Mfuko
wa Changamoto za Milenia (MCC) wa Marekani umeonya kuwa hali ya kisiasa
Zanzibar na tukio la hivi karibuni la watu kukamatwa chini ya sheria
mpya ya uhalifu mtandaoni yanaweza kuathiri vigezo vya kuiwezesha
Tanzania kupata msaada.
Katika
barua ya MCC ya Novemba 19, ambayo imesainiwa na Naibu Makamu wa Rais
wa Idara ya Operesheni ya Miradi kwa Afrika, Jonathan O. Bloom kwenda
kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile, mfuko huo
umetaka maelezo kuhusu utatuzi wa mgogoro wa Zanzibar pamoja na
ufafanuzi wa sheria ya uhalifu wa mtandaoni.
“MCC
inashukuru kwa uongozi na dhamira yako wakati wa mchakato mzima wa
maendeleo ya mradi huu. Msaada wa dola milioni 472 (ambazo ni zaidi ya
Sh trilioni moja), una nafasi kubwa ya kusaidia kuleta mageuzi katika
sekta ya nishati na kuwaunganisha maelfu ya watu katika gridi.
“Lakini mgogoro wa Zanzibar na ukamataji watu wa hivi karibuni kupitia sheria mpya ya uhalifu mtandaoni umetutia wasiwasi.
“Kama
ujuavyo, mataifa washirika wa MCC wanapaswa kuendeleza na kuonyesha
dhamira ya utawala bora, ambayo ni pamoja na kufuata misingi ya
demokrasia na kulinda uhuru wa kutoa mawazo.
"Hata hivyo, matukio ya karibuni yanaifanya MCC na wadau wetu kujawa na maswali kuhusu dhamira hiyo,” inasomeka barua hiyo ya MCC iliyosainiwa na Bloom.
Kwa
mujibu wa barua hiyo, MCC inafuatilia kwa karibu nyendo za Serikali
katika ushughulikiaji wa masuala hayo ya utawala bora, hasa kipindi hiki
kuelekea mkutano wa mwezi ujao wa bodi ya mfuko huo.
“Utatuzi
wa mgogoro wa Zanzibar kwa namna ya kuridhisha pande zote husika na
haja ya kuiona Serikali ikifafanua hadharani nia yake na sheria ya
uhalifu wa mtandaoni, kama vile kuchapisha utekelezaji wa kanuni
zinazoakisi mchango wa mdau na kuonyesha dhamira ya kuendelea kulinda
uhuru wa kutoa maoni, kutaisaidia MCC kuitathimini Tanzania kwa namna
chanya juu ya kuendelea kwa dhamira yake ya kutimiza sharti la kufuzu
kupata misaada,” ilisema barua hiyo.
Barua hiyo ilimalizia kwa kusema:
“Wasiwasi huu ni kikwazo cha mipango yetu ya ushirika. Tunaamini
utashughulikia wasiwasi huu ipasavyo na tunatarajia kupata jibu kutoka
kwako.”
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Likwelile, hakupatikana na hata alipotafutwa kwa njia ya simu hakupokea.
Pamoja
na juhudi hizo, pia alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu hakujibu, ambapo
alipotafutwa Msemaji wa Wizara ya Fedha, Ingiahedi Mduma, kuhusu barua
hiyo ya MCC, alisema hana taarifa na hajaiona.
“Sina
taarifa na wala sijaiona barua hiyo, hivyo siwezi kusema chochote labda
mpaka nitakapoongea na bosi aniambie kama amepokea barua hiyo,” alisema Mduma.
Mwanzoni
mwa Oktoba mwaka huu, Rais mstaafu Jakaya Kikwete akiwa nchini Marekani
kuhudhuria shughuli za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN), alikutana
na Mtendaji Mkuu wa MCC, Dana J. Hyde na watumishi waandamizi, akiwamo
Makamu wa Rais wa Operesheni za mfuko huo, Kamran Khan.
Katika
mkutano huo, MCC ilitangaza kuwa Tanzania imetimiza masharti yote ya
kupatiwa awamu ya pili ya fedha za maendeleo kutoka katika mfuko huo,
kuanzia mwakani, zaidi ya dola za Marekani milioni 472.8, sawa na zaidi
ya Sh trilioni moja za Tanzania.
Katika
mkutano huo, Rais mstaafu Kikwete, aliambatana na ujumbe wa maofisa
kadhaa akiwamo Waziri wa Fedha wa Zanzibar, Yusuf Omar Mzee.
Katika awamu ya kwanza ya fedha za MCC, Tanzania ilipata dola za Marekani milioni 698 (sawa na Sh trilioni 1.46).
Kama
MCC wataridhika na maelezo ya Serikali kupitia Wizara ya Fedha,
Tanzania itakuwa imepata jumla ya Sh trilioni 2.45 kwa awamu zote mbili
kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika kipindi cha miaka 10.
Awamu ya kwanza ya fedha hizo zilitumika kujenga Barabara za Tunduma- Sumbawanga, Tanga-Horohoro na Namtumbo- Songea- Mbinga.
0 comments:
Post a Comment