WAKATI Bunge likimtema rasmi aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki (CCM), Lazaro Nyalandu, mwenyewe amejitokeza na kuponda habari zinazosambazwa kueleza ubaya akisema ni uzushi.
Jana Nyalandu alisema taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, ikiwamo WhatsApp na Facebook kuelezea kasoro za kiutendaji akiwa Waziri wa Maliasili na Utalii ni uzushi ambao Watanzania wanapaswa kuupuuza.
Nyalandu alitangaza kujivua gamba CCM, kuandika barua ya kuachia kiti cha ubunge na kueleza nia yake ya kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Jumatatu iliyopita.
Chadema, kupitia Katibu Mkuu wake, Dk. Vicent Mashinji, kilitangaza kumpokea awe mwanachama na kwamba alichelewa kutoa uamuzi huo.
Lakini jana taarifa ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, ilieleza kuwa hajapokea barua ya Nyalandu kujiuzulu nafasi yake.
Aidha, Ndugai alisema alichopokea ni barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa CCM ya Oktoba 30, kimsingi, ikimtaarifu kuwa Nyalandu amepoteza sifa ya kuwa mwanachama wa chama hicho na ubunge kwa mujibu wa ibara ya 13 ya katiba yao.
Katika ujumbe alioandika katika akaunti yake ya mtandao wa Tweeter jana, Nyalandu alisema ni uzushi, uongo wa kupuuzwa na aibu kubwa.
"Fake news alert! (Tahadhari habari za uzushi!) Habari hii ni ya kutungwa na kufikirika. Kibaya zaidi ni ya uongo. Siasa za aina hii ni za kizamani. Aibu tupu!" Aliandika Nyalandu katika akaunti yake hiyo.
Katika ukurasa huo, Nyalandu ambaye amekuwa Mbunge wa CCM tangu mwaka 2000, aliambatanisha na majadiliano ya watu wanne kwenye kundi la WhatsApp liitwalo 'Chadema Taifa' yakionyesha washirikia wake ni Mchungaji Peter Msigwa, Nyalandu na muundaji wa kundi.
Katika kundi hilo, ilidaiwa Nyalandu ameandika kuwa yuko katika wakati mgumu kwa kuwa serikali inataka kumshtaki kwa kuhusika kuuza vitalu na wanyama, na kwamba anaomba ushauri.
Katika majadiliano hayo, muundaji wa kundi, anayedaiwa kuwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, anaonekana kumpa pole Nyalandu na kumshauri kuhama chama hicho.
Mbali na chapisho hilo la Nyalandu, maandiko mbalimbali yamesambaa kwenye mitandao ya kijamii tangu tamko la Nyalandu la Jumatatu, yakieleza jinsi alivyogawa vitalu vya uwindaji na wanyamapori.
Mwaka 2012, aliyekuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi ya CCM, Nape Nnauye, alitangaza operesheni ya kuvua magamba, akiwataka wanachama wa CCM wote ambao hawatakiwi, kukihama chama hicho haraka kabla ya kuvuliwa magamba.
Kutokana na operesheni hiyo ya CCM, Chadema kiliibuka na operesheni 'Vua Gamba Vaa Gwanda', ikiwa na lengo la kuvuna wanachama wengi waliokataliwa CCM na kuwataka kuvaa sare za chama hicho na kuungana nao.
Katika taarifa yake ya kujitoa CCM Nyalandu aliyochapisha katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram, Nyalandu aliomba kutua Chadema ili aungane nao kuleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi nchini.
"Nitaomba kama itawapendeza wanachama wa Chadema, basi waniruhusu kuingia malangoni mwao, niwe mwanachama, ili kuungana na Chadema na Watanzania wote wanaopenda kuleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi nchini kwa kupitia mfumo wa kidemokrasia na uhuru wa mawazo."
Nyalandu (45) alisema amejiuzulu ubunge kuruhusu kufanyika kwa uchaguzi mwingine ili wananchi wapate fursa ya kuchagua itikadi wanayoona inawafaa kwa majira na changamoto lukuki.
Mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Singida na Mjumbe wa Kamati za Siasa Wilaya na Mkoa, alisema: "Ni imani yangu, kamwe hayatakuwa ya bure maneno haya, wala uamuzi huu niufanyao mbele ya Watanzania leo ili kwamba, sote kama taifa tuingie kwenye mjadala wa kuijenga upya misingi ya nchi yetu."
Aliandika zaidi: "Ni maombi yangu kwa Mungu kuwa haki itamalaki Tanzania, upendo, amani na mshikamano wa watu wa imani zote za dini, mitazamo yote ya kiitikadi za kisiasa na makabila yote nchini uimarike. Tushindane kisera na kuruhusu tofauti za mawazo, lakini tubaki kama ndugu na taifa lililo imara na nchi yenye adili."
Nyalandu alitangaza nia kuwania urais Desemba 28, 2014 katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Ilongero jimboni kwake, wakati akihutubia mamia ya wananchi.
Katika mkutano huo, Nyalandu alisisitiza "sasa ni zamu ya vijana kuongoza nchi" huku akiwaambia wananchi kuwa safari yake ya ubunge kwa miaka 15 inaanzisha safari nyingine bila kuwaeleza ikiwa bado ana nia na ubunge au la. Siku hiyo, aliambatana na mkewe, watoto na wazazi wake.
Ingawa alikuwa mmoja kati ya wanaCCM 38 waliojitokeza kuwania urais mwaka 2015, jina lake lilikatwa pamoja na kina Lowassa na Sumaye na kuteuliwa Rais Magufuli kupeperusha bendera ya chama hicho.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment