Rais wa Kenya amefanya mabadiliko
katika Baraza lake la Mawaziri na kuwaacha wote ambao wizara zao
zilikumbwa na tuhuma za ufisadi.
Rais Uhuru Kenyatta amechukua
hatua hiyo siku moja tu baada ya kutangaza ufisadi kuwa tishio kwa
usalama wa kitaifa. Rais ameahidi kufanya mabadiliko zaidi katika afisi
yake hivi karibuni.
Katika hotuba ilioonyeshwa kwa njia ya
Televisheni, Rais Kenyatta ameongeza idadi ya wizara kutoka 16 hadi 20
na kuongeza idara mpya chini ya wizara mbalimbali katika kile alichosema
ni kusaidia mawaziri kutekeleza majukumu yao bora zaidi.
Idara hizo zimeongezwa kutoka 26 hadi 41.
Rais
Kenyatta amefanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri baada ya
mawaziri sita kulazimika kujiondoa kutokana na wizara walizosimamia
kuhusishwa na ufisadi huku wawili kati yao wakikabiliwa na kesi
mahakamani.
Ni mabadiliko yaliyotarajiwa hasa baada ya hatua ya
aliyekuwa waziri wa Ugatuzi Anne Waiguru kujihuzulu mwishoni mwa juma
kutokana na kile alichosema ni ushauri wa daktari wake- baada ya
usumbufu aliopata wizara yake ilipohusishwa na sakata kadhaa za ufisadi.
Kwa
mujibu wa katiba idadi ya mawaziri inapaswa kuwa kati ya 14 na 22 na
hivyo kujiuzulu kwa Bi Waiguru kulisababisha idadi hiyo kupungua hadi
13.
Baraza jipya la mawaziri linajumuisha wanawake wanne na wanaume 16.
Baadhi
ya mawaziri wamesalia katika nafasi zao huku wengine wapya wakiteuliwa
kuchukua nafasi za mawaziri waliohusishwa na ufisadi.
Hatua itakayofuata sasa ni kwa mawaziri wapya kuchunguzwa na kamati ya bunge kabla ya kuidhinishwa kikamilifu.
Serikali
ya Rais Uhuru Kenyatta imekuwa ikikabiliwa na changamo ya ufisadi
katika wizara kadhaa na kumekuwepo shinikizo sio tu kutoka kwa wananchi
lakini pia kutoka kwa mashirika ya kijamii,viongozi wa upinzani na hata
mabalozi wa nchi za kigeni kutaka hatua zichukuliwe.
0 comments:
Post a Comment