biashara na Viwanda, Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar.

Ndugu Julian Banzi RAPHAEL anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Ndugu Juma RELI ambaye muda wake umemalizika tarehe 12 Julai, 2015.

Gerson P. Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU,
DAR ES SALAAM.
28/01/2016

#YALIYOJIRI>>>Serikali Yatangaza Mkakati wa Kuwafilisi Mafisadi na Wahujumu Uchumi.Fahamu zaidi hapa.

  Mkurugezni wa Mashtaka Bw. Biswalo Mganga
SERIKALI kupitia vyombo vyake vya dola, imetangaza kuzitaifisha mali za wote waliopatikana na hatia ya Ufisadi na Uhujumu Uchumi na kueleza kuwa utaratibu huo ndio utakaoendelea kwa watuhumiwa ambao bado kesi zao hazijamalizika au hazijapelekwa mahakamani.
 
Tangazo hilo la serikali limetolewa leo Januari 28, 2016 na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini, DPP, Bw. Biswalo Mganga, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Jeshi la Polisi(DCI), Kamishna wa Polisi, Diwani Athumani na Mkurugenzi wa Upeleelzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), wakati wa mkutano wao wa pamoja na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam.
 
Katika kuhakikisha kuwa jukumu hilo linatekelezwa, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai amesema, mwaka 2012 idara yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kwa pamoja walikubaliana kufanya kazi ya ufuatiliaji wa mali zinazohusiana na uhalifu kama sheria inavyotaka na kwa upande wa jeshi hilo tayari kitengo chake cha upelelezi wa makosa ya uhalifu wa kifedha (Money laundering) kiko kazini.
 
“Katika kutekeleza mkakatihuo, Jeshi la Polisi limekamilisha upelelezi wa kesi 23 ambazo ziliwasilishwa kwa DPP na kati ha hizo ,kesi tatu (3) zimetolewa uamuzi na nyingine ishirini ziko katika hatua ya maombi ya kupata amri ya Mahakama ili ziweze kuzuiwa au kutaifishwa (Restraint or confiscation).” Alifafanua Kamishna Diwani Athumani
 
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Upelelezi kutoka TAKUKURU, Bw. Alex Mfungo, yeye amesema, taasisi yake imeona hakuna maana yoyote kwa mhalifu wa Ufisadi na uhujumu uchumi ukamfunga gerezani na kisha kumuachia baada ya kifungo halafu aendelee kutumia mali alizochuma kwa njia za haramu.

“Tumeona njia mbadala ya kudhibiti hali hiyo na kwa mujibu wa sheria ni kumfilisi mhusika hata kama atatumikia kifungo.” Alibainisha Bw. Alex

Naye Mkurugenzi wa Mashtaka, DPP, Bw. Biswalo Mganga, yeye amesema ili kuendana na dhana ya Hapa Kazi Tu, ni lazima kukabiliana na wahujumu uchumi na Mafisadi ili hatimaye Wananchi walio wengi waweze kunufaika na rasilimali zao. 

“Natoa wito kwa nyie waandishi wa habari muujulishe umma wa Watanzania kuwa kama mtu anayo taarifa au anajua mali zinazomilikiwa na mtu isivyo halali hususan watumishi wa umma basi atoe taarifa.” Alisema
 DCI Kamishna wa Polisi Diwani Athumani
 Mkurugenzi wa Upelelezi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, TAKUKURU, Bw. Alex Mfungo
 DCI Kamishna wa Polisi Diwani Athumani
Bw. Mfungo, (kulia), akiwa na DPP, Mganga.

Breaking News>>>>>CUF Wagoma Kushiriki Uchaguzi wa Marudio Zanzibar.Fahamu zaidi hapa.

Azimio La Baraza Kuu La Uongozi La Taifa Kuhusu Tangazo La Mwenyekiti Wa Tume Ya Uchaguzi Ya Zanzibar La Kuitisha Uchaguzi Wa Marudio Zanzibar

Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi), likiwa ndiyo chombo cha juu cha maamuzi katika Chama baada ya Mkutano Mkuu wa Taifa, limefanya kikao cha dharura leo, tarehe 28 Januari, 2016, katika Ofisi Kuu ya CUF, mjini Dar es Salaam. 

Kikao hicho kilikuwa na ajenda moja tu, ambayo ni kufanya maamuzi kuhusiana na tangazo la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar la kuitisha uchaguzi wa marudio.

Baada ya kujadili kwa kina tamko hilo la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salum Jecha, la kuitisha uchaguzi wa marudio tarehe 20 Machi, 2016 na mwenendo mzima wa hali ya kisiasa Zanzibar tokea alipotoa tamko lake batili la tarehe 28 Oktoba, 2015 kudai kwamba amefuta uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na matokeo yake, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limefikia maazimio yafuatayo:

1. KWAMBA Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar umeshafanyika tarehe 25 Oktoba, 2015, ambapo kwa upande wa uchaguzi wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani ulikwisha kamilika na washindi wote kupewa shahada za kuwathibitisha na kuwatambua kama washindi halali. 

Kwa upande wa uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, matokeo yalikwisha bandikwa nje ya vituo vya majumuisho vya majimbo yote 54. Kilichokuwa kinaendelea baada ya hapo ni kuhakiki matokeo hayo kutoka majimboni na kazi hiyo ilikwishakamilika kwa majimbo 40 na katika hayo, matokeo ya uchaguzi wa Rais kwa majimbo 31 yalikwishatangazwa kabla ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jecha Salum Jecha, kutangaza isivyo halali kwamba ameufuta uchaguzi huo.

2. KWAMBA Chama Cha Wananchi (CUF) hakitoshiriki katika uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika tarehe 20 Machi, 2016 kwa sababu uchaguzi huo si halali kwani uchaguzi halali ulishafanyika.

3. KWAMBA linatoa wito kwa Wazanzibari wote wanaoipenda nchi yao na ambao wanaamini katika utawala wa sheria, demokrasia na kuheshimu Katiba na Sheria za nchi yetu kutoshiriki katika uchaguzi huo usio halali wa marudio.

4. KWAMBA sababu kuu ya Baraza Kuu kufikia maamuzi haya ni kutokana na matamko yote mawili ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salum Jecha, kutokuwa halali na kwenda kinyume na Katiba ya Zanzibar na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Nam. 11 ya 1984. 

Hakuna kifungu chochote cha Katiba ya Zanzibar au Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar kinachotoa uwezo kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na hata kwa Tume yenyewe kufuta uchaguzi au kuitisha uchaguzi wa marudio.

5. KWAMBA linazipongeza na limetiwa moyo sana na taasisi na jumuiya zote za kimataifa na kikanda zikiwa ni pamoja na Jumuiya ya Madola (The Commonwealth), Umoja wa Ulaya (European Union), Umoja wa Afrika (African Union), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na nchi za Marekani na Uingereza kwa msimamo wao wa kuungana na Wazanzibari na kutetea haki yao ya kidemokrasia na maamuzi halali waliyoyafanya katika uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na kutaka mchakato wa uchaguzi huo ukamilishwe na matokeo yake kutangazwa.

6. KWAMBA linazipongeza na kutiwa moyo pia na taasisi za hapa nchini zikiwemo taasisi na jumuiya za kidini, taasisi za haki za binadamu, vyombo huru vya habari, vyama vyengine vya siasa na Wazanzibari na Watanzania wote wanaopenda amani na demokrasia kwa msimamo wao wa kutetea maamuzi ya Wazanzibari waliyoyafanya katika uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na kuendelea kusisitiza haja ya kuheshimu na kufuata Katiba na Sheria za nchi yetu na pia haja na umuhimu wa kutunza amani ya nchi yetu kwa kutaka haki itendeke. 

Baraza Kuu linazihakikishia taasisi na jumuiya hizo zote na pia kuwahakikishia Wazanzibari na Watanzania wote kwamba CUF itaendelea kusimama kidete katika kulinda na kutetea Katiba na Sheria za nchi yetu na pia kutetea maamuzi ya Wazanzibari waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015.

7. KWAMBA limesikitishwa na kushangazwa na kitendo cha Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kuandika barua na kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kutaka vyama vya siasa vishiriki uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika tarehe 20 Machi, 2016 bila ya kujali kwamba uchaguzi huo ni haramu na unakiuka matakwa ya Katiba ya Zanzibar na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Nam. 11 ya 1984.

 Baraza Kuu halikutarajia mtu mwenye hadhi ya Ujaji kufanya kazi ya kutumikia maslahi ya watawala ambao wameamua kuvunja Katiba na Sheria za nchi yetu na kukanyanga misingi ya haki na demokrasia huku akishindwa kukemea uhuni mkubwa uliofanywa wa kubaka demokrasia na haki za watu.

8. KWAMBA limesikitishwa na kitendo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli, kukwepa dhamana na wajibu wake kama Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu kwa kuiacha njiani kazi aliyoianza ya kutafuta ufumbuzi wa mkwamo wa uchaguzi Zanzibar.

 Baraza Kuu linamtaka Rais Magufuli kujitathmini na kujiuliza anajiweka vipi na kutoa taswira gani mbele ya macho ya Watanzania na jumuiya ya kimataifa kutokana na kutosimamia ahadi yake aliyoitoa mbele ya Watanzania wakati akilizindua Bunge jipya kwamba atafanya kazi na vyama vya CUF na CCM ili kuupatia ufumbuzi mkwamo huu.

9. KWAMBA linalaani matumizi ya nguvu kubwa ya vyombo vya ulinzi na usalama vya Jamhuri ya Muungano na Vikosi vya SMZ dhidi ya wananchi wasio na hatia na ambao wamekuwa watulivu licha ya vitendo vingi vya uchokozi wa makusudi na hata mashambulizi ya hujuma dhidi yao yanayofanywa na makundi ya vijana wa CCM waliowekwa katika makambi kadhaa kisiwani Unguja.

10. KWAMBA linaitaka jumuiya ya kimataifa na hasa taasisi zinazosimamia haki za binadamu na zinazopambana na makosa ya jinai kimataifa ikiwemo Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (International Criminal Court – ICC) kufanya uchunguzi wa kauli na matendo ya uhalifu, uvunjwaji mkubwa wa haki za binadamu na ubaguzi ambao umekuwa ukifanywa dhidi ya wananchi wa Zanzibar na kuchukua hatua dhidi ya watu walio nyuma ya maamuzi na utekelezaji wa matukio hayo.

11. KWAMBA linawapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kuonesha ukomavu wa hali ya juu na kuwa watulivu licha ya machungu makubwa waliyoyapitia na wanayoendelea kuyapitia tokea pale maamuzi yao yalipopinduliwa na CCM kwa kumtumia Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salum Jecha. 

Baraza Kuu linatoa wito kwa Wazanzibari wote kuungana pamoja chini ya chama chao cha CUF walichokipa ridhaa halali kupitia uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 kutetea maamuzi yao waliyoyafanya kupitia sanduku la kura kwa njia za amani.

Baraza Kuu linawasisitiza tena Wazanzibari kwamba waendelee kutunza amani ya nchi yetu na kutambua kwamba kutunza amani si udhaifu bali ni jambo linaloipa nguvu jumuiya ya kimataifa kufuatilia haki za kidemokrasia za wananchi wa Zanzibar.

12. Baraza Kuu la Uongozi la Taifa linawatahadharisha CCM na watawala wasiowajali na kuwaheshimu wananchi kwamba zama za utawala wa mabavu usioheshimu Katiba na Sheria za nchi hazina nafasi tena katika dunia ya leo. Baraza Kuu lina imani kwamba HAKI ITASHINDA.

LIMETOLEWA NA:
BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA
THE CIVIC UNITED FRONT
(CUF – Chama Cha Wananchi)
DAR ES SALAAM
28 JANUARI, 2016

#YALIYOJIRI>>>CUF Kutoa Tamko Zito Leo Kuhusu Suala la Zanzibar.Fahamu zaidi hapa.

Baraza Kuu la Chama Cha Wananchi (CUF), leo linatarajia kutangaza uamuzi mzito kutokana na kikao cha Kamati ya Utendaji, kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam chini ya Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad.

Kikao hicho cha Kamati ya Utendaji kilifanyika kwa saa tatu kujadili suala la tarehe iliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ya kurudia uchaguzi wa Zanzibar, uliofutwa Oktoba 28, mwaka jana.

Kamati hiyo ambayo ilikuwa na ajenda moja pekee, ilijadili na  kutoa uamuzi mzito ambayo yatawasilishwa kwenye Baraza Kuu leo na kutolewa kwa umma.

Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji, ambaye hakutaka kutajwa jina , alisema kuwa maazimio yaliyotolewa na kikao hicho kilichoanza saa nne asubuhi, yataishangaza dunia.

Alisema uchaguzi uliotangazwa na ZEC kuwa utafanyika  Machi 20, mwaka huu, ni batili kwa kuwa tayari mshindi wa uchaguzi huo anafahamika ni Maalim  Seif.

“Jukumu kubwa la kikao cha Kamati Tendaji kwa mujibu wa Katiba (ya CUF) ni kuandaa ajenda kwa ajili ya kikao cha Baraza Kuu litakaloanza kesho (leo) na baada ya hapo tutatangaza msimamo wetu juu ya uchaguzi huo,” kilieleza chanzo hicho.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa CUF, Silas Bwire, Kamati ya Utendaji ilikuwa na wajumbe 18 kutoka Tanzania Bara na  Zanzibar, ambao ni viongozi waandamizi wa chama.

Baraza kuu ambalo linatarajia kufanya kikao chake leo, litakalopokea ajenda zilizojadiliwa jana, lina wajumbe 60.

Kikao cha Baraza ambacho kitaongozwa na Mwenyekiti wake, Dk. Twaha Tasilima, kitajadili kwa kina ajenda zitakazowasilishwa pamoja na kuzitolea uamuzi.


==>Wakati hatima ya CUF kushiriki au kutoshiriki uchaguzi wa marudio inatarajia kufahamika leo, mgawanyiko mkubwa umeibuka miongoni mwa wajumbe wake wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa.

Katika mgawanyiko huo, wamo wanaopinga kushiriki huku wengine wakitaka chama kuangalia upya msimamo wa kususia uchaguzi huo.

==>Akizungumzia mgawanyiko huo, Mkurugenzi wa Mawasiliano  wa  CUF, Ismail Jussa Ladhu, alisema kutokana na ukubwa na uzito wa mgogoro wa uchaguzi, mgawanyiko ni jambo ambalo halikwepeki kwa chama kikubwa kama hicho.

Alisema uongozi wa chama uko makini katika kujadili ajenda ya mgogoro wa uchaguzi na kuwataka viongozi na wanachama pamoja na wananchi kwa ujumla kuwa na moyo wa subira wakati Baraza Kuu la Uongozi la Chama linajiandaa kutoa kauli ya mwisho juu ya hatima ya uchaguzi huo.

Jussa alisema uamuzi utakaotolewa na Baraza Kuu ndio utakuwa mwongozo kwa wagombea wote wa chama pamoja na wanachama na watu wanaokiunga mkono chama.

Alisema mchezo aliyoufanya Jecha wa kufuta matokeo ya uchaguzi kwa manufaa ya CCM, haukubaliki katika misingi ya demokrasia na utawala bora.

#YALIYOJIRI>>>>Waziri Mkuu Asisitiza Bungeni Leo Kuwa TBC Hawatarusha Live Matangazo ya Bunge.Fahamu zaidi hapa.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kwamba matangazo ya bunge hayatarushwa yote live kama serikali ilivyosema jana na tayari hatua hiyo imekwisha kuanza.

Majaliwa ameyasema hayo alipokuwa akijibu swali la papo kwa papo la Mbunge wa Hai ambaye pia ni msemaji wa kambi ya upinzani Bungeni Freeman Mbowe aliyetaka kujua kwanini serikali imefanya maamuzi ya kuzuia wananchi wasione matangazo ya Bunge moja kwa moja.

Akijibu swali hilo Waziri Mkuu amesema kwamba uamuzi wa kutoonyeshwa kwa matangazo ya moja kwa moja uliombwa na chombo cha umma chenyewe kwamba hakina uwezo kujiendesha na uamuzi wao huo umeungwa mkono na serikali.

''Maamuzi ya chombo hiki yameungwa mkono na serikali na waziri Nape Nnauye amefanya kipindi maalum kuhusiana na jambo hilo na wananchi wameelewa vizuri na wameiunga mkono serikali kwamba matangazo yatarekodiwa na yatarushwa kama kipindi maalum usiku'' Amesema Waziri Majaliwa.

#YALIYOJIRI>>>Wabunge wa Upinzani Watoka Bungeni tena.......Ni Baada ya Naibu Spika Tulia Ackson Kuwanyima Muongozo ili Waongee.Fahamu zaidi hapa.

Hali ya sintofahamu imeendelea ndani ya bunge baada ya wabunge wote wa Upinzani kutoka ndani ya bunge.

Hali hiyo imetokea baada ya Naibu Spika Tulia Mwansasu kumtaka katibu wa Bunge kuarifu bunge ratiba inayoendelea, ambapo katibu wa Bunge alibainisha kwamba kazi ya ratiba ya leo inaonyesha kwamba ni kuchangia hotuba ya Rais aliyoitoa wakati wa ufunguzi wa Bunge.

Baada ya hapo wabunge wa upinzani waliomba miongozo kutoka kwa Naibu Spika, ambapo Naibu spika alimruhusu Mbunge wa Tarime Mjini Ester Matiko.

Mbunge huyo aliuliza swali kuhusu mapungufu yaliyojitokeza kwa elimu bure kwa wanafunzi kutozwa michango katika jimbo lake.

Naibu wa spika akitoa majibu ya muongozo huo alisema kwamba serikali inatambua matatizo yanayojitokeza na inayafanyia kazi

Jambo hilo liliwakasirisha wabunge wa upinzani na kuzidi kuomba miongozo ambapo Naibu Spika aliwakataza na kuruhusu ratiba iliyo mbele ya bunge kuendelea,hali ambayo iliwafanya wabunge wa upinzani wasuse na  kutoka nje.

==>Wabunge wa CCM wanaendelea  kujadili Hotuba ya Rais.

#YALIYOJIRI>>>>Waziri Mkuu Atoa Ufafanuzi Kuhusu Kauli Yake Ya Kupiga Marufuku Mikutano Ya Vyama Vya Siasa.Fahamu zaidi hapa.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo amefafanua kauli yake ya kupiga marufuku mikutano ya vyama vya siasa nchini  kuwashukuru wananchi hasa kwa wale wagombea walioshindwa uchaguzi  kwa kusema  kuwa mwandishi aliyeripoti tukio hilo alimnukuu vibaya.

“.......na tumesema, siasa tumeshazimaliza. Sasa tunataka tufanye kazi za maendeleo. Hatuhitaji tena watu kuja kutuvuruga. Mikutano ya shukrani itafanywa na wale tu walioshinda kwenye maeneo yao. Wengine watulie.

“Vyama sasa viache wale tu waliochaguliwa kwenye maeneo yao washukuru, wengine hawa watakuja kuleta maneno ambayo yatatuvuruga. "
Waziri Mkuu alinukuliwa akiyasema hayo Wilayani Ruangwa mkoani Lindi

Akijibu Swali la Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani bungeni Mhe. Freeman Mbowe  leo asubuhi kuhusiana na kauli hiyo, Waziri Mkuu alisema kuwa serikali inaendeshwa kwa mujibu wa sheria na katiba hivyo inatambua kuwa katika mfumo wa vyama vingi,  vyama vya siasa vinaruhusiwa kufanya mikutano ila kwa utaratibu maalumu.

Waziri Majaliwa alisema  mwandishi aliyemnukuu kuhusiana na kauli hiyo hakumtendea haki kwa kuwa aliitoa kauli hiyo  akiwa kama mbunge wa kawaida na si Waziri mkuu na yalikuwa ni makubaliano ya vyama vya siasa katika jimbo lake  na kwamba halikuwa agizo kwa nchi nzima.

Waziri Mkuu huyo aliongeza kuwa kauli hiyo aliitoa wakati alipokutana na madiwani na viongozi wengine wa mkoa wake ambapo walikubaliana kuweka siasa pembeni na kufanya kazi kwa pamoja katika kuleta maendeleo.

#YALIYOJIRI>>>Tusimruhusu Rais Magufuli Kusimika Utawala Wa Kidikteta Nchini- ACT Wazalendo.Fahamu zaidi hapa.

JANA limetokea tukio la aibu katika nchi yetu pale serikali ilipofanya jaribio la hatari la kuzuia wananchi kuona na kusikia kinachoendelea bungeni.

Kitendo cha serikali ya CCM kuzuia kuonyeshwa moja kwa moja vipindi vya bunge katika televisheni ya taifa ni cha kijima na sisi chama cha ACT-Wazalendo tunakilaani kwa nguvu zetu zote.
 
Tunakitafsiri kitendo hiki cha serikali kama mwendelezo wa hatua na juhudi za Rais Magufuli za kuminya demokrasia na kusimika utawala wa kiimla.

Tunawasihi wananchi kusimama imara na kuzipinga jitihada zozote ovu za kuminya demokrasia nchini.
 
Tunawapongeza wabunge wazalendo wa upinzani kwa kusimama pamoja na kupinga nia ovu ya serikali ya kuua demokrasia katika nchi yetu.

Tunawatia shime wabunge wote wazalendo kuendelea kupigania maslahi mapana ya taifa letu.

ACT-Wazalendo! Taifa kwanza leo na kesho!

Imetolewa na;
Samson Mwigamba,
KATIBU MKUU.