Thursday, 4 February 2016

#YALIYOJIRI>>>>Mahakama Ya Rufaa Kuamua Ugomvi Wa Nyumba Kati Ya Afande Suleiman Kova Na Godfrey Nzowa.Fahamu zaidi hapa.

Mahakama ya Rufaa wiki ijayo inaanza kusikiliza kesi za rufani 50 za jinai na madai katika Kanda ya Arusha ikiwamo rufaa ya makamishna wawili wa Jeshi wa Polisi wanaogombea nyumba ya serikali iliyopo Uzunguni Arusha.

Maofisa hao, Godfrey Nzowa ambaye ni Mkuu wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya katika Jeshi hilo amemshitaki mahakamani aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova akipinga kuuziwa nyumba hiyo. Kamishna Kova hata hivyo amestaafu rasmi mapema mwaka huu.

Kwa mujibu wa orodha ya kesi zitakazosikilizwa na majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa kwa mwezi mmoja mjini hapa, Nzowa anamlalamikia Kova na wenzake kupinga kuuziwa nyumba hiyo aliyokuwa akiishi alipokuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) wa Mkoa wa Arusha.

Nyumba hiyo aliuziwa Kamishna Kova akiwa ameshahama mkoani Arusha na wakati inauzwa Nzowa alikuwa akiishi katika nyumba hiyo, familia yake akiwa RCO kabla ya kuhamishiwa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuendelea na wadhifa huo, Kova akiwa bosi wake.

Orodha hiyo yenye jumla ya mashauri 50 inaonesha mahakama hiyo itasikiliza rufani ya Wakili maarufu jijini Arusha, Median Mwale ambaye amekata rufaa dhidi ya Jamhuri katika kesi yake ya kudaiwa kutakatisha fedha chafu na kujipatia mabilioni ya fedha kwa njia ya udanganyifu akiwa na wenzake watatu.

Rufani hiyo namba 395 ya mwaka 2013 ya Wakili Mwale dhidi ya Jamhuri imepangwa kusikilizwa na majaji watatu, Mbarouk Salim Mbarouk, Bernard Luanda na Semistocles Kaijage watakaosikiliza pia mashauri mengine kabla ya kutoa uamuzi Machi 5, mwaka huu.

Orodha iliyotolewa na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa, E.Y. Mkwizu inaonesha kesi nyingine yenye mvuto ni ile ya wafanyabiashara Philemon Mang’ehe na Gesso Bajuta iliyodumu kwa miaka 20 sasa.

Katika kesi hiyo, Mang’ehe wa Kampuni ya Bukine anamdai fidia ya mamilioni ya fedha Bajuta baada ya kudai kuharibiwa biashara yake ya kusambaza vifaa vya ofisi katika Mahakama ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) mwaka 1996.

0 comments:

Post a Comment