ZIARA
ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis nchini Uganda
imetajwa kuwa itafufua mchakato wa kumtangaza Hayati Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Nyerere kuwa mtakatifu.
Kwa
mujibu wa mtandao wa ETN wa nchini Uganda, ziara hiyo ya kitume ya Papa
Francis itamfikisha katika eneo la Namugongo ambalo mashahidi wa imani
ya dini ya Kikristu walichomwa moto.
Ni
katika eneo hilo la Namugongo ambako Hayati Nyerere alitangazwa kuwa
Mwenyeheri huku mchakato wa kumtangaza mtakatifu ukiwa ulianza miaka
tisa iliyopita.
Namugongo ndiko ambako pia waumini wa dini ya Kikristu wa Afrika Mashariki na sehemu nyingine duniani hufika kuhiji.
Taarifa
ya ETN imeeleza kuwa ziara ya Papa Francis Namugongo itasaidia kufufua
mchakato uliodumu kwa miaka tisa sasa wa kumtangaza Hayati Baba wa Taifa
kuwa mtakatifu.
Tayari
mjane wa Hayati Mwalimu Nyerere, Mama Maria Nyerere yuko nchini Uganda
ambako amekwenda kujumuika na waumini wengine wa dini ya Kikristu
kumpokea na kushiriki ibada itakayoongozwa na Papa Francis.
ETN
imemkariri Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, akisema kuwa mchakato wa
kumtangaza Hayati Mwalimu Nyerere kuwa mtakatifu umetokana na mchango
wake wa kuhimiza heshima na usawa kwa binadamu ambao aliutoa wakati
akiwa kiongozi.
Kwa
mujibu wa ETN, Rais Museveni amesifu mchango wa Hayati Mwalimu Nyerere
ambao haukuwa tu wa kuunganisha Watanzania bali alifanya kazi kwa kujali
utu wa Waafrika.
“Hayati
Julius Nyerere alikuwa mwanaharakati wa Afrika ambaye alimpenda Mungu
na alijali utu, aliwaunganisha Watanzania wa dini zote na alisaidia
ukombozi wa mataifa mengine ya Afrika kama vile Zimbabwe, Namibia,
Angola, Afrika Kusini na Uganda,” alisema Museveni.
Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini, jana alisema mchakato wa kumtangaza Hayati Mwalimu Nyerere kuwa mtakatifu unaendelea vizuri.
Alisema
suala la kuendesha mchakato huo ni jukumu la Tanzania na si Uganda
hivyo jina la Hayati Mwalimu Nyerere linaweza kuibuka katika ziara ya
Papa nchini Uganda kwa kutajwa tu, kwa sababu Rais wa nchi hiyo, Yoweri
Museveni, amekuwa na mazingira ya karibu na familia ya Hayati Mwalimu
Nyerere.
“Jukumu
la kuendesha mchakato wa kumtangaza Hayati Baba wa Taifa kuwa Mtakatifu
ni letu na linaendelea vizuri. Kuna mambo mengi ya kuchunguzwa mpaka
mtu kutangazwa kuwa mtakatifu, inawezekana Papa akamzungumzia Mwalimu
kwa sababu ya Rais Museveni mara kwa mara ameonyesha kuguswa na mwenendo
wa mchakato huo,” alisema Askofu Kilaini.
Papa
Francis aliwasili nchini Uganda jana jioni saa 4:50 na kulakiwa na Rais
Museveni na viongozi wa Kanisa Katoliki nchini humo.
Kwa
mujibu wa ziara yake nchini humo iliyotolewa na Kanisa Katoliki la
Uganda leo anatarajiwa kufanya ziara ya kitume katika miji ya Munyonyo,
Nikiyanja, Nalukolongo, Namugongo, Kalolo na Rubaga na kesho atamaliza
ziara yake nchini humo na kusafiri kwenda nchini Afrika ya Kati (CAR).
Taarifa
kutoka nchini Uganda zinaeleza kuwa ulinzi umeimarishwa na Serikali
imeandaa wahudumu wa afya 400 na magari 38 ya kubebea wagonjwa ambayo
yamepelekwa maeneo yote ambayo Papa atayatembelea.
Papa
Francis atakuwa Papa wa tatu kutembelea taifa hilo ambapo mwaka 1969,
Papa Paul VI alitembelea nchi hiyo akifuatiwa na Papa Paul II mwaka
1993.
Kampeni za urais zasimama
Katika
hatua nyingine wagombea urais wa vyama vyote wamelazimika kuahirisha
mikutano yao ya kampeni kwa ajili ya kupisha ziara ya Papa Francis
nchini humo.
Rais
Museveni ambaye anawania urais kwa muhula mwingine, aliwaambia wafuasi
wa chama chake kuwa atamuomba Papa asaidie kutangaza utalii wa taifa
hilo.
Akemea ukabila na rushwa nchini Kenya
Awali
kabla hajaondoka nchini Kenya, Papa Francis alihutubia maelfu ya vijana
katika Uwanja wa Kasarani jijini Nairobi ambapo aliwahimiza vijana wa
taifa hilo wasijihusishe na ukabila.
Alisema
vijana wanaweza kuchangia katika kukabiliana na changamoto za ukabila
ambazo zimekuwa zikikwamisha maendeleo ya mataifa ya Afrika.
Aliwashauri
viongozi wa Serikali kuhakikisha vijana wanapata elimu na ajira kwa
sababu hiyo ndiyo njia pekee ya kuwazuia kujiingiza katika makundi yenye
itikadi kali za kigaidi.
Kabla
ya kuhutubia vijana katika Uwanja wa Kasarani, Papa Francis,
alitembelea Mtaa wa Kangemi ambako wanaishi watu masikini na kukemea
dhuluma ya huduma bora ambazo wanatakiwa wapatiwe masikini.
“Ninafahamu
kuhusu tatizo kubwa linalosababishwa na wawekezaji wasio na sura ambao
hujitwalia ardhi na hata kujaribu kunyakua viwanja vya kuchezea watoto
wenu shuleni. Hili ndilo hufanyika tunaposahau kwamba Mungu aliwapa watu
wote ardhi waitumie kwa maisha yao bila kutenga au kupendelea yeyote,” alisema Papa Francis.
0 comments:
Post a Comment