Wakati kesho CCM ikiadhimisha miaka 39 tangu kuzaliwa kwake, kada
mkongwe na muasisi wa chama hicho, Pius Msekwa amechambua uwezo na
udhaifu wake, akibainisha kuwa kimepoteza sifa ya asili ya kuwa chama
cha wanyonge.
Msekwa amesema kuwa matukio mbalimbali yanayokikumba chama hicho, ikiwamo migogoro baina ya
viongozi wake, makundi na tuhuma za ufisadi, yameathiri taswira yake kwa
jamii.
Msekwa ambaye ni katibu mkuu wa kwanza wa Tanu
na makamu mwenyekiti mstaafu (Bara), alibainisha kuwa CCM imepoteza
sifa yake ya asili ya kuwa chama kinachojali wanyonge na kubebeshwa
mzigo wa kuitwa “chama cha matajiri”.
“Migogoro miongoni mwa
viongozi, hususan baina ya makundi yanayozozana au kuhasimiana ndani ya
chama na tuhuma za ufisadi, imechangia kuifanya CCM ibebeshwe mzigo wa
kuonekana kuwa ni chama kinachokumbatia mafisadi,” alisema.
Aliongeza
kuwa CCM pia imeathiriwa na kujipenyeza kwa kasi kubwa kwa
wafanyabiashara wasio waadilifu katika baadhi ya vikao vyake vya uamuzi.
Hata hivyo, Msekwa alisema ujio wa
Rais John Magufuli umeleta matumaini mapya miongoni mwa wananchi juu ya
taswira ya chama hicho.
“Nafarijika kwamba uongozi mpya wa Rais
anayetokana na CCM, Dk John Magufuli umeleta matumaini hayo mapya
miongoni mwa wananchi walio wengi,” alisema.
Alieleza kuwa CCM
kupitia viongozi wake, haina budi kuonyesha kwamba inaweza kuleta
mabadiliko yenye tija na yenye kuleta matumaini mapya miongoni mwa
wananchi walio wengi.
Alisema ukongwe wa chama hicho kwa maana
ya kuwa kimekuwapo na kimekuwa madarakani mfululizo tangu nchi ilipopata
uhuru wake mwaka 1961, una faida na hasara zake.
“Faida ni
kwamba kwa sababu ya uzoefu wake huo wa miaka mingi, kina (CCM) fursa
kubwa ya kuendesha shughuli zake vizuri na kuendelea kupata ushindi
katika chaguzi zijazo,”alisema.
Alibainisha pia kuwa kitendo cha CCM kuwapo madarakani muda mrefu kinaweza kusababisha hatari inayotokana na hulka ya binadamu.
Alifafanua
kuwa wakati mwingine watu wanaweza kutaka mabadiliko tu ya uongozi wa
nchi hata kama chama kilichopo madarakani kinafanya vizuri kiasi gani.
“Hatari
iliyopo ni watu wanaweza kuchoka tu kuendelea kuwa chini ya uongozi wa
chama kilekile na hatari hiyo inakuwa kubwa zaidi pale matendo ya
viongozi wake yatakapokuwa mabaya kiasi cha kuwaudhi watu,”alisema.
Msekwa alisema katika kipindi hicho cha uhai wa CCM,
maadili ya viongozi yameporomoka kwa kiwango kikubwa.
Alitaja
sababu za kuporomoka kwa maadili kuwa ni pamoja na kuingia katika mfumo
wa vyama vingi vya siasa nchini na ushindani mkali wa kuwania kushika
dola uliojikita katika mfumo huo.
Alisema hali hiyo pia
inatokana na hatua ya kusitishwa kwa mafunzo ya viongozi, makada na
watendaji wa chama hicho yaliyokuwa yakitolewa kwenye vyuo mbalimbali.
“Hatua
hiyo ilichukuliwa kutokana na kusitishwa kwa ruzuku iliyokuwa inatolewa
na Serikali kwa chama kwa ajili ya kuendesha mafunzo hayo, katika vyuo
vya chama vya Kivukoni na vyuo vyake sita vya kanda vilivyokuwa mikoa
mbalimbali,” alisema.
Alisema kutokuwapo kwa msaada wa mafunzo
ya maadili na uadilifu kwa viongozi, pia kulichangia kuporomosha maadili
ndani ya chama.
“Hapo ilibidi kila kiongozi alazimike kutumia
akili zake tu katika shughuli zake za uongozi. Kama wasemavyo Waswahili;
akili ni nywele, kila mtu ana zake,” alisema.
Alieleza pia kuwa ushindani katika mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini, umesababisha kukithiri rushwa katika uchaguzi.
Alisema
hili hujitokeza wakati wa kura za maoni ndani ya CCM ambako baadhi ya
makada wake wameanza tabia ya kuwashawishi wapigakura kwa rushwa ili
wachaguliwe katika nafasi wanazozitafuta.
Alisema yapo mambo
muhimu ya kuzingatia, wakati wa kutafakari chama hicho kilikotoka na
kwamba katika kipindi chote hicho kimekuwa kikipata ushindi unaopanda na
kushuka katika chaguzi zote zilizofanyika chini ya mfumo wa vyama vingi
vya siasa.
0 comments:
Post a Comment