Vyama
vitano vya siasa vitashiriki katika uchaguzi wa marudio wa Zanzibar,
utakaofanyika Machi 20 mwaka huu, uliotangazwa na Tume ya Uchaguzi
Zanzibar (ZEC). Vyama hivyo ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), ADC, CCK, TLP
na SAU.
Hatua
hiyo inatokana na vyama vitatu vya siasa Zanzibar vya CCK, SAU na TLP,
kutangaza kuwa wagombea wake, watashiriki katika uchaguzi huo wa Machi
20. Taarifa ya viongozi wa vyama vya CCK, SAU na TLP, iliyosomwa kwa
pamoja katika Ukumbi wa Culture eneo la Mji Mkongwe jana, ilisema
wagombea wa vyama hivyo vitatu, watashiriki uchaguzi huo.
Taarifa
hiyo ilieleza kuwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, ulifutwa
baada ya kujitokeza kwa kasoro mbalimbali, zilizoonesha wazi kwamba
hauwezi tena kuwa huru na haki.
Wagombea
wa vyama hivyo vya siasa, waliotangaza kushiriki katika uchaguzi huo ni
Ali Khatib kutoka CCK, Issa Mohamed Zonga kutoka SAU na Hafidh Hassan
Simai kutoka TLP.
Mgombea
wa CCK, Ali Khatib Ali alisema kwamba tayari wamejipanga vizuri kwa
ajili ya uchaguzi huo na kuwataka wanachama na wafuasi wake na wananchi,
kuitumia fursa hiyo ya kidemokrasia kuchagua viongozi watakaoongoza
nchi.
“Tangazo
la Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) limetutaka kurudia uchaguzi kwa
sababu ule wa awali umefutwa kwa hivyo hatuna sababu ya kususia uchaguzi
huo na tunachofanya kwa sasa ni kuwataka wanachama wetu na wafuasi
kujitayarisha kwa uchaguzi wa marudio,” alisema Ali.
Jumapili
iliyopita, Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein
alisema chama hicho kipo tayari kwa uchaguzi wa marudio Machi 20 kwa
lengo la kuhakikisha kinashika dola.
Akihutubia
mamia ya wanachama wao katika viwanja vya Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui
wakati wa kuzindua maadhimisho ya miaka 39 ya CCM, Dk Shein alisema
maamuzi ya kurudiwa kwa Uchaguzi Mkuu, yamefanywa na ZEC ambayo ndiyo
chombo halali kwa mujibu wa Katiba cha kushughulikia masuala yote ya
uchaguzi nchini.
Aliwataka
wanachama na wafuasi wao kujipanga vizuri na kushiriki uchaguzi huo
kikamilifu, kwani kwa mujibu wa Katiba ya CCM ni kushinda chaguzi zote
zinazofanyika nchini ili kushika dola na kuwatumikia wananchi.
“Hayo
ndiyo maamuzi ya chama chetu tuliyokubaliana kushiriki Uchaguzi Mkuu wa
marudio baada ya kufutwa kwa ule wa Oktoba 25 mwaka jana kwa hivyo
wanachama na wafuasi jitayarisheni kushiriki kikamilifu kwa ajili ya
kushika dola,” alisema Dk Shein.
0 comments:
Post a Comment