Thursday, 4 February 2016

#YALIYOJIRI>>>Serikali Yalaani Kitendo Cha Kudhalilishwa Kwa Mtanzania Nchini India.Fahamu zaidi hapa.

Serikali ya Tanzania imesikitishwa na inalaani vikali kitendo cha udhalilishwaji alichofanyiwa mwanafunzi wa kike wa Kitanzania na Kundi la watu katika jimbo la Bangalore nchini India.

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Ramadhani Muombwa Mwinyi alipokutana na Wandishi wa Habari kwa ajili ya kuwaeleza hatua zilizochukuliwa na Serikali kufuatia kitendo hicho cha kudhalilishwa kwa mwanafunzi wa Kitanzania nchini India.
 
Balozi Mwinyi alisema kuwa, hatua zilizochukuliwa ni pamoja na Ubalozi wa Tanzania nchini India kuiandikia Serikali ya nchi hiyo kuomba maelezo kamili kuhusu tukio hilo pamoja na kuitaka Serikali ya India kuwachukulia hatua za kisheria watu wote waliohusika pamoja na kuimarisha usalama katika maeneo wanayoishi wanafunzi wa Kitanzania. 
 
Aidha, Balozi Mwinyi alieleza kuwa amemwita Balozi wa India hapa nchini, Mhe. Sandeep Arya na kumweleza masikitiko ya Serikali ya Tanzania kufuatia kitendo hicho cha kushambuliwa na kudhalilishwa kwa mwanafunzi wa kike kutoka Tanzania.
 
Katika mazungumzo yao, Balozi Arya alieleza bayana kuwa Serikali ya India imesikitishwa na tukio hilo la udhalilishaji na kwamba Serikali imeahidi kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainika kutekeleza uovu huo.
 
Alisema kuwa Waziri Mkuu wa Jimbo la Bangalore aliongea na umma kuelezea masikitiko yake kuhusu uovu huo na kuahidi kuwa mamlaka za jimbo hilo zitaimarisha usalama katika maeneo yote wanayoishi wanafunzi wa Tanzania na raia wengine kutoka nje.
 
Balozi Arya aliihakikishia Serikali ya Tanzania kuwa India inaheshimu ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na nchi yake, hivyo itashughulikia suala hilo kwa ukamilifu na hadi wakati huu tayari watu watano wanashikiliwa na vyombo vya usalama wakituhumiwa kuhusika na tukio hilo.

Sanjari na taarifa hiyo, Balozi Mwinyi aliwaomba Watanzania kutohusisha tukio hili la uhalifu na ajali ya Mtanzania, Bw. Christian Benjamin Mlyansi iliyotokea nchini India jana usiku na kusababisha kifo chake.

Alisema kuwa Bw. Mlyansi alipata ajali ya kawaida alipokuwa anaendesha pikipiki ambapo ilipoteza mwelekeo na kugonga ukingo wa kati wa barabara.

0 comments:

Post a Comment