Tumepokea
taarifa kwamba Balozi Seif Ali Iddi amehojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya
Radio France International (RFI) na kusema kwamba eti viongozi wa CCM na
CUF WAMEKUBALIANA UCHAGUZI ZANZIBAR URUDIWE, na kinachojadiliwa hivi
sasa ni NANI ASIMAMIE UCHAGUZI WA MAREJEO kwa sababu ZEC ya JECHA
INAONEKANA KUTOAMINIKA.
Tunapenda kuwawekea wazi Wazanzibari wote kwamba taarifa hizo hazina ukweli wowote, ni za uzushi na wazipuuze.
Msimamo
wa CUF na Maalim Seif Sharif Hamad uko pale pale kwamba HAKUNA KURUDIWA
UCHAGUZI na kwamba MSHINDI HALALI WA UCHAGUZI WA TAREHE 25 OKTOBA, 2015
ATANGAZWE NA KUAPISHWA.
Kauli
za Balozi Seif Ali Iddi ni za kutapatapa zianzolenga kuwatuliza
wana-CCM ambao wanaonekana kukata tamaa baada ya kushindwa vibaya na CUF
kwenye uchaguzi mkuu wa Rais wa Zanzibar, Wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi, Wabunge na Madiwani uliofanyika tarehe 25 Oktoba, 2015.
Kwenye
uchaguzi mkuu wa Urais wa Zanzibar, mgombea wa CUF, Maalim Seif Sharif
Hamad, alimbwaga vibaya mgombea wa CCM, Dk. Ali Mohamed Shein, kwa zaidi
ya kura 25,000.
Balozi
Seif Ali Iddi mwenyewe akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni ya CCM
anatuhumiwa na wana-CCM kushindwa kazi na kukisababishia chama chao
kushindwa vibaya kuliko wakati wowote katika historia ya chaguzi za
Zanzibar.
Lakini
kama hilo halitoshi, wana-CCM wanamtuhumu Balozi Seif na wajumbe
wengine wa Kamati ya Kampeni aliyokuwa akiiongoza kusimamia matumizi
mabaya ya kiasi kikubwa cha fedha za kampeni za Chama hicho ambazo
sehemu kubwa walimdanganya mgombea wao, Dk. Ali Mohamed Shein, kwamba
zimetumika kuleta ushindi wa CCM kisiwani Pemba lakini kumbe ziliishia
katika mifuko ya watu binafsi.
Haistaajabishi
kwamba sasa Balozi Seif Ali Iddi ameamua kuja na njia ya kutoa taarifa
za udanganyifu ili kujinusuru na mzigo wa tuhuma za kushindwa kazi na
kusimamia matumizi mabaya ya fedha za kampeni kutoka kwa CCM wenzake.
CUF
tunamtaka Balozi Seif Ali Iddi awache kudanganya umma na badala yake
awajibu CCM wenzake kwa nini amekitia chama hicho aibu na fedheha kubwa
ya kupata kipigo kibaya katika uchaguzi kilichopelekea CCM kupoteza
majimbo tisa (9) kisiwani Unguja na Dk. Ali Mohamed Shein kushindwa
uchaguzi wa Urais wa Zanzibar kwa zaidi ya kura 25,000 huku wakidai
kutumia mamilioni ya fedha ambazo hawana maelezo zimetumika vipi.
CUF
tunawataka Wazanzibari kutobabaishwa na kauli za kushindwa kazi za
Balozi Seif Ali Iddi na watulie wakijua kuwa ufumbuzi wa haki wa
uchaguzi mkuu utapatikana kwa kutangaza matokeo ya kura kwa majimbo
yaliyobakia na hatimaye mshindi kutangazwa na kuapishwa.
HAKI SAWA KWA WOTE
ISMAIL JUSSA
MKURUGENZI WA MAWASILIANO - CUF
26 NOVEMBA, 2015
0 comments:
Post a Comment