Friday, 27 November 2015

#YALIYOJIRI>>>Kamishina mkuu wa TRA Rished Bashe asimamishwa kazi na Magufuli.Fahamu zaidi hapa.



Rais Dk Magufuli amemsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa mamlaka ya mapato Tanzania ( TRA) Rished Bade na kumteua Philiph Mpango kukaimu nafasi hiyo

#YALIYOJIRI>>>Serikali Yakanusha Hazina Kuachwa Tupu na Rais Kikwete.Fahamu zaidi hapa.

Serikali imekanusha taarifa zinazosambazwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa Rais mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kuwa amekomba fedha hazina na kuiacha Serikali bila fungu lolote.

Hayo yamesemwa jijini dare es salaam na Kamishina wa Bajeti kutoka Wizara ya Fedha Bwa. John Cheyo huku akiwataka wananchi kupuuza habari hiyo kwani hazina ukweli wowote.

“Hazina inazo pesa za kutosha  na tunajivunia kufanya uchaguzi wa mwaka huu,  kununua mashine za BVR  kwa kutumia pesa za watanzania bila kutegemea msaada wowote kutoka nje ya nchi  na kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu mwaka huu” alisema Bwa. Cheyo.

Pia aliongeza kuwa serikali imeendelea kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa bomba la gesi ambalo limekamilika hivi karibuni, vinu vya kuchakata gesi na ujenzi wa barabara nchini.

Aliendelea kusema kwamba mfumo wa serikali wa bajeti unaiwezesha serikali kupanga vipaumbele vya matumizi kulingana na bajeti ilivyopangwa ambapo fedha zinazokusanywa kupitia mfuko mkuu wa serikali ndizo hutumika.

Bajeti iliyoidhinishwa na Bunge kwa kipindi cha 2015-2016 ni shilingi Trilioni 22.5 na bajeti hiyo inatengenezewa mpango wa makusanyo na matumizi kwa kulipia mishahara ya wafanyakazi na miradi mbalimbali iliyoidhinishwa.

Pia katika matumizi mengine bajeti hiyo inalipia chakula cha wanafunzi, mikopo ya wanafunzi elimu ya juu, ununuzi wa dawa na vifaa tiba na chakula cha hifadhi ya taifa

#YALIYOJIRI>>>Kassim Majaliwa Waziri Mkuu Afanya Ziara ya Kushtukiza Bandarini,Awafuta Kazi na Kuamuru Kukamatwa Kwa Maofisa Kibao wa TRA.Fahamu zaidi hapa.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amefanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es Salaam mapema leo na kubaini upotevu wa makontena 349.

 Waziri Mkuu amebaini upotevu wa makontena hayo ambayo yana thamani ya zaidi ya shilling bilioni 80, na kuagiza kufutwa kazi mara moja kwa maafisa waliohusika na upotevu huo.

Majaliwa amewasimamisha kazi Kamishna wa Kodi, Tiagi Masamaki pamona na Habibu Mpozya wa kitengo cha huduma kwa wateja.

Uamuzi huo wa Waziri Mkuu umekuja baada ya kubaini kuwa katika kumbukumbu za Mamlaka ya Bandari kuna taarifa ya makontena 349 yenye thamani ya shilingi bilioni 80 lakini taarifa hizo hazipo kwenye kumbukumbu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Waziri Mkuu ameelekeza Polisi kuwakamata maafisa wote waliohusika na sakata hilo kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.

#YALIYOJIRI>>>CUF Yakanusha Taarifa za Kukubaliana na CCM Kurudia Uchaguzi wa Zanzibar.Fahamu zaidi hapa.

Tumepokea taarifa kwamba Balozi Seif Ali Iddi amehojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Radio France International (RFI) na kusema kwamba eti viongozi wa CCM na CUF WAMEKUBALIANA UCHAGUZI ZANZIBAR URUDIWE, na kinachojadiliwa hivi sasa ni NANI ASIMAMIE UCHAGUZI WA MAREJEO kwa sababu ZEC ya JECHA INAONEKANA KUTOAMINIKA.

Tunapenda kuwawekea wazi Wazanzibari wote kwamba taarifa hizo hazina ukweli wowote, ni za uzushi na wazipuuze.

Msimamo wa CUF na Maalim Seif Sharif Hamad uko pale pale kwamba HAKUNA KURUDIWA UCHAGUZI na kwamba MSHINDI HALALI WA UCHAGUZI WA TAREHE 25 OKTOBA, 2015 ATANGAZWE NA KUAPISHWA.

Kauli za Balozi Seif Ali Iddi ni za kutapatapa zianzolenga kuwatuliza wana-CCM ambao wanaonekana kukata tamaa baada ya kushindwa vibaya na CUF kwenye uchaguzi mkuu wa Rais wa Zanzibar, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Wabunge na Madiwani uliofanyika tarehe 25 Oktoba, 2015.

Kwenye uchaguzi mkuu wa Urais wa Zanzibar, mgombea wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alimbwaga vibaya mgombea wa CCM, Dk. Ali Mohamed Shein, kwa zaidi ya kura 25,000.

Balozi Seif Ali Iddi mwenyewe akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni ya CCM anatuhumiwa na wana-CCM kushindwa kazi na kukisababishia chama chao kushindwa vibaya kuliko wakati wowote katika historia ya chaguzi za Zanzibar.

Lakini kama hilo halitoshi, wana-CCM wanamtuhumu Balozi Seif na wajumbe wengine wa Kamati ya Kampeni aliyokuwa akiiongoza kusimamia matumizi mabaya ya kiasi kikubwa cha fedha za kampeni za Chama hicho ambazo sehemu kubwa walimdanganya mgombea wao, Dk. Ali Mohamed Shein, kwamba zimetumika kuleta ushindi wa CCM kisiwani Pemba lakini kumbe ziliishia katika mifuko ya watu binafsi.

Haistaajabishi kwamba sasa Balozi Seif Ali Iddi ameamua kuja na njia ya kutoa taarifa za udanganyifu ili kujinusuru na mzigo wa tuhuma za kushindwa kazi na kusimamia matumizi mabaya ya fedha za kampeni kutoka kwa CCM wenzake.

CUF tunamtaka Balozi Seif Ali Iddi awache kudanganya umma na badala yake awajibu CCM wenzake kwa nini amekitia chama hicho aibu na fedheha kubwa ya kupata kipigo kibaya katika uchaguzi kilichopelekea CCM kupoteza majimbo tisa (9) kisiwani Unguja na Dk. Ali Mohamed Shein kushindwa uchaguzi wa Urais wa Zanzibar kwa zaidi ya kura 25,000 huku wakidai kutumia mamilioni ya fedha ambazo hawana maelezo zimetumika vipi.

CUF tunawataka Wazanzibari kutobabaishwa na kauli za kushindwa kazi za Balozi Seif Ali Iddi na watulie wakijua kuwa ufumbuzi wa haki wa uchaguzi mkuu utapatikana kwa kutangaza matokeo ya kura kwa majimbo yaliyobakia na hatimaye mshindi kutangazwa na kuapishwa.

HAKI SAWA KWA WOTE
ISMAIL JUSSA
MKURUGENZI WA MAWASILIANO - CUF
26 NOVEMBA, 2015

#YALIYOJIRI>>>Marekani yatoa tamko kwa Tanzania Yaitaka Serikali itoe Maelezo Uchaguzi Zanzibar na Sheria ya Mtandao , Yatishia kusitisha Msaada wa Trilioni.Fahamu zaidi hapa.

Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC) wa Marekani umeonya kuwa hali ya kisiasa Zanzibar na tukio la hivi karibuni la watu kukamatwa chini ya sheria mpya ya uhalifu mtandaoni yanaweza kuathiri vigezo vya kuiwezesha Tanzania kupata msaada.

Katika barua ya MCC ya Novemba 19, ambayo imesainiwa na Naibu Makamu wa Rais wa Idara ya Operesheni ya Miradi kwa Afrika, Jonathan O. Bloom kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile, mfuko huo umetaka maelezo kuhusu utatuzi wa mgogoro wa Zanzibar pamoja na ufafanuzi wa sheria ya uhalifu wa mtandaoni.

“MCC inashukuru kwa uongozi na dhamira yako wakati wa mchakato mzima wa maendeleo ya mradi huu. Msaada wa dola milioni 472 (ambazo ni zaidi ya Sh trilioni moja), una nafasi kubwa ya kusaidia kuleta mageuzi katika sekta ya nishati na kuwaunganisha maelfu ya watu katika gridi.

“Lakini mgogoro wa Zanzibar na ukamataji watu wa hivi karibuni kupitia sheria mpya ya uhalifu mtandaoni umetutia wasiwasi.

“Kama ujuavyo, mataifa washirika wa MCC wanapaswa kuendeleza na kuonyesha dhamira ya utawala bora, ambayo ni pamoja na kufuata misingi ya demokrasia na kulinda uhuru wa kutoa mawazo. 
 
"Hata hivyo, matukio ya karibuni yanaifanya MCC na wadau wetu kujawa na maswali kuhusu dhamira hiyo,” inasomeka barua hiyo ya MCC iliyosainiwa na Bloom.

Kwa mujibu wa barua hiyo, MCC inafuatilia kwa karibu nyendo za Serikali katika ushughulikiaji wa masuala hayo ya utawala bora, hasa kipindi hiki kuelekea mkutano wa mwezi ujao wa bodi ya mfuko huo.

“Utatuzi wa mgogoro wa Zanzibar kwa namna ya kuridhisha pande zote husika na haja ya kuiona Serikali ikifafanua hadharani nia yake na sheria ya uhalifu wa mtandaoni, kama vile kuchapisha utekelezaji wa kanuni zinazoakisi mchango wa mdau na kuonyesha dhamira ya kuendelea kulinda uhuru wa kutoa maoni, kutaisaidia MCC kuitathimini Tanzania kwa namna chanya juu ya kuendelea kwa dhamira yake ya kutimiza sharti la kufuzu kupata misaada,” ilisema barua hiyo.

Barua hiyo ilimalizia kwa kusema: “Wasiwasi huu ni kikwazo cha mipango yetu ya ushirika. Tunaamini utashughulikia wasiwasi huu ipasavyo na tunatarajia kupata jibu kutoka kwako.”

Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Likwelile, hakupatikana na hata alipotafutwa kwa njia ya simu hakupokea.

Pamoja na juhudi hizo, pia alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu hakujibu, ambapo alipotafutwa Msemaji wa Wizara ya Fedha, Ingiahedi Mduma, kuhusu barua hiyo ya MCC, alisema hana taarifa na hajaiona.

“Sina taarifa na wala sijaiona barua hiyo, hivyo siwezi kusema chochote labda mpaka nitakapoongea na bosi aniambie kama amepokea barua hiyo,” alisema Mduma.

Mwanzoni mwa Oktoba mwaka huu, Rais mstaafu Jakaya Kikwete akiwa nchini Marekani kuhudhuria shughuli za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN), alikutana na Mtendaji Mkuu wa MCC, Dana J. Hyde na watumishi waandamizi, akiwamo Makamu wa Rais wa Operesheni za mfuko huo, Kamran Khan.

Katika mkutano huo, MCC ilitangaza kuwa Tanzania imetimiza masharti yote ya kupatiwa awamu ya pili ya fedha za maendeleo kutoka katika mfuko huo, kuanzia mwakani, zaidi ya dola za Marekani milioni 472.8, sawa na zaidi ya Sh trilioni moja za Tanzania.

Katika mkutano huo, Rais mstaafu Kikwete, aliambatana na ujumbe wa maofisa kadhaa akiwamo Waziri wa Fedha wa Zanzibar, Yusuf Omar Mzee.

Katika awamu ya kwanza ya fedha za MCC, Tanzania ilipata dola za Marekani milioni 698 (sawa na Sh trilioni 1.46).

Kama MCC wataridhika na maelezo ya Serikali kupitia Wizara ya Fedha, Tanzania itakuwa imepata jumla ya Sh trilioni 2.45 kwa awamu zote mbili kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika kipindi cha miaka 10.

Awamu ya kwanza ya fedha hizo zilitumika kujenga Barabara za Tunduma- Sumbawanga, Tanga-Horohoro na Namtumbo- Songea- Mbinga.

#YALIYOJIRI>>>Manyaunyau Ahukumiwa Jela Miaka 3 Kwa Kushindwa Kufufua Maiti.Fahamu zaidi hapa.

Dk. Manyaunyau jina lake Dunia Salumu Mkazi  wa Dar es Salaam, amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela pamoja na kulipa fidia ya Sh milioni 10 baada ya kupatikana na hatia ya kujipatia fedha Sh milioni 29.6 kwa njia ya udanganyifu.

Manyaunyau anadaiwa kujipatia kiasi hicho cha fedha kutoka kwa mlalamikaji, Tekra Modesta kama malipo ya kazi ya kumfufua marehemu kaka yake aliyefahamika kwa jina moja la Modest ambaye alifariki dunia miaka kadhaa iliyopita.

Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, Flora Haule, alisema mtuhumiwa huyo ametiwa hatiani baada ya ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka kujitosheleza.

“Mahakama inatoa hukumu kwa mtuhumiwa kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela na kulipa fidia ya Sh milioni 10 baada ya kumaliza kutumikia kifungo chake ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo,” alisema Hakimu Flora.

Upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi wanne ambao wote waliithibitishia mahakama juu ya mtuhumiwa kujipatia kiasi hicho cha fedha kwa njia za udanganyifu.

Awali Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Estar Kyala, aliiambia mahakama kuwa hakuna kumbukumbu za makosa ya nyuma dhidi ya mshtakiwa na hivyo kuiomba kutoa adhabu kali ili kuwa fundisho kwa wote wenye tabia kama hizo.

Katika maelezo ya awali, ilidaiwa kuwa mtuhumiwa alijipatia kiasi hicho cha fedha kutoka kwa mlalamikaji kama malipo ya tukio la kutaka kumfufua kaka wa mlalamikaji.

Ilielezwa kuwa mtuhumiwa alipokea fedha hizo kwa awamu mbili tofauti ambapo awali Mei 2007 jijini Dar es Salaam alipewa kiasi cha fedha ambacho hakikufahamika.

Mei Mosi, mwaka 2008 mtuhumiwa alipokea kiasi kingine cha fedha kama malipo kwa ajili ya kumalizia kazi yake ya kumfufua marehemu ambaye ni ndugu wa mlalamikaji jambo ambalo alishindwa kulitekeleza.

Manyaunyau amejizolea umaarufu mkubwa katika maeneo mengi nchini kwa kile kinachodaiwa kuwa anao uwezo wa kutibu na kuwafichua wachawi popote walipo sambamba na staili yake ya kunyonya damu ya paka akiwa katika shughuli zake za uganga.

Katika tukio lililovuta wakazi wengi wa Dar es Salaam, Manyaunyau anadaiwa kumwibua nyoka ambaye alikuwa tishio na kuzusha hofu kubwa kwa wakazi wa maeneo ya Manzese Midizini ambapo ilidaiwa kuwa alikuwa akiwagonga watu katika mazingira ya kutatanisha katika njia inayopita kwenye makaburi.

Inaaminika kuwa baada ya kuitwa, Dk. Manyaunyau aliweza kumuibua nyoka huyo na kuonekana hadharani tukio lililohisiwa kuwa ni la kimazingara zaidi.

Wednesday, 25 November 2015

#YALIYOJIRI>>>Rais Uhuru Kenyatta amefanya mabadiliko katika Baraza lake la Mawaziri.Fahamu zaidi hapa.

Rais wa Kenya amefanya mabadiliko katika Baraza lake la Mawaziri na kuwaacha wote ambao wizara zao zilikumbwa na tuhuma za ufisadi.

Rais Uhuru Kenyatta amechukua hatua hiyo siku moja tu baada ya kutangaza ufisadi kuwa tishio kwa usalama wa kitaifa. Rais ameahidi kufanya mabadiliko zaidi katika afisi yake hivi karibuni.

Katika hotuba ilioonyeshwa kwa njia ya Televisheni, Rais Kenyatta ameongeza idadi ya wizara kutoka 16 hadi 20 na kuongeza idara mpya chini ya wizara mbalimbali katika kile alichosema ni kusaidia mawaziri kutekeleza majukumu yao bora zaidi.

Idara hizo zimeongezwa kutoka 26 hadi 41.
Rais Kenyatta amefanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri baada ya mawaziri sita kulazimika kujiondoa kutokana na wizara walizosimamia kuhusishwa na ufisadi huku wawili kati yao wakikabiliwa na kesi mahakamani.

Ni mabadiliko yaliyotarajiwa hasa baada ya hatua ya aliyekuwa waziri wa Ugatuzi Anne Waiguru kujihuzulu mwishoni mwa juma kutokana na kile alichosema ni ushauri wa daktari wake- baada ya usumbufu aliopata wizara yake ilipohusishwa na sakata kadhaa za ufisadi.

Kwa mujibu wa katiba idadi ya mawaziri inapaswa kuwa kati ya 14 na 22 na hivyo kujiuzulu kwa Bi Waiguru kulisababisha idadi hiyo kupungua hadi 13.

Baraza jipya la mawaziri linajumuisha wanawake wanne na wanaume 16.
Baadhi ya mawaziri wamesalia katika nafasi zao huku wengine wapya wakiteuliwa kuchukua nafasi za mawaziri waliohusishwa na ufisadi.

Hatua itakayofuata sasa ni kwa mawaziri wapya kuchunguzwa na kamati ya bunge kabla ya kuidhinishwa kikamilifu.

Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta imekuwa ikikabiliwa na changamo ya ufisadi katika wizara kadhaa na kumekuwepo shinikizo sio tu kutoka kwa wananchi lakini pia kutoka kwa mashirika ya kijamii,viongozi wa upinzani na hata mabalozi wa nchi za kigeni kutaka hatua zichukuliwe.

#YALIYOJIRI>>>Aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo la Kahama Mjini (CHADEMA ), James Lembeli amefungua kesi Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga kupinga matokeo Ubunge Jimbo la kahama Mjini, Mgombea wa CCM Jumanne Kishimba alitangazwa mshindi.Fahamu zaidi hapa.

Aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo la Kahama Mjini (CHADEMA ), James Lembeli amefungua kesi Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga kupinga matokeo yaliyompa ushindi mgombea wa CCM, Jumanne Kishimba.

Lembeli anawakilishwa na Joachim Hamis wa kampuni ya Mpoki & associates Advocates ya Dar es salaam, hii kesi si ya kukosa, itakuwa ni ya kusisimua sana.

Tuesday, 24 November 2015

#YALIYOJIRI>>>Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Ataka Apewe Sababu Kwa Nini Mabasi yaendayo kasi Hayajaanza kazi Hadi Leo.Fahamu zaidi hapa.

WAZIRI MKUU Majaliwa Kassim Majaliwa amewataka wakurugenzi wa vitengo na wakuu wa taasisi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) wapate nakala ya hansard ya hotuba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kuzindua Bunge la 11, waisome na kufanyia kazi maeneo yote aliyoyaainisha.

“Katibu Mkuu hakikisha umepata hansard ya hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati akizindua Bunge na uhakikishe kila mkurugenzi ana nakala na kila mmoja wenu lazima ahakikishe anafanyia maeneo ambayo Mheshimiwa Rais ameyaainisha. Ni lazima tuelewane ni nini tunapaswa tufanye,” alisema.

Ametoa kauli hiyo jana (JANA) mchana (Jumanne, Novemba 24, 2015) wakati akizungumza na wakuu wa taasisi, wakurugenzi na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) kwenye mkutano uliofanyika ofisi ndogo ya TAMISEMI, barabara ya Kivukoni, jijini Dar es Salaam.

“Ninatamani kuona mabadiliko ya utendaji kazi Serikalini katika kipindi kifupi. Natamani kila mmoja asiridhike na uzembe unaofanywa huku chini. Ni nyote ni wataalamu, kwa hiyo mnapaswa kudhirisha elimu yenu na ujuzi mlionao,” aliwasisitizia Wakurugenzi hao.

Alisema kila mkurugenzi na mkuu wa taasisi anapaswa kuongeza usimamizi na ufuatiliaji wa kazi kwenye sekta yake kwani hilo litasaidia kukidhi matarajio ya Watanzania ya kuona mabadiliko ya utendaji kazi kwenye Serikali ya Awamu ya Tano. 
 
“Ninyi wakurugenzi siyo desk officers bali ni field officers. Nataka muweke utaratibu wa kwenda vijijini mkasimamie watu wenu, pia mhimize uadilifu, uaminifu na weledi wa kazi,” alisisitiza.

“Mambo ninayotaka mhimize watendaji waliopo chini yenu ni pamoja na haya yafuatayo: muda wa kuripoti kazini uzingatiwe, muda wa kukaa kazini uzingatiwe, utokaji kazini kwenda kwenye chai na chakula cha mchana udhibitiwe, na mipango na malengo ya kazi kwa siku ni lazima yafikiwe,” alisema.

“Tunataka kujua mtumishi amefanya nini tangu alipoingia ofisini. Suala siyo kukaa tu ofisini, kwani kuna mtu anakaa ofisini, hajaenda hata kunywa chai lakini ukiuliza amefanya nini hupati jibu la kueleweka. Sisi kama vongozi wao ni lazima tujue wanafanya kazi gani wanapokuwa maofisini,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa ameitisha kikao ofisini kwake kesho (LEO )saa 4 asubuhi akitaka kupatiwa taarifa ni kwa nini mradi wa mabasi yaendayo kasi (DART) haujaanza kazi hadi sasa.
 
 “Kesho( LEO)  saa 4 asubuhi Katibu Mkuu, Mkurugenzi Mkuu DART na watendaji wako mje ofisini. Nataka kupata maelezo ni kwa nini mabasi hayajaanza kazi hadi leo, je ni lini yataanza kazi, je ni nani anakwamisha. Na hata kama ni sheria, ni kwa nini tusiziharmonise ili kuondoa hivyo vikwazo,?” alihoji Waziri Mkuu.

“Ninataka kupata haya maelezo kwa sababu Watanzania na hasa wana-Dar es salaam, wamesubiri kwa muda kuona mradi ukianza kazi ili uondoe kero ya usafiri. Wao wanajua anayehusika ni TAMISEMI,” aliongeza.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na watumishi na viongozi wa TAMISEMI, Katibu Mkuu wa OWM-TAMISEMI, Bw. Jumanne Sagini alimweleza baadhi ya mafanikio na changamoto ambazo wizara hiyo imekabiliana nazo katika utendaji wake wa kazi.

Kuhusu ujenzi wa vyumba vya maabara kwa ajili ya kuimarisha ufundishaji wa masomo ya sayansi, Bw. Sagini alisema vyumba hivyo vimeongezeka kutoka 247 mwaka 2005/2006 na kufikia 6,161 mwaka 2014/2015. Pia alisema vyumba 4,228 viko kwenye hatua za kukamilika ujenzi wake.

Kuhusu utengaji wa madirisha ya kuhudumia makundi yenye msamaha kama wazee na watu wenye ulemavu hospitalini na kwenye vituo vya afya, Katibu Mkuu alisema nayo yameongezeka kutoka madirisha 5,074 mwaka 2010 na kufikia 7,903 mwaka 2014/2015 sawa na ongezeko la asilimia 55.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM

#YALIYOJIRI>>> Familia ya Alphonce Mawazo na CHADEMA Washinda Kesi ya Pingamizi la Polisi, Sasa kesi ya Msingi kusikilizwa.Fahamu zaidi hapa.

Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Lameck Mlacha, ametupilia mbali mapingamizi yaliyowekwa na RPC wa Mwanza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya kesi iliyofunguliwa jana na familia ya Marehemu Alphonce mawazo kuomba tafsri ya mahakama baada ya jeshi la polisi mkoani Mwanza kupiga marufuku mikusanyiko ya kuuaga mwili wa marehemu. 
 
Katika mapingamizi hayo, mwanasheria mkuu wa serikali  alidai kuwa mleta maombi ambae ni Baba mdogo wa Mawazo hana uhalali wa kisheria wa kuleta maombi hayo mahakamani  kwa kuwa yeye si baba mzazi wa marehemu, na kuwa hajaleta hoja za kubishaniwa kwenye maombi hayo.
 
Upande wa utetezi unaoongozwa na mawakili John Mallya, James Millya na Paul Kipeja ulijibu hoja hizo kuwa katika hatua hiyo masuala ya kubishaniwa hayana sababu ya kuletwa kwa kuwa ni hatua ya awali sana.

Kuhusu uhalali wa kisheria wa baba mdogo wa marehemu, majibu yalikuwa kwamba baba mdogo kwa kuwa ndiye aliemlea Marehemu Mawazo, anayo mamlaka na uhalali wa kisheria wa kuleta maombi hayo.

Mahakama imekubaliana na hoja za mawakili wa mleta maombi na kuamua kuruhusu kesi ya msingi kufunguliwa kama ilivyoombwa, na kutupilia mbali mapingamizi ya RPC na mwanasheria mkuu.

Upande wa wapeleka maombi utawasilisha maombi ya kesi ya msingi leo hii mchana, kisha utasubiri maelekezo ya Mahakama kuwa kesi hiyo itaanza kusikilizwa lini kisha uamuzi wa kesi hiyo.
Alphonce Mawazo  alikuwa ni mwenyekiti wa chadema mkoani Geita kabla ya kuuawa kikatili kwa kukatwa mapanga na mashoka na watu wasiojulikana Novemba 14 mwaka huu katika kijiji cha katoro wilayani Geita.

Friday, 13 November 2015

#MICHEZO>>>James Milner mchezaji wa Liverpool amesema kuwa anatamani sana mchezo wao dhidi ya Man City.Fahamu zaidi hapa.

Kusoma zaidi kutoka James Milner juu ya matarajio yake ya kupona kutokana na majeraha yanayo mkabili ilicha ya hayo yote yeye macho yake yote kweye mchezo wao na  Man City tarehe November 21,2015.

Milner 'Ni lazima kuwa muda mrefu sana na pengine mimi itakuwa nyuma kwa mchezo ujao.

Wednesday, 11 November 2015

#YALIYOJIRI>>>Traffic askari wa usalama barabarani aliyerekodiwa akichukua rushwa toka kwa dereva eneo la Kabuku Tanga, afukuzwa kazi.Fahamu zaidi hapa.

Taarifa hizi zinadai Askari huyo wa usalama barabarani ametiwa kibindoni na wakuu wake wa kitengo akisubiri hatua zaidi kuchukuliwa dhidi yake.