Thursday, 4 February 2016

#YALIYOJIRI>>>>Pius Msekwa Asema CCM imepoteza Sifa Ya Kuwa Chama Cha Wanyonge.Fahamu zaidi hapa.

Wakati kesho CCM ikiadhimisha miaka 39 tangu kuzaliwa kwake, kada mkongwe na muasisi wa chama hicho, Pius Msekwa amechambua uwezo na udhaifu wake, akibainisha kuwa kimepoteza sifa ya asili ya kuwa chama cha wanyonge.

Msekwa amesema   kuwa matukio mbalimbali yanayokikumba chama hicho, ikiwamo migogoro baina ya viongozi wake, makundi na tuhuma za ufisadi, yameathiri taswira yake kwa jamii.

Msekwa  ambaye ni katibu mkuu wa kwanza wa Tanu na makamu mwenyekiti mstaafu (Bara), alibainisha kuwa CCM imepoteza sifa yake ya asili ya kuwa chama kinachojali wanyonge na kubebeshwa mzigo wa kuitwa “chama cha matajiri”.

“Migogoro miongoni mwa viongozi, hususan baina ya makundi yanayozozana au kuhasimiana ndani ya chama na tuhuma za ufisadi, imechangia kuifanya CCM ibebeshwe mzigo wa kuonekana kuwa ni chama kinachokumbatia mafisadi,” alisema.

Aliongeza kuwa CCM pia imeathiriwa na kujipenyeza kwa kasi kubwa kwa wafanyabiashara wasio waadilifu katika baadhi ya vikao vyake vya uamuzi.

Hata hivyo, Msekwa alisema ujio wa Rais John Magufuli umeleta matumaini mapya miongoni mwa wananchi juu ya taswira ya chama hicho.

“Nafarijika kwamba uongozi mpya wa Rais anayetokana na CCM, Dk John Magufuli umeleta matumaini hayo mapya miongoni mwa wananchi walio wengi,” alisema.

Alieleza kuwa CCM kupitia viongozi wake, haina budi kuonyesha kwamba inaweza kuleta mabadiliko yenye tija na yenye kuleta matumaini mapya miongoni mwa wananchi walio wengi.

Alisema ukongwe wa chama hicho kwa maana ya kuwa kimekuwapo na kimekuwa madarakani mfululizo tangu nchi ilipopata uhuru wake mwaka 1961, una faida na hasara zake.

“Faida ni kwamba kwa sababu ya uzoefu wake huo wa miaka mingi, kina (CCM) fursa kubwa ya kuendesha shughuli zake vizuri na kuendelea kupata ushindi katika chaguzi zijazo,”alisema.

Alibainisha pia kuwa kitendo cha CCM kuwapo madarakani muda mrefu kinaweza kusababisha hatari inayotokana na hulka ya binadamu.

Alifafanua kuwa wakati mwingine watu wanaweza kutaka mabadiliko tu ya uongozi wa nchi hata kama chama kilichopo madarakani kinafanya vizuri kiasi gani.

“Hatari iliyopo ni watu wanaweza kuchoka tu kuendelea kuwa chini ya uongozi wa chama kilekile na hatari hiyo inakuwa kubwa zaidi pale matendo ya viongozi wake yatakapokuwa mabaya kiasi cha kuwaudhi watu,”alisema. 

Msekwa alisema katika kipindi hicho cha uhai wa CCM, maadili ya viongozi yameporomoka kwa kiwango kikubwa.

Alitaja sababu za kuporomoka kwa maadili kuwa ni pamoja na kuingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini na ushindani mkali wa kuwania kushika dola uliojikita katika mfumo huo.

Alisema hali hiyo pia inatokana na hatua ya kusitishwa kwa mafunzo ya viongozi, makada na watendaji wa chama hicho yaliyokuwa yakitolewa kwenye vyuo mbalimbali.

“Hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na kusitishwa kwa ruzuku iliyokuwa inatolewa na Serikali kwa chama kwa ajili ya kuendesha mafunzo hayo, katika vyuo vya chama vya Kivukoni na vyuo vyake sita vya kanda vilivyokuwa mikoa mbalimbali,” alisema.

Alisema kutokuwapo kwa msaada wa mafunzo ya maadili na uadilifu kwa viongozi, pia kulichangia kuporomosha maadili ndani ya chama.

“Hapo ilibidi kila kiongozi alazimike kutumia akili zake tu katika shughuli zake za uongozi. Kama wasemavyo Waswahili; akili ni nywele, kila mtu ana zake,” alisema.

Alieleza pia kuwa ushindani katika mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini, umesababisha kukithiri rushwa katika uchaguzi.

Alisema hili hujitokeza wakati wa kura za maoni ndani ya CCM ambako baadhi ya makada wake wameanza tabia ya kuwashawishi wapigakura kwa rushwa ili wachaguliwe katika nafasi wanazozitafuta.

Alisema yapo mambo muhimu ya kuzingatia, wakati wa kutafakari chama hicho kilikotoka na kwamba katika kipindi chote hicho kimekuwa kikipata ushindi unaopanda na kushuka katika chaguzi zote zilizofanyika chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa. 

#YALIYOJIRI>>>>Mahakama Ya Rufaa Kuamua Ugomvi Wa Nyumba Kati Ya Afande Suleiman Kova Na Godfrey Nzowa.Fahamu zaidi hapa.

Mahakama ya Rufaa wiki ijayo inaanza kusikiliza kesi za rufani 50 za jinai na madai katika Kanda ya Arusha ikiwamo rufaa ya makamishna wawili wa Jeshi wa Polisi wanaogombea nyumba ya serikali iliyopo Uzunguni Arusha.

Maofisa hao, Godfrey Nzowa ambaye ni Mkuu wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya katika Jeshi hilo amemshitaki mahakamani aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova akipinga kuuziwa nyumba hiyo. Kamishna Kova hata hivyo amestaafu rasmi mapema mwaka huu.

Kwa mujibu wa orodha ya kesi zitakazosikilizwa na majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa kwa mwezi mmoja mjini hapa, Nzowa anamlalamikia Kova na wenzake kupinga kuuziwa nyumba hiyo aliyokuwa akiishi alipokuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) wa Mkoa wa Arusha.

Nyumba hiyo aliuziwa Kamishna Kova akiwa ameshahama mkoani Arusha na wakati inauzwa Nzowa alikuwa akiishi katika nyumba hiyo, familia yake akiwa RCO kabla ya kuhamishiwa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuendelea na wadhifa huo, Kova akiwa bosi wake.

Orodha hiyo yenye jumla ya mashauri 50 inaonesha mahakama hiyo itasikiliza rufani ya Wakili maarufu jijini Arusha, Median Mwale ambaye amekata rufaa dhidi ya Jamhuri katika kesi yake ya kudaiwa kutakatisha fedha chafu na kujipatia mabilioni ya fedha kwa njia ya udanganyifu akiwa na wenzake watatu.

Rufani hiyo namba 395 ya mwaka 2013 ya Wakili Mwale dhidi ya Jamhuri imepangwa kusikilizwa na majaji watatu, Mbarouk Salim Mbarouk, Bernard Luanda na Semistocles Kaijage watakaosikiliza pia mashauri mengine kabla ya kutoa uamuzi Machi 5, mwaka huu.

Orodha iliyotolewa na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa, E.Y. Mkwizu inaonesha kesi nyingine yenye mvuto ni ile ya wafanyabiashara Philemon Mang’ehe na Gesso Bajuta iliyodumu kwa miaka 20 sasa.

Katika kesi hiyo, Mang’ehe wa Kampuni ya Bukine anamdai fidia ya mamilioni ya fedha Bajuta baada ya kudai kuharibiwa biashara yake ya kusambaza vifaa vya ofisi katika Mahakama ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) mwaka 1996.

#YALIYOJIRI>>>>Maalim Seif Shariff Hamad Adai Kikwete Ndiye Aliyevuruga Uchaguzi Zanzibar.Fahamu zaidi hapa.

Mgombea  urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad amemtuhumu Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete kwa kuingilia uchaguzi Zanzibar.

Akizungumza kwenye mkutano wa viongozi wa wilaya na majimbo wa chama hicho uliofanyika kwenye Ukumbi wa Majid, Kiembe Samaki visiwani Zanzibar jana, Maalim Seif ambaye ndiye Katibu Mkuu wa CUF alisema, Rais Kikwete amesababisha kuwepo kwa mgogoro mkubwa wa kisiasa na kikatiba.

Alisema, saa chache kabla ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kutangaza kufuta uchaguzi huo, kituo kikuu cha kutangazia matokeo kilichokuweko Hoteli ya Bwawani kilizingirwa na vikosi vya jeshi na polisi na kwamba kitendo hicho kuwa ni “Mapinduzi ya Kikatiba”.

“Aliyekuwa Amiri Jeshi Mkuu wakati ule alikuwa Rais Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete na ndiye aliyepeleka vikosi vile baada ya kuona chama chake kimeelekea kushindwa kwa upande wa Zanzibar,” alisema Maalim Seif na kuongeza;

“Dkt. Shein wala Balozi Seif (Seif Ali Idd) hawamiliki jeshi wala polisi, vile ni vikosi vya Dk. Kikwete wakati ule na hawezi kukwepa lawama ya kuingilia uchaguzi wa Zanzibar.”

Maalim Seif pia amewashutumu baadhi ya viongozi wakiwemo wa dini wanaojaribu kupotosha ukweli na kuunga mkono uamuzi batili wa kurejewa uchaguzi uliotangazwa na ZEC.

Akizungumzia kuhusu vikao vya kutafuta muafaka wa mkwamo wa kisiasa vilivyokuwa vikifanyika Ikulu ya Zanzibar, Maalim Seif alisema katika vikao hivyo walijadiliana na kukubaliana kuwa ZEC imepoteza sifa ya kusimamia uchaguzi.

Alisema, ameshangazwa na kitendo cha ZEC kutangaza uchaguzi wa marejeo, huku viongozi wa CCM walioshiriki mazungumzo hayo wakiunga mkono.
Akizungumzia hali ya kisiasa Zanzibar, Maalim Seif alisema, siasa za nguvu na kimabavu zinazoendeshwa na CCM hazitoisaidia Zanzibar na badala yake zinaweza kuzidisha mgogoro uliopo.

Kauli ya CUF kugomea uchaguzi uliotangazwa kufanyika tarehe 20 Machi mwaka huu, imeungwa mokono na viongozi hao wa wilaya na majimbo visiwani humo wakiwakilisha wananchi na wafuasi wa chama hicho.

Viongozi hao waliunga mkono hatua hiyo iliyotanguliwa na tamko lililotolewa na Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho tarehe 28 Januari mwaka huu.

Kwenye mkutano huo walieleza kuwa uchaguzi halali, huru na wa haki ulifanyika tarehe 25 Oktoba mwaka jana ambapo wananchi walio wengi walimchagua Maalim Seif na uchaguzi huo kufutwa bila sababu za msingi.

#YALIYOJIRI>>>>Mbowe Na Zitto Kabwe Wazika Rasmi Ugomvi Wao Wa Muda Mrefu.Fahamu zaidi hapa.

Uhasama  uliodumu kwa muda mrefu kati ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe sasa ni wazi unaonekana kumalizika.

Hali hiyo inatokana na viongozi hao kwa nyakati tofauti jana kuweka ujumbe kwenye mitandao yao ya kijamii ya facebook na twitter, ambao unaonyesha kila mmoja akijutia makosa yake na kutaka waungane kwa ajili ya kutetea masilahi ya taifa.

Tangu kuanza kwa mijadala mbalimbali bungeni mjini Dodoma wiki iliyopita, Mbowe na Zitto wameonyesha kukubaliana katika misimamo yao na hivyo kuzua maswali kwamba huenda mbunge huyo wa Kigoma Mjini anataka kujiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, akiwa na Zitto wiki iliyopita waliwaongoza wabunge wengine wa Ukawa kususia kikao cha Bunge kupinga hatua ya Serikali kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya Bunge kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Baadaye viongozi hao pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi, James Mbatia, waliitisha mkutano na waandishi wa habari kueleza umma ambavyo Serikali inarudisha taifa katika zama za udikteta kwa kuzuia haki ya wananchi kupata habari.

Katika kikao hicho cha Bunge, Serikali kupitia kwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye, ilitoa taarifa kuwa wanasitisha matangazo hayo ya moja kwa moja ili kubana matumizi ya Serikali yanayofikia zaidi ya Sh bilioni nne kwa mwaka.

Katika ukurasa wake wa facebook na twitter jana, Zitto alinukuu ujumbe wa Mbowe  ambao ulitafsiriwa kwamba ni hatua ya kiongozi huyo wa upinzani kutaka kumaliza tofauti zake za kisiasa na mbunge huyo.

“Kushirikiana na Zitto si jambo la ajabu kama ambavyo umeona tukifanya. Yapo majeraha mengi ambayo tumeyapitia pande zote (Chadema na Zitto) ambayo huwezi kuyatibu kwa siku moja. Yapo ambayo yatapona kulingana na muda. Unaweza kumfanyia mtu kitu kibaya, lakini baadaye ukatambua kuwa umekosea. Chochote katika siasa kinawezekana,” aliandika Mbowe.

Jana kupitia ukurasa wake wa facebook, Zitto ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, alisema nafasi ya chama chake bungeni ni upande wa upinzani hivyo atakuwa pamoja na Ukawa.

“Mbowe siku zote amekuwa kiongozi wangu na siwezi kubeza nafasi yake katika kujenga demokrasia nchini. Tulipishana, tulikoseana, tusameheane.

“Mimi binafsi siwezi kuwa mfungwa wa magomvi yetu ya miaka ya nyuma. Nilishasamehe walionikosea na kuomba radhi niliowakosea.

“Tunaweza kupishana kwenye mkakati wa utekelezaji, hatuwezi kupishana kwenye masilahi ya nchi yetu ya kujenga demokrasia na kukataa udikteta.

“Nafasi ya ACT-Wazalendo bungeni ni upande wa upinzani, na hivyo tutakuwa na wenzetu wa upinzani kwenye kujenga hoja zote za kitaifa.

“Mimi nikiwa mbunge wa ACT-Wazalendo, natekeleza kwa vitendo maelekezo ya chama kwa kushirikiana na wabunge wenzangu wa upinzani bungeni.

“Chama chochote makini huweka tofauti binafsi pembeni kwa masilahi mapana ya taifa. Chama cha ACT-Wazalendo kinaamini katika umoja,” alisema Zitto.

Zitto alifukuzwa Chadema na kujiunga na ACT-Wazalendo Machi 21, 2015 chama ambacho hakina ushirikiano na vyama vinavyounda Ukawa, lakini ameonekana kuwa karibu na umoja huo katika vikao vya Bunge la 11 vinavyoendelea mjini Dodoma.

Mwaka 2013, mwanasiasa huyo machachari pamoja na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema, Profesa Kitila Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba walifukuzwa kwenye chama hicho, baada ya mfulululizo wa muda mrefu wa mivutano ya uongozi na baadaye wakaanzisha chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT) mwaka 2014.

Chadema ilichukua uamuzi huo baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutupilia mbali pingamizi la Zitto dhidi ya Kamati Kuu kutojadili uanachama wake.

Tuesday, 2 February 2016

#YALIYOJIRI>>>Vyama Vitano Kushiriki Uchaguzi Wa Marudio Zanzibar.Fahamu zaidi hapa.

Vyama vitano vya siasa vitashiriki katika uchaguzi wa marudio wa Zanzibar, utakaofanyika Machi 20 mwaka huu, uliotangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC). Vyama hivyo ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), ADC, CCK, TLP na SAU.

Hatua hiyo inatokana na vyama vitatu vya siasa Zanzibar vya CCK, SAU na TLP, kutangaza kuwa wagombea wake, watashiriki katika uchaguzi huo wa Machi 20. Taarifa ya viongozi wa vyama vya CCK, SAU na TLP, iliyosomwa kwa pamoja katika Ukumbi wa Culture eneo la Mji Mkongwe  jana, ilisema wagombea wa vyama hivyo vitatu, watashiriki uchaguzi huo.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, ulifutwa baada ya kujitokeza kwa kasoro mbalimbali, zilizoonesha wazi kwamba hauwezi tena kuwa huru na haki. 

Wagombea wa vyama hivyo vya siasa, waliotangaza kushiriki katika uchaguzi huo ni Ali Khatib kutoka CCK, Issa Mohamed Zonga kutoka SAU na Hafidh Hassan Simai kutoka TLP.

Mgombea wa CCK, Ali Khatib Ali alisema kwamba tayari wamejipanga vizuri kwa ajili ya uchaguzi huo na kuwataka wanachama na wafuasi wake na wananchi, kuitumia fursa hiyo ya kidemokrasia kuchagua viongozi watakaoongoza nchi. 

“Tangazo la Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) limetutaka kurudia uchaguzi kwa sababu ule wa awali umefutwa kwa hivyo hatuna sababu ya kususia uchaguzi huo na tunachofanya kwa sasa ni kuwataka wanachama wetu na wafuasi kujitayarisha kwa uchaguzi wa marudio,” alisema Ali.

Jumapili iliyopita, Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein alisema chama hicho kipo tayari kwa uchaguzi wa marudio Machi 20 kwa lengo la kuhakikisha kinashika dola. 

Akihutubia mamia ya wanachama wao katika viwanja vya Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui wakati wa kuzindua maadhimisho ya miaka 39 ya CCM, Dk Shein alisema maamuzi ya kurudiwa kwa Uchaguzi Mkuu, yamefanywa na ZEC ambayo ndiyo chombo halali kwa mujibu wa Katiba cha kushughulikia masuala yote ya uchaguzi nchini.

Aliwataka wanachama na wafuasi wao kujipanga vizuri na kushiriki uchaguzi huo kikamilifu, kwani kwa mujibu wa Katiba ya CCM ni kushinda chaguzi zote zinazofanyika nchini ili kushika dola na kuwatumikia wananchi.

“Hayo ndiyo maamuzi ya chama chetu tuliyokubaliana kushiriki Uchaguzi Mkuu wa marudio baada ya kufutwa kwa ule wa Oktoba 25 mwaka jana kwa hivyo wanachama na wafuasi jitayarisheni kushiriki kikamilifu kwa ajili ya kushika dola,” alisema Dk Shein.

#YALIYOJIRI>>>Polisi Yapiga Marufuku maandamano ya vijana wa Chadema kwenda Ikulu Kesho.Fahamu zaidi hapa.

Jeshi la Polisi limetoa tamko kuhusu tangazo la Baraza la Vijana wa Chadema (BAVICHA) kuwa kesho wamepanga kufanya maandamano hadi Ikulu kwa lengo la kuishinikiza serikali kubadili msimamo wake kuhusu TBC kutorusha Live baadhi ya vikao vya Bunge.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Siro amepiga marufuku maandamano hayo na kuwataka vijana hao kutumia njia mbadala za kupata ufumbuzi wa suala hilo badala ya maandamano.

Akitoa sababu za kuzuia kufanyika kwa maandamano hayo, Kamanda Sirro alisema kuwa hakuna taarifa  na pia hakuna uthibitisho kuwa maandamano hayo yatapokewa na Rais Magufuli.

Pia, Kamanda Sirro alieleza kuwa BAVICHA hawakuanisha barabara ambazo wanatarajia kutumia katika maandamano hayo.

“Siku hiyo sio nzuri sana kwa sababu ni siku ambayo watu wanakuwa kazini. Ni siku ambayo wengi watataka kutumia barabara hizo kwa ajili ya huduma za kijamii. Na kwa sababu kuna option nyingine ya kuweza kupata suluhu hiyo, nisema tu kwamba maandamano hayo yamepigwa marufuku,” alisema.

#YALIYOJIRI>>>BAKWATA Waunga Mkono Uchaguzi wa Marudio Zanzibar.Fahamu zaidi hapa.

 WAKATI Chama  cha wananchi CUF ambacho ni chama kikuu cha Upinzani visiwani Zanzibar kikiwa kimesusia uchaguzi wa marudio ambao unafanyika Marchi 20 ya mwaka huu,Baraza la Waislam  (BAKWATA)  limesema marudio ya  uchaguzi huo ndo njia ya kipee ya kurudisha amani visiwani humo..

Akizungumza na waandishi wa habari leo,Jijini Dar es Salaam, Sheikh Mkuu mkoani hapa,heikh alhadj Mussa Salum  amesema  Bakwata wanaunga mkono Tangazo la ZEC la kurudiwa kwa uchaguzi hu.
 
“Uchaguzi huu wa marudio  kwetu Bakwata tunaona ndio njia ya kipekee ya kukiweka kisiwa cha Zanzibar kuwa sehemu ya Amani na utulivu,natumia nafasi hii kuwaomba chama cha CUF kushiriki uchaguzi huu” Amesema Sheikh Salum.

Sheikh Salum ameongeza kwa kusema  kuwa hata kiongozi wa jumuiya ya Uamsho Visiwani Zanzibar, Sheikh Farid Hadi Ahmad amemwandikia barua na kumweleza kuwa kurudiwa kwa uchaguzi kutasaidia kurudisha Amani visiwani humo.
Katika hatua nyingine, Baraza hilo limeipongeza serikali ya awamu ya tano kwa jitihada mbalimbali inazofanya za kuimarisha nidhamu, kubana matumizi na kukuza uchumi.
"Pia tunaipongeza serikali ya awamu ya tano, inayoongozwa na Mh. John Magufuli, kutokana na hatua mbali mbali inazozichukua zenye lengo la kuimarisha nidhamu hasa kwa watumishi wa umma, hatua mabazo zimeanza kuleta tija kubwa ka taifa letu kama wote hivi leo tunavyoweza kushuhudia jinsi pato la serikali likongezeka mwezi hadi mwezi”, alisema Sheikh alhadj Mussa Salum  na kuongeza;

“Aidha tunaipongeza kwa dhamira yake ya kubana na kupunguza matumizi ya serikali, na badala yake kuelekeza fedha kwenye huduma za jamii na watanzania tumeshaanza kunufaika na huduma hizo kama vile suala la elimu bure."

#YALIYOJIRI>>>Afande Sele Aungana Na Mbunge Joseph Msukuma Kuitaka Serikali Ihalalishe Matumizi Ya Bhangi.Fahamu zaidi hapa.

Msanii mkongwe wa hip hop nchini, Afande Sele amefunguka na kusema serikali ihalalishe matumizi ya bangi na si kukosoa juu ya hoja iliyotolewa na mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma.

Ikiwa imepita siku moja toka mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma (CCM), kusema haoni sababu ya serikali kuzuia bangi kuwa zao la biashara kwa maana haoni madhara yake huku akidai kwamba viroba vina madhara zaidi kuliko bangi, Afande Sele amefunguka na kusema serikali ihalalishe matumizi ya bangi na si kukosoa juu ya hoja hiyo ya Joseph Msukuma.

Afande Sele amedai kuwa kuna nchi ambazo tayari wao wamehalalisha matumizi ya bangi na kuthibitisha kuwa pombe ina madhara makubwa zaidi kuliko bangi.

"Legalize it, Don't criticize it. Korea Kaskazini, Marekani, Mexico Uruguay na mataifa mengine ya Ulaya yamethibitisha pombe ina madhara kuliko Cannabis Sativa" Amesema Afande Sele.

#YALIYOJIRI>>>Bungeni: Serikali Kuajiri Vijana 71,408 Mwaka Huu,Halmashauri Zaagizwa Kutenga Asilimia 5 Ya Mapato Kwa Ajili Ya Kuwasaidia Vijana.Fahamu zaidi hapa.

Serikali katika mwaka wa fedha 2016/2017 imepanga kuongeza ajira kwa vijana ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana wengi wa kitanzania kwa kuongeza ajira na kuwezesha wengine kujiajiri kupitia mifuko ya uwezeshaji toka Halmashauri za Wilaya nchini.

Akijibu swali la Mhe.Mgumba Tebweta Omary Mbunge wa Morogoro Kusini (CCM) lenye sehemu a na b lililouliza Serikali itaanza lini kuwawezesha vijana wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki  kifedha ili waweze kujiajiri na kuondokana na tatizo la ajira na umaskini ,Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe  Suleiman Jafo amesema vijana katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Kusini Mashariki wamekuwa wakiwezeshwa kiuchumi kupitia fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambapo kila Halmashauri hupaswa kutenga asilimia 5 ya mapato yake ya ndani kila mwaka kwa ajili ya vijana.

Mhe  Suleiman Jafo ameongeza kuwa katika Bajeti ya mwaka 2014/2015,Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ilifanikiwa kutoa Shillingi Millioni 10.3 kwa vikundi vya vijana 19 kwa ajili ya kutekeleza shughuli mbalimbali za kiuchumi na katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016 vikundi vya vijana vilitengewa Shilllingi Millioni 87.5 ili kuviwezesha kiuchumi kwa kujiajiri.

“Katika kutatua changamoto zilizopo kwa vijana tunawawezesha  kifedha ili kujiajiri ili kumekuwa na tatizo la fedha kuchelewa kufika kwa walengwa ila Serikali kupitia Wizara yangu tunalifanyia kazi ili fedha zifike kwa wakati na tumetenga Shillingi Millioni 50 kwa kila kijiji kwa ajili ya kuwezesha vijana walioko katika vikundi mbalimbali mfano SACCOS ili waweze kujiajiri na kujikwamua kiuchumi kwa kujiondoa katika hali ya umaskini”

“Napenda kuwaomba wabunge tusaidiane sababu wao  wanahusika katika kamati za fedha za Halmashauri za Wilaya, waende wakasimamie hizo fedha kwa ajili ya kuwezesha vijana  zitoke na ziwasaidie walengwa” Alisema Mhe Jafo.

Aidha Mhe  Suleiman Jafo amesema kuwa Serikali imetenga Shillingi Billioni 233 kwa ajiri ya kuajiri vijana wapya takribani 71,408 kati ya hao watumishi wapya wa Afya wanatarajiwa kuwa takribani 10,871 na Waalimu 40,000 kwa nchi nzima ili kupunguza tatizo la ajira kwa vijana wanaomaliza vyuo mbalimbali nchini.

Serikali kupitia Halmashauri za Wilaya imejipanga katika kuwawezesha vijana katika maeneo yao kujikwamua kiuchumi kwa kujiajiri na kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali itaboresha zaidi mifuko ya kuwezesha vijana katika Halmashauri za Wilaya kwa kununua vifaa zaidi vya kujifunza stadi mbalimbali za kazi zitakazowezesha vijana wengi zaidi kuwa na ujuzi utakaowasaidia kujipatia kipato na kujikwamua kiuchumi.

#YALIYOJIRI>>>Zitto Kabwe Ang’ang’ania Ufisadi Benki ya Stanbic,Mwanasheria Mkuu Amshauri Apeleke Nyaraka Serikalini.Fahamu zaidi hapa.

MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT- Wazalendo) ameitaka serikali kumwagiza Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) ili kubaini wizi wa Sh. 608 trilioni zilizokopwa kupitia Benki ya Stanbic yenye tawi lake nchini hapa.

Alitoa kauli hiyo jana bungeni wakati akiuliza swali la nyongeza kutaka kujua ni hatua gani ambazo zinachukuliwa kutokana na ufisadi mkubwa wa fedha hizo ambazo ni trilioni 6.8.

“Jumla ya fedha ambazo serikali ilizikopa nje kwa mfumo wa namna hiyo ni shilingi trilioni 6.8 na katika taarifa ya hukumu inaonesha mtindo huo wa kutumia vikampuni kwa ajili ya kupata mikopo imekuwa ikitumika na mabenki mengi ya kibiashara hapa nchini.

“Serikali haioni kwamba umefika wakati CAG aweze kufanya ukaguzi maalum wa mikopo yote ya kibiashara ambayo serikali imechukua katika kipindi hicho ili kuweza kujua kama pia kulikuwa kuna aina za rushwa za namna hiyo ambazo zimekuwa zinafanyika,”alihoji Zitto.

Zitto alisema DFA (Hukumu ya Uingereza) ilikuwa ina lengo la kuilinda Benk ya Uingereza ambayo ndiyo ilitoa hongo kwa maofisa wa Tanzania ili iweze kupata biashara ambapo alihoji, serikali haioni kwamba ni wakati muafaka sasa kufungua kesi dhidi ya benki hiyo ya Uingereza ili iwe fundisho kwa kampuni za nje zinazohonga kwa lengo la kupata biashara katika nchi za kiafrika

Akijibu maswali hayo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji George Masaju alisema CAG anayo majukumu ya kikatiba na hilo ni jukumu ambalo anaweza kulitekeleza wakati wowote ili kujiridhisha kama mikopo hiyo ambayo imekuwa ikipatikana kwa namna ambayo inaifanya nchi iingie kwenye hasara.

Alisema, kama Zitto anazo taarifa zozote zinazoweza kuisaidia serikali ama kufungua shauti la madai ama jinai ashirikiane na vyombo husika ikiwemo Ofisi ya AG na kuliangalia ili kuona kama linakidhi sifa na sheria na kwa kuzingatia pia uhusiano uliopo kwa nchi ya Uingereza ili kuona kama kesi ya jinai inaweza kufunguliwa.

Aidha alisema serikali imepokea ushauri wa Zitto na itaufanyia kazi kwa kuzingatia sheria za ndani ya nchi na uhusiano wa kisheria katika Jumuiya ya Kimataifa.

Awali katika swali la msingi la Zitto alitaka kujua serikali inaichukulia hatua gani Stanbic Bank ili walipe fidia zaidi.

“Mwaka 2013 serikali ilizuia hatifungani ya thamani ya dola za Kimarekani milioni 600 (USD 600.0 mili) kupitia Benki ya Sdandard yenye tawi hapa nchini (Stabic).

“Shirika la Corrupition Watch la Uingereza kwa kutumia vyombo kama IFM imeonesha kuwa hatifungani hiyo imeipa Serikali ya Tanziania hasara ya Dola za Marekani miliono 80 na serikali imelipwa fidia Dola za Marekani milioni 6.

“Je kwa nini serikali haichukulii hatua Stanbic Bank ili ilipe fidia zaidi?”alihoji Zitto.

Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Ashantu Kijaju alisema, serikali imefuatilia taarifa za hasara kwa Serikali ya Tanzania ya Dola za Marekani 80 iliyotajwa na Zitto lakini haikupata ushahidi wake.

Hata hivyo Dk. Kijaju alisema Benki Kuu ya Tanzania imeiandikia Benki ya Stanbic barua ya kusudio la kuitoza faini ya Sh. 3 bilioni kwa kosa la kufanya miamala inayokiuka sheria na kanuni za mabenk na taasisi za fedha.

#YALIYOJIRI>>>Mke wa Kafulila Amlipua Dr. Mwakyembe Kuhusu Sakata La Mabehewa FEKI,Mwakyembe Akomaa, Asema Yupo Tayari Kujiuzulu Ikithibitika Fahamu zaidi hapa.

Sakata la ununuzi wa mabehewa kwa ajili ya Shirika la Reli Tanzania (TRL) yanayodaiwa kuwa mabovu liliibuka jana Bungeni na kumuinua Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe ambaye alikuwa Waziri wa Uchukuzi katika serikali ya awamu ya nne.

Waziri Mwakyembe alikanusha madai yaliyotolewa na Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Jesca Kishoa kuwa ununuzi huo wa mabehewa mabovu uliisababishia sherikali hasara ya shilingi bilioni 238, huku akitaka ripoti ya ukaguzi wa ununuzi huo iwasilishwe bungeni.

Akitumia kanuni ya 63 (3) kuomba kutoa taarifa, Mwakyembe alikanusha kiwango cha fedha kilichotajwa na mbunge huyo wa viti maalum ambaye ni mke wa aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila.

“Mbunge aliyesimama kabla, aliyejitambulisha kama mke wa Kafulila, ameeleza kwamba serikali ilitumia zaidi ya shilingi bilioni 238 na kuleta hasara kwa kununua mabehewa mabovu. Mheshimiwa Mwenyekiti nataka kukuthibitishia kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kwa kununua mabehewa 274 haijawahi kutumia zaidi ya shilingi bilioni 60,” alisema Mwakyembe.

Waziri huyo alienda mbali na kueleza kuwa endapo mbunge huyo atawasilisha uthibitisho wa kiwango hicho cha fedha kutumika kununua mabehewa hayo, atajiuzulu nafasi yake ya ubunge.

“Mimi naomba athibitishe hiyo shilingi bilioni 238. Na nitashukuru sana kama akileta hapa. Na akileta hiyo, mimi nitajiuzulu hata ubunge,” alisema Mwakyembe.

Baada ya kauli hiyo ya Mwakyembe, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee naye alisimama na kueleza kuwa Waziri huyo hakutumia kifungu sahihi kutoa taarifa kwa kuwa alipaswa kutumia kifungu cha 63 (4) kutoa ushahidi wa kukanusha kwake kwanza.

Naye Kishoa aliendelea kusisitiza kuwa Serikali inapaswa kuwasilisha bungeni hapo ripoti ya ukaguzi wa manunuzi ya mabehewa hayo.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bunge, Dk. Mary Mwanjelwa alitoa siku tatu kwa mbunge huyo wa viti maalum kuwasilisha ushahidi kuhusu madai yake.

#YALIYOJIRI>>>>>CRDB Yawatoa Hofu Wateja Wake Baada Ya Serikali Kuagiza Akaunti za Taasisi zake Katika Mabenki ya Kibiashara Zifungwe.Fahamu zaidi hapa.

(Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk. Charles Kimei akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kuhusu serikali kuhamishia akaunti zote za mapato Benki Kuu. Kulia ni Mkurugenzi wa Hazina wa Benki ya CRDB, Alex Ngusaru na Mkurugenzi wa Masoko, Utafiti na Huduma kwa Wateja, Tully Mwambapa.)

****
SIKU chache baada ya Serikali kutangaza kuchukua hatua za kupunguza riba za mabenki kwa wananchi kwa kuagiza akaunti za mashirika na taasisi zake katika mabenki ya kibiashara zifungwe na kuhamisha fedha zilizopo katika akaunti hizo kwenda Benki Kuu ya Tanzania (BoT), benki ya CRDB imeunga mkono hatua hiyo.

Pia benki hiyo imewataka wananchi wasiwe na hofu juu ya mpango huo, kutokana na hofu iliyojengeka kwamba kuna hatari benki za kibiashara kufilisika nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk.Charles Kimei alisema uamuzi uliofanywa na Serikali utasaidia kukuza uchumi pamoja na kutambua fedha zake mahali zilipo.

Alisema Serikali ina haki na nia njema kwa kutaka akaunti hizo zifunguliwe BoT kwa kuwa zimekuwa zikifunguliwa kwenye mabenki makubwa ya kibiashara, huku baadhi ya Wakala wa ukusanyaji wa fedha wakishindwa kuzifikisha serikalini  kama inavyotakiwa.

Pia alieleza kuwa mfumo huo hauna utofauti na awali kwani utofauti utakuwepo kutokana na mashirika na taasisi kufungua akaunti BoT, ambapo lengo kubwa ni walaka wa Hazina kulenga kuboresha mapato ya serikali ammbayo yanaweza kutumiwa kwa namna mbalimbali.

“Mfumo huu…utakuwa hauna tofauti na ilivyo sasa kwa kuwa fedha zitakazokuwa zikiingizwa kwenye akaunti hizo ni zile zilizokuwa zikiingizwa kwenye benki awali, ili kupunguza kiwango cha riba,” alisema.

Pia alisema hofu nyingine inayojengeka kwa wananchi inatokana na mfumo huo kutotumiwa kwa muda mrefu na BoT, licha ya kuwa kuna baadhi ya nchi inatumia mfumo huo na hakuna madhara yoyote.

“Hivyo tunafikiri maamuzi hayo hayana athari zozote kwani nchi mbalimbali zimekuwa zikitumia mfumo huo ikiwemo Uganda, Rwanda na Kenya ila  kwetu unaonekana mgeni kutokana na kutotumika kwa muda mrefu,”alisema.

Pia Dk.Kimei alisema kuwa kutokana na uwepo wa mfumo huo,benki za kibiashara zitawakopesha zaidi sekta binafsi, ikiwa tofauti na malalamiko ya mwanzo kwamba Serikali inapata manufaa kutokana na kukopeshwa zaidi.

“Hii itasaidia hata wananchi wa kiwango cha chini kuchukua mikopo kutokana na riba kuwa ndogo, ambapo hata wananchi wa chini wataweza kuchukua mkopo, ikiwa tofauti na awali wananchi wanashindwa kuchukua mikopo kutokana na riba kuonekana kuwa juu zaidi ya asilimia 10,”alisema.

Mbali na hilo, pia Kimei alisema endapo riba ikiwa inapungua itasaidia kukuza uchumi kutokana na wananchi wengi wa hali ya chini kuchukua mikopo.

Habari Katika Magazeti ya siku ya Leo Jumanne ya Februari 2 yako hapa.


#YALIYOJIRI>>>>>Wabunge Wa Upinzani Wagoma Kuteua Wenyeviti PAC Na LAAC.Fahamu zaidi hapa.

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesema kutokana na Spika wa Bunge kuteua kibaguzi wajumbe wa kamati za kudumu za Bunge, wabunge wa upinzani hawatashiriki uchaguzi wa wenyeviti wa kamati mbili ambazo zinapaswa kuongozwa na upinzani.

Amedai kuwa katika kamati hizo za Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Mashirika ya Umma (LAAC), wameteuliwa wabunge wa upinzani ambao hawana uwezo mkubwa katika kutekeleza majukumu hayo na wamekataa kabisa kumhamisha na kumuweka Freeman Mbowe kuwa mjumbe wa kamati hizo.

Kwa mujibu wa Tundu Lissu,  ili Mbowe aweze kuwa mwenyekiti wa PAC au LAAC ni lazima awe mjumbe wake, jambo ambalo limekuwa gumu baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kukataa kumpeleka huko.

Tundu Lissu amesema Ndugai amefanya hivyo kwa madai kwamba amepokea amri kutoka mamlaka za juu  asihamishe mjumbe wa kamati zozote ambazo zimetangazwa

Amesema endapo hawataafikiana na Spika na kufanya marekebisho ya wajumbe wa kamati kama wanavyotaka, kamwe hawatakuwa tayari kuongoza kamati hizo

“Hili Bunge litakuwa la vichekesho, maana unasema kamati za usimamizi wa fedha za umma zitaongozwa na wapinzani halafu unawachagulia nani aongoze hizo kamati. Hatushiriki uchaguzi acha waendelee.”

“Kwa mujibu wa mabunge ya jumuiya za madola, kamati hizo mbili lazima ziongozwe na wabunge kutoka upinzani, hivyo majukumu ya PAC hayawezi kuhamishiwa PIC (kamati mpya ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma).”

Mara baada ya Spika kutangaza majina ya Kamati za Kudumu za Bunge, wabunge wa upinzani walipinga jinsi uteuzi huo ulivyofanyika kwa maelezo kuwa wabunge wenye weledi mkubwa walipangiwa kamati zisizojihusisha na masuala makubwa ya kitaifa.

Akizungumzia suala hilo, Naibu Katibu wa Bunge, John Joel alisema kamati hizo zinaweza kuendelea na kazi bila kuwa na wenyeviti.

“Kiutaratibu mwenyekiti wa kamati hizo mbili lazima atoke upinzani ila makamu wake hutokea CCM. Hata wasiposhiriki zitaendelea na kazi chini ya makamu mwenyekiti. Hakuna kanuni inayoeleza kuwa lazima kamati iwe na mwenyekiti. Ni kama bungeni asipokuwepo Spika, shughuli zitaendelea kufanywa na Naibu Spika,” alisema.