Sakata
la ununuzi wa mabehewa kwa ajili ya Shirika la Reli Tanzania (TRL)
yanayodaiwa kuwa mabovu liliibuka jana Bungeni na kumuinua Waziri wa
Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe ambaye alikuwa Waziri wa
Uchukuzi katika serikali ya awamu ya nne.
Waziri
Mwakyembe alikanusha madai yaliyotolewa na Mbunge wa Viti Maalum
(Chadema), Jesca Kishoa kuwa ununuzi huo wa mabehewa mabovu
uliisababishia sherikali hasara ya shilingi bilioni 238, huku akitaka
ripoti ya ukaguzi wa ununuzi huo iwasilishwe bungeni.
Akitumia
kanuni ya 63 (3) kuomba kutoa taarifa, Mwakyembe alikanusha kiwango cha
fedha kilichotajwa na mbunge huyo wa viti maalum ambaye ni mke wa
aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila.
“Mbunge
aliyesimama kabla, aliyejitambulisha kama mke wa Kafulila, ameeleza
kwamba serikali ilitumia zaidi ya shilingi bilioni 238 na kuleta hasara
kwa kununua mabehewa mabovu. Mheshimiwa Mwenyekiti nataka
kukuthibitishia kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kwa kununua
mabehewa 274 haijawahi kutumia zaidi ya shilingi bilioni 60,” alisema Mwakyembe.
Waziri
huyo alienda mbali na kueleza kuwa endapo mbunge huyo atawasilisha
uthibitisho wa kiwango hicho cha fedha kutumika kununua mabehewa hayo,
atajiuzulu nafasi yake ya ubunge.
“Mimi
naomba athibitishe hiyo shilingi bilioni 238. Na nitashukuru sana kama
akileta hapa. Na akileta hiyo, mimi nitajiuzulu hata ubunge,” alisema Mwakyembe.
Baada
ya kauli hiyo ya Mwakyembe, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee naye alisimama
na kueleza kuwa Waziri huyo hakutumia kifungu sahihi kutoa taarifa kwa
kuwa alipaswa kutumia kifungu cha 63 (4) kutoa ushahidi wa kukanusha
kwake kwanza.
Naye
Kishoa aliendelea kusisitiza kuwa Serikali inapaswa kuwasilisha bungeni
hapo ripoti ya ukaguzi wa manunuzi ya mabehewa hayo.
Hata
hivyo, Mwenyekiti wa Bunge, Dk. Mary Mwanjelwa alitoa siku tatu kwa
mbunge huyo wa viti maalum kuwasilisha ushahidi kuhusu madai yake.
0 comments:
Post a Comment