Tuesday, 31 May 2016

#YALIYOJIRI>>>Mabadiliko Ya Tarehe Ya Kuripoti Katika Makambi Ya Jkt Kwa Vijana Wa Form Six Waliochaguliwa Kujiunga Na Mafunzo Ya JKT.Fahamu zaidi hapa.

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) linautangazia umma mabadiliko ya tarehe ya kuripoti makambini vijana wote waliohitimu kidato cha sita mwaka 2016 na kuchaguliwa kujiunga na mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria kwa mwaka 2016.

Taarifa ya awali kwa vyombo vya habari nchini ilianisha tarehe ya kuripoti kuwa ni tarehe 01 June hadi tarehe 05 Juni 2016. 

Tarehe hiyo imeafanyiwa mabadiliko badala yake vijana hao wanatakiwa kuripoti katika makambi ya JKT waliyopangiwa kuanzia tarehe 07 June hadi tarehe 10 June 2016 bila kukosa.

Atakayesikia tangazo hili amtaarifu na mwezie.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Habari na Uhusiano
Makao Makuu ya JKT
Tarehe 31 Mei 2016

#MICHEZO>>>CAF YARUDISHA HATUA YA MTOANO MICHUANO YA KLABU.Fahamu zaidi hapa.

Shirikisho la Soka Afrika limetaja mfumo mpya wa mashindano kuanzia mwakani, na sasa limerudisha mfumo wa mechi za mtoano kuanzia hatua ya Robo Fainali.

Katika kikao cha Jumanne ya Mei 24, mwaka 2016 mjini Cairo, Misri; Kamati ya Mashindano ya Klabu ya CAF ilikubaliana juu ya mfumo mpya wa Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho. Mabadiliko katika mashindano hayo mawili yalitangazwa na Rais wa CAF, Issa Hayatou katika Mkutano Mkuu wa 38 wa shirikisho hilo uliofanyika mjini Mexico City, kwamba kuanzia mwakani kutakuwan na timu 16.

#YALIYOJIRI>>>Rais Magufuli Ashiriki Katika Hafla Ya Utoaji Wa Tuzo Za Rais Kwa Wazalishaji Bora Wa Viwanda Kwa Mwaka 2015.i.Fahamu zaidi hapa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wadau mbalimbali wa CTI na kutoka Sekta ya Viwanda nchini kabla ya kutoa Tuzo za Rais kwa viwanda vilivyofanya vizuri kwa mwaka 2015 katika Ukumbi wa Serena Jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizindua nembo mpya ya Tuzo za Rais kwa Wazalishaji bora wa Viwanda  PMAYA The President’s Manufacure of the Year  pamoja na Mwenyekiti wa Wenyeviwanda Tanzania CTI Dkt. Samwel Nyantahe katika Ukumbi wa Serena Jijini Dar es Salaam.

#MICHEZO>>>MAJIBU YA AZAM FC KUHUSU KIPRE TCHETCHE KUTIMKIA UARABUNI.Fahamu zaidi hapa.

Mtendaji Mkuu wa klabu ya Azam FC Saad Kawemba amekanusha taarifa za nyota wao Kipre Tchetche kusaini kwenye klabu moja ya nchi za falme za Kiarabu lakini akasema, wapo tayari kuzungumza na klabu yeyote ambayo inahitaji huduma ya mchezaji huyo.

“Taarifa hizo tumeziona na kwa maana ya wakati usajili hivyo ni vitu vya kawaida kwenye mpira, unasikiliza halafu unasubiri matokeo yake. Kwasasababu sisi ni klabu na nimeona kwenye mtandao mmoja amesema anamkataba na klabu na ni kweli bado tunamkataba naye wa mwaka mmoja”, amesema Saad Kawemba mtendaji mkuu wa klabu bya Azam FC alipohojiwa na Sports Extra ya Clouds FM.

“Kwahiyo tunaamini yeyote ambaye anamuhitaji atafika kwenye klabu yetu tuzungumze. Lakini katika kipindi hiki cha usajili tunategemea mambo kama hayo kutokea kwa wachezaji wengi na si yeye pekeyake.”

Jana pia zilitoka taarifa zinazomhusu raia huyo wa Ivory Coast kutakiwa na mabingwa VPL na FA Cup Dar Young Africans.

Alikiba Akanusha Kumuimbia Jokate Wimbo ‘Aje’.Fahamu zaidi hapa.

Alikiba amesema Aje si wimbo aliomuimbia Jokate wala msichana yeyote bali aliimba kwaajili ya mashabiki wake.
“Sijamuimbia mtu yeyote kwa kweli, mi nimeimba kwa ajili ya mashabiki wangu, kwanza sijawahi kumuimbia mtu kabisa, sijawahi, so ni kwa ajili ya mashabiki wangu,” Kiba alikiambia kipindi cha Friday Night Live cha EATV.

Hata hivyo Kiba alikiri kuwa kumtaja Wema kwenye wimbo huo kimekuwa ni kitu cha surprise kwa mrembo huyo.

Aje ni miongoni mwa nyimbo zinazofanya vizuri kwa sasa si tu Tanzania, bali sehemu nyingi za Afrika.

Bongo5

#MICHEZO>>>>MIAKA 16, MABADILIKO 16 YA MAKOCHA, MILOVAN ANAREJEA SIMBA KUFANYA NINI?.Fahamu zaidi hapa.

Na Baraka Mbolembole

SIMBA SC ipo katika hatua za mwisho kumsaini mkufunzi, Milovan Curkovic ambaye aliifundisha timu hiyo kwa vipindi viwili (lakini si zaidi ya miaka miwili.) Kwa mara ya kwanza, Mserbia huyo alijiunga na Simba kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa ligi kuu Tanzania Bara msimu wa 2007/08.

Milovan alishuhudia timu hiyo ikimaliza katika nafasi ya tatu nyuma ya Yanga SC waliotwaa taji na Tanzania Prisons ilimaliza katika nafasi ya pili.

Baada ya kurejea nyumbani kwao Serbia kwa mapumziko, Milovan aliyekuwa na mkataba wa muda mfupi hakurejea tena kuinoa timu hiyo licha ya kwamba tayari mkataba mpya ulikuwa umeandaliwa na uongozi wa Mzee Hassan Dalali.

Siasa za Simba na Yanga zilitajwa kama sababu ya mwalimu huyo kutorejea huku Mserbia mwenzake, Dusan Kondic aliyekuwa kocha wa Yanga akitajwa kama ‘mshawishi aliyemkataza’ Milovan kurejea kuinoa timu iliyokuwa na ‘msuguano wa viongozi’.

Dalali na aliyekuwa katibu wake Mwina Kaduguda walikuwa na tofauti za mara kwa mara ambazo ziliwafa, Neidor Dos Santos na Nelson Elias raia wa Brazil kushindwa kufanya nao kazi.

Milovan si kocha mbaya, lakini anarudi Simba kufanya nini? Anapenda kufundisha mpira wa chini na wa kupasiana. Simba wanatamaduni ya kiuchezaji ambayo makocha watatu tu kati ya 16 waliopita ndani ya miaka 16 hii waliimudu kiasi cha kupendwa sana mashabiki.

Mkenya, James Siang’a alikuwa na miaka minne ya kupendeza sana kati ya mwaka 2000 hadi 2004. Vipindi viwili tofauti vya Mzambia, Patrick Phiri viliambatana na mchezo wa kuvutia kwa ‘Wekundu wa Msimbazi’ na Milovan anakumbukwa kwa msimu wa 2011/12 ambao Simba ilitwaa taji lake la mwisho la ligi kuu huku pia wakiwachapa 5-0 mahasimu wao Yanga (kipigo cha kihistoria katika karne mpya.)

Lakini yatakuwa ni makosa kumrejesha Milovan kwa maana mwalimu huyo si mtu makini wa kusimamia nidhamu katika timu.

Rejea sehemu ya MAKALA HAYA ambayo niliyaandika Novemba, 2012 baada ya Simba kushindwa kupata ushindi dhidi ya Polisi Moro FC na Mtibwa Sugar. Makala haya yalitumika na uongozi wa Ismail Aden Rage kumuondoa mwalimu huyo ambaye alirejea kwa mara ya pili klabuni hapo Novemba, 2011 kuchukua nafasi ya Mganda, Moses Basena.

Tuesday, November 6, 2012 
SIKU SITA ZA SIMBA MORO NA POINTI YAO MOJA: NA KOCHA MILOVAN
Simba ilifikia katika, Hotel ya Usambara, ambayo humilikiwa na Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Mzee Yusuph Makamba. Kuna wachezaji waliolala katika vyumba vya gharama ya 20,000 na wapo waliolala katika vile vya gharama ya 25, 000.

Kocha Milovan Curkovic, yeye aliandaliwa chumba cha gharama ya 50, 000. Vikaanza vioja. Kocha akakataa kufikia Hotel isiyo na huduma ya Internet. Viongozi kwa kushirikiana na Meneja wa Hotel hiyo wakamtafutia Kompyuta yenye huduma ya Internet, lakini, Milovan, akakataa na kusema kwa kiswahili kizuri.

“Nataka yenye wireless” viongozi wachache tena wa ngazi ya chini, wakashindwa na kuingia katika mtego wa Milovan, ambaye tangu awali alionesha kutotaka kukaa katika Hotel ile. Kocha wa makipa wa timu hiyo akasema.

“Hana lolote, hakuna cha Internet wala nini anataka Mwanamke tu huyo kocha hamna kitu na sasa anaongea hadi Kiswahili…”, alikuwa akiongea mbele ya wachezaji wachache.

Milovan, akahamishiwa katika hotel yenye hadhi zaidi na gharama ya chumba ni zaidi ya 60, 000. Hakwenda pamoja na timu akitokea hotelini. Simba walitoka zao kivyao kutokea, Usambara, Milovan, akatokea ARC Hotel. Wakapata pointi moja mbele ya Polisi Moro.
…………………..
Milovan anarudi tena Simba akiwa na mafanikio gani kiufundishaji tangu alipoondoka Desemba, 2012? Alipoondolewa alimsema sana Geofrey Nyange ‘Kaburu’ kwamba ni ‘kiongozi anayependa kuingilia majukumu ya kocha katika upangaji wa timu.’

Je, ataweza kufanya kazi na Zacharia Hans Poppe? Ni kujidanganya wenyewe, kuamini Milovan anaweza kuirejesha juu Simba. Ndani ya wachezaji wenyewe timu imekosa kiongozi, ndani ya uongozi kuna utofauti mkubwa. Milovan anaweza kufanya kazi hivi sasa na Kaburu kwa maana kwa mwaka sasa amejiondoa katika ‘mtindo wake wa kuingilia majukumu ya kiufundi’.

Lakini mtu tishio zaidi kwake ni Poppe na Milovan mwenyewe ni mtu wa kuzurura hovyo na kujijali binafsi kuliko nidhamu yake mbele ya wachezaji, na kuheshimiana kati ya wachezaji kwa wachezaji.
Simba ingeongeza nguvu kumpata Mscotland, Bobby Williamsons na kuachana na makocha wa dola 6000. Bobby ni ghali lakini Simba imekuwa ikimtamani. Amerejesha nidhamu na uwajibikaji katika timu ya Taifa ya Kenya na aliweza kufanikiwa zaidi katika hilo katika miaka yake mitano akiwa kocha wa timu ya Taifa ya Uganda.

Kocha mwingine mzuri ambaye labda Simba inapaswa kumtazama kwa ‘macho-maangavu’ ni Mserbia, Goran Kopunovic ambaye Januari hadi June, 2015 alikuwa kocha wa mpito klabuni hapo. Goran alisimamia vizuri nidhamu yake, na jambo hilo likasambaa kwa wachezaji lakini alitaka kulipwa si chini ya milion 26 kwa mwezi ili asaini mkataba mpya.

Kazi yake katika mzunguko wa pili wa ligi kuu msimu wa 2014/15 ilikuwa nzuri sana kwani si tu aliweza kushinda kikombe cha Mapinduzi Cup, bali akiwatumia wachezaji wengi vijana Simba ilikuwa ikiweka mpira chini. Alishinda dhidi ya Yanga na Azam FC na kazi yake haina shaka, aliweza kuijenga ‘timu iliyokuwa goigoi’ na kuipa nguvu ya kupigania ‘TOP2.’

Sababu za kimaslai ziliwafanya Simba kushindwa kuendelea kuwa naye. Alikuwa na thamani ya zaidi ya waliyotaka kumpa Simba.

Alipoondolewa Mcroatia, Z.Logarusic na nafasi yake kuchukuliwa na Mzambia, Patrick Phiri, Agosti, 2014 niliuliza, Phiri amerejeshwa kwa mafanikio gani aliyopata tangu alipoondoka Simba mwaka 2011? Nilisema sababu zilizile zilizomuondoa 2005 na 2011 kama zisingerekebishwa ndizo zingemuondoa kwa mara ya tatu ‘bila kuaga.’

Phiri hakupenda kupangiwa timu yake na viongozi wa klabu, na mara zote alizorejeshwa aliahidiwa kutokuwapo tena kwa kadhia hiyo. Ila alidanganywa kwa maana Poppe baada ya sare ya 1-1 dhidi ya Prisons katika uwanja wa Sokoine alisikika akiponda mbinu za Phiri katika moja ya vituo vikubwa vya radio nchini, pia bila hofu alisema namna alivyotaka yeye kuona Simba ikicheza.

Milovan amekuwa akiitaka sana Simba, kwa kuwa anapendwa na mashabiki, pia aliipa taji la mwisho la VPL lilioambatana na kuwachapa 5-0 ‘Watani wao wa Jadi’ katika game ya kufunga msimu. Lakini, je, nani amejibadilisha na kupiga hatua mbele za kiutendaji kati ya watendji wa klabu na Milovan? Yetu macho, tusubiri na tuone.

Tangu 2000 hadi sasa
Mkenya, James Siang’a (2000-2004-Nilimuelewa sana Tu)
Trott Moloto-Sauz (2005-Sikumuelewa)
Patrick Phiri- Zambia (2005)
Neidor dos Santos-Brazil (2006 aliwapa nafasi yosso)
Nelson Elias-Brazil (2006 Siku kadhaa)
Talib Hilal & Julio (2007)
Milovan Curkovic-Serbia (Nov.2007-April 2008)
Patrick Phiri-Zambia (2009-2011)
Moses Basena-Uganda (June 2011-Novemba)
Milovan Curkovic-Serbia (Novemba 2011-Novemba 2012)
Patrick Liewig-Ufaransa (Desemba 2012-Mei 2013)
Abdallah ‘King’ Kibadeni (June 2013-Novemba)
Z.Logarusic-Croatia (Desemba 2013-June 2014)
Patrick Phiri (Agosti 2014-Novemba 2014)
Goran Kopunovic-Serbia (Disemba 2014 -June 2015)
Dylan Kerr-Malta (Julai 2015- 2016 Januari)
Jackson Mayanja (Januari 2016 –Mei)

#YALIYOJIRI>>>Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) Profesa Tunus Mgaya Aliyesimamishwa Kazi na Waziri wa Elimu Afunguka Mambo Mazito.Fahamu zaidi hapa.

ALIYEKUWA Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), Profesa Tunus Mgaya amesema amesikitishwa na taarifa zilizoandikwa katika vyombo vya habari za kukosoa maamuzi ya serikali ya kuwasimamisha kazi kuwa hayakuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa.

Mgaya ambaye hakuwa tayari kueleza kama taratibu za kusimamishwa kwao zilifuata utaratibu au la, amewataka waandishi wa habari kuwa na vyanzo vya uhakika katika habari zao.

“Mimi nikiwa miongoni mwa watendaji waliopumzishwa kazi, napenda kueleza kuwa sihusiki na taarifa hizo, suala hili limeshapita na kutolewa uamuzi na serikali na tuiache Tume iendelee kufanya kazi,” alisema Profesa Mgaya alipozungumza na waandishi wa habari jana mara baada ya kukabidhi ofisi.

Aidha, Profesa Mgaya aliweka wazi kuwa, anaunga mkono jitihada za Rais John Magufuli katika kuhakikisha kuwa watanzania wengi zaidi wanapata elimu ya msingi bure na kutolewa kwa elimu inayokidhi viwango stahiki kitaifa na kimataifa na kusema jambo hilo ni jema na linapaswa kuungwa mkono kwa nguvu zote.

Katika hatua nyingine, alimtaka Waziri wa Elimu, Sayansi,Teknolojia na Ufundi , Profesa Joyce Ndalichako kuendeleza jitihada za kuinua ubora wa elimu katika ngazi zote ili kuwa na taifa lenye watu walioelimika vizuri na lenye mchango mkubwa katika kuendeleza taifa.

Breaking News>>>Bunge Lawasimamisha Wabunge 7 Kwa Kufanya Vurugu Bungeni.Fahamu zaidi hapa.

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge limepitisha azimio la  kuwasimamisha kuhudhuria vikao vya Bunge baadhi ya wabunge wa Kambi ya Upinzani waliohusika katika kufanya vitendo vya vurugu ndani ya ukumbi na kudharau Mamlaka ya Spika Januari, 27, 2016.

Wabunge waliosimamishwa kuhudhuria vikao hivyo ni Mhe.Kabwe Zubeiri Ruyangwa Kabwe, Mhe.John Heche, Mhe.Halima Mdee,Mhe.Tundu Lissu, Mhe.Halima Mdee, Mhe.Pauline Gekul  na Mhe. Ester Bulaya.
 
 Azimio la adhabu kwa wabunge hao limetolewa na Bunge chini ya Kifungu cha 30A (1) cha sheria ya Haki Kinga na Madaraka ya Bunge Sura ya 296 na kanuni ya 74 (4) na (6).

Akisoma adhabu hizo Mwenyekiti wa kamati hiyo yenye wajumbe 15 Mhe.George Huruma Mkuchika amesema kuwa uchunguzi uliofanywa na Kamati hiyo kwa kuwaita na kuwahoji wahusika ulibaini kuwa wabunge hao walitenda kosa kwa kukiuka kanuni zinazoliongoza bunge hilo.
 
 Imebainishwa kuwa Mhe.Zitto Kabwe alivunja masharti ya Kifungu cha 24(c), (d) na (e) cha Sheria ya Haki na Kinga na Madaraka ya Bunge Sura ya 296 na Kanuni ya 60(2) na (12) , 74(1) na (b) kwa kusimama na kuzungumza bila kufuata utaratibu na kudharau mamlaka ya Spika.

Kamati hiyo ilibaini kuwa Mhe.Godbless Lema, Mbunge wa Arusha alivunja Masharti ya kifungu cha 24 (c),(d) na (e) cha Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge Sura ya 296 pamoja na Kanuni ya 74(1) (a) na (b) ya kanun hiyo Kudharau Mamlaka ya Spika.

Kwa upande wa Mhe.John Heche alivunja kanuni ya 72 (1) na 68(10) ya kanuni za Bunge kwa kuendelea kusimama na kuomba mwongozo kwa jambo ambalo limekwishatolewa mwongozo na kuongeza kuwa vitendo hivyo vilivuruga shughuli za Bunge.

Kwa mujibu wa maelezo ya kamati hiyo Mhe.Halima Mdee, Mhe.Tundu Lissu,Mhe Pauline Gekul  na Mhe.Ester Bulaya walivunja masharti ya kifungu cha 24 (c), (d) na (e) cha sheria ya Haki,Kinga na Madaraka ya Bunge Sura ya 296 na Kanuni ya 72 (1)68 (10), 60(2) na 12 na 74(1) (a) na (b) kwa kusimama na kuendelea kuomba mwongozo kwa jambo ambalo limekwishatolewa uamuzi, kuzungumza bila kufuata utaratibu na kudharau Mamlaka ya Spika.

Kufuatia uchunguzi huo Bunge kupitia kamati hiyo limeazimia kuwa Mhe. Ester Bulaya na Mhe.Tundu Lisu wasihudhurie vikao vyote vya mkutano wa tatu wa Bunge la Kumi na Moja vilivyobaki kuanzia tarehe 30 Mei , 2016 pamoja na vikao vyote vya Mkutano wa Nne wa Bunge la Kumi na Moja kwa kuwa walipatikana na makosa ya ukiukwaji wa Kanuni na kuonyesha dharau kubwa kwa mamlaka ya Spika.

Aidha, Bunge limeazimia kuwa Mhe. Pauline Gekul, Mhe.Godbless Lema, Mhe.Zitto Kabwe na Mhe Halima Mdee wasihudhurie vikao vyote vya mkutano wa tatu wa Bunge kuanzia tarehe 30 Mei 2016.

Aidha  Bunge limeazimia Mhe.John Heche asihudhurie vikao kumi mfululizo vya Mkutano wa Tatu wa Bunge hilo kuanzia Mei, 30, 2016 kwa kuwa alipatikana na kosa moja na pia kwa kuwa alitoa ushirikiano kwa kamati kwa kufika na kujibu maswali yote kama alivyoulizwa pamoja na kuheshimu vikao vya kamati na Mwenyekiti aliyeongoza vikao hivyo.

Pamoja na adhabu hizo Kamati hiyo imetoa maoni na mapendekezo kuwa Bunge liandae mafunzo ya kutosha kwa wabunge wote kuhusu matumizi ya uzingatiaji sahihi wa kanuni sahihi wa kanuni za Kudumu za Bunge hasa kanuni za majadiliano ndani ya Bungeni.

Aidha, Kamati hiyo imesema kuwa ipo haja ya kutungwa kwa kanuni za maadili kwa wabunge wote kama kifungu cha 12 A Cha Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge kinavyoelekeza ili kuweza kudhibiti nidhamu kwa wabunge kwa kuhakikisha heshima na hadhi ya Bunge inadumishwa.

Kwa upande wao baadhi ya wabunge wakichangia kwa nyakati tofauti kuhusu suala hilo wamesema kuwa ipo haja ya Bunge kurudisha heshima yake kwa wabunge wote kuheshimiana na kutoa michango yenye staha kwa kuzingatia nafasi walizonazo katika jamii.

Wamesema kuwa michango wanayoitoa ndani ya Bunge hilo lazima ijikite katika masuala yanayowahusu wananchi wanaowawakilisha badala ya mambo yanayochochea vurugu na kulifanya Bunge lipoteze heshima yake katika jamii.

Aidha, wabunge hao wamekubali kwa kauli moja kuanza upya kuzingatia kanuni zinazoendesha vikao vya Bunge huku wakimtaka Spika wa Bunge au Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kutosita kuchukua hatua za haraka kwa mbunge yeyote atakayekiuka utaratibu na kanuni zilizowekwa.

#Breaking News>>>Wabunge wa Upinzani wametoka nje ya bunge kuonyesha kutokuwa na imani na Naibu Spika Tulia Ackson.Fahamu zaidi hapa.

Wabunge wa vyama vya upinzani leo wametoka nje kwa mara nyingine kupinga Naibu Spika Dk. Tulia Ackson kuendesha vikao vya Bunge na kumwachia Bunge yeye na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Taarifa kutoka Bungeni zinaeleza kuwa, wabunge wote wa upinzani wametoka nje kususia kikao cha Bunge ikiwa ni kutekeleza azimio lao la kutokuwa na imani na Dk Tulia.

Baada tu ya kusomwa dua ya kufungua Bunge asubuhi wabunge hao wametoka nje na kumwacha Dk. Tulia akiwa na wabunge wa CCM pekee.

Hata hivyo Dk. Tulia ameanza kupaniwa na wapinzani tangu jana. Ni kwa madai kuwa wapinzani hawamwamini tena.

Wameeleza kuwa, namna anavyoliongoza Bunge, kauli zake na kuyumba kwake katika kusimamia haki kwa wabunge wa Ukawa na wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumechochea kuonekana kuwa, nafasi aliyonayo haimstahili.

Kutokana na hali hiyo, Freeman Mbowe ambaye ni Kiongozi Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni jana aliahidi kuanzisha mgomo dhidi ya Dk. Tulia.

Mbowe aliwaambia hayo wabunge wenzake mjini Dodoma kwenye kikao cha dharura alichoitisha na kushirikisha waandishi wa habari.

Alisema, Dk. Tulia ndio tatizo kuu la Bunge la Kumi na Moja na kwamba, kiongozi huyo wa Bunge kila anapokuwa kwenye kiti na kuongoza Bunge, mtafaruku hutokea.

“Nitapendekeza kuwa kila kikao cha Bunge kinachoongozwa na Tulia Ackson, sote tutoke nje ili kuonesha kwamba hatuna imani naye katika kuendesha shuguli za bunge,” Mbowe alisema jana.

Utekelezwaji wa kauli ya Mbowe umeanza leo ambapo sasa Dk. Tulia amebaki na wabunge wa CCM pekee.

#YALIYOJIRI>>>>Mke wa Trafiki Kinyogori Adaiwa Kukiri Kumuua Mumewe.Fahamu zaidi hapa.

MKE wa askari polisi wa kikosi cha usalama barabarani (trafiki), Sajenti Ally Salum (Kinyogori) aliyeuawa hivi karibuni, inadaiwa amekiri kuhusika kwenye mauaji hayo, akidai ilitokana na mumewe kumuacha na kuoa mke mwingine.

Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa mwanamke huyo anashikiliwa na polisi kwa mauaji hayo yaliyofanyika nyumbani kwa Kinyogori, Mkuranga mkoani Pwani.

Wakati huo huo, Kamanda Sirro amezungumzia pia mauaji ya Anathe Msuya yaliyofanyika hivi karibuni Kigamboni na kusema polisi inaendelea kumtafuta msichana wa kazi za nyumbani aliyetoroka siku moja kabla ya kifo cha mwanamke huyo.

Anayetuhumiwa kuua mumewe 
Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu matukio mbalimbali ya uhalifu yaliyojitokeza jijini Dar es Salaam, Sirro alisema katika mahojiano ya awali mke wa Kinyogori amekiri kuhusika.

Kwa mujibu wa kamanda, mwanamke huyo ambaye hata hivyo hakutaja jina lake kwa sababu za kipelelezi, aliamua kumtuma mtu kutekeleza mauaji hayo baada ya mumewe kumwacha na kuoa mke mwingine.

“Ni jambo la kusikitisha kuona mtu anatoa uhai wa mtu sababu ya kuachwa. Tunawasihi wananchi kuepuka kujihusisha na matukio kama haya, eti sababu tu ya kuachwa wanawake wapo wengi na wanaume wapo wengi unaweza kuachwa na ukaolewa na ukaoa kuliko kuondoa uhai wa mtu,” alisisitiza Sirro.

Hata hivyo, Sirro alisema wanaendelea kuwahoji watuhumiwa hao ili waweze kuwataja watu wengine walioshirikiana nao kutekeleza tukio hilo baada ya kuonekana kuwepo kwa wahusika wengine.

‘Hausigeli’ asakwa 
Kuhusu mauaji ya Anathe aliyechinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, Kamanda Sirro alisema wanaendelea na jitihada za kumtafuta msichana huyo ahojiwe kuhusu tukio hilo.

Aidha alisema mtu mmoja anashikiliwa akituhumiwa kuhusika na tukio hilo huku polisi ikiwa imeandaa timu ya upelelezi itakayoshughulikia tukio hilo kufanikisha kuwakamata wote waliohusika na tukio hilo.

Sirro alisema msichana huyo aliondoka siku moja kabla ya tukio hilo la mauaji hivyo kupatikana kwake, kunaweza kusaidia polisi kujua kama kuondoka kwake kulikuwa salama au kuna kitu kimejificha.

“Msichana huyu tunaendelea kumsaka tujue kama aliondoka salama na kumhoji zaidi juu ya kuondoka kwake siku moja tu, tukio linatokea nina imani tutafanikiwa kumpata na wote waliohusika na kukomesha matukio haya,” alisema Sirro.

Mamia wajitokeza msibani 
Vilio na simanzi jana vilitawala wakati mamia ya wakazi wa Kibada Kigamboni na Salasala walipokuwa wakiuaga mwili wa marehemu Anathe Msuya (30), aliyeuawa Mei 25 nyumbani kwake kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana.

Mwili ulichukuliwa jana asubuhi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili na kupelekwa nyumbani kwake Kibada, kwa ajili ya kuagwa na majirani zake kabla ya kusafirishwa kwenda kuzikwa mkoani Arusha leo.

Akizungumza baada ya mamia kumuaga nyumbani kwa marehemu, mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Nyakwale Kibada, Said Pazi alisema kuwa wao kama majirani waliomba familia wapate fursa ya kumuaga jirani yao ambaye tangu ahamie ana muda wa miezi sita.

“Baada ya kuambiwa msiba upo Salasala tuliomba kama majirani na sisi tupatiwe fursa ya kuuaga mwili wa ndugu yetu ambaye alihamia mwaka jana… kwa kweli msiba wake umetusikitisha sana” alisema.

Akizungumzia tukio hilo alisema kuwa mtoto wa marehemu huyo, Allan Kimario (4) aliwataarifu majirani kuwa mama yake haamki na ndipo walipofika wakakuta ameuawa.

Mwenyekiti huyo alitoa pole na kusema atahakikisha wanaimarisha ulinzi na kuhimiza wenye viwanja ambavyo havijajengwa, wavifanyie usafi ili kuondoa vichaka ambavyo ni hatari kwa usalama.

#YALIYOJIRI>>>>Wanafunzi wa chuo kikuu cha cha Dar es salaam Wagoma.Fahamu zaidi hapa.

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) leo wamegoma wakiishinikiza Bodi ya Mikopo(HESLB) kuwapatia fedha zao za kujikimu.

Kwa kawaida wanafunzi hupewa fedha za kujikimu kila baada ya miezi miwili.
 
Makamu wa Rais wa serikali ya wanafunzi, Shamila Mshengema amesema mgomo huo ni matokeo ya taarifa zisizoeleweka zilizo kuwa zikitolewa na bodi juu ya lini fedha hizo zitatolewa.
 
Kwa kawaida pesa ya chakula huingiziwa kila baada ya siku 60 na mpaka sasa yapata wiki mbili pesa hiyo haijaingizwa
 
Mgomo huo unakuja zikiwa zimebaki siku mbili kabla ya Rais Magufuli Kuzulu chuo hicho kwa ajili ya uzinduzi wa jengo la Maktaba.

Monday, 30 May 2016

#YALIYOJIRI>>>Rais Magufuli amteua Mama Makinda kuwa Mwenyekiti Bodi ya NHIF, Jaji Lila kuwa jaji Mahakama ya Rufani.Fahamu zaidi hapa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Mhe. Jaji Shabani Ally Lila kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Kabla ya uteuzi huo Mhe. Jaji Shabani Lila alikuwa Jaji Kiongozi. Uteuzi huu umeanza leo tarehe 30 Mei, 2016.

Wakati huo huo, Rais Dkt. Magufuli amemteua Mhe. Anne Semamba Makinda kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF). Uteuzi wa Mhe. Anne Semamba Makinda ambaye ni Spika Mstaafu wa Bunge Ia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umeanza tarehe 25 Mei, 2016.

Mhe. Anne Semamba Makinda anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Balozi Ali Mchumo. Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amemteua Prof. Apollinaria Elikana Pereka kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (Dar es salaam Institute of Technology -DIT).

Prof. Apollinaria Elikana Pereka ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) Morogoro. Prof. Pereka anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Prof. Fredrick Mwanuzi ambaye amemaliza muda wake. Uteuzi huu umeanza leo tarehe 30 Mei, 2016.

#YALIYOJIRI>>>Serikali imeanza kutengeneza sheria ya kutambulisha Dodoma kama Makao Makuu ya nchi.Fahamu zaidi hapa.

Serikali imeanza kutengeneza sheria ya kutambulisha Dodoma kama Makao Makuu ya nchi na inatarajiwa kupelekwa bungeni ili kuondoa changamoto ya migogoro baina ya Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) na wananchi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama alisema hayo bungeni hivi karibuni.Alisema kuanzishwa kwa sheria hiyo kutarahisisha katika kuhamia Dodoma pamoja na kuondoa migongano ya kisheria kati ya taasisi mbalimbali inayosimamia masuala ya ardhi mkoani Dodoma, ikiwa ni pamoja na kueleza mipaka ya CDA.


“Nataka wananchi wa Dodoma waamini kuwa serikali ina lengo la kuhakikisha azma hii ya serikali kuhamia Dodoma inatekelezeka, ikiwa ni pamoja na kuondoa migogoro yote kwa kufuata sheria na taratibu na kunapokuwa na matatizo kwa ushirikiano wetu na wao inaisha,” alisema.Alisema.


watahakikisha migogoro yote inaisha, lakini kwa kufuata sheria ikiwa wananchi wana haki watapata na pale sheria inapowataka wao waipe haki serikali waoneshe ushirikiano.Waziri huyo alisema mji wa Dodoma utajengwa kisasa na kuonesha kweli ni makao makuu kama ilivyo miji mingine duniani kwa kuwa kioo cha nchi ilivyo.Alisema katika kuonesha nia ya serikali ya kuhamishia makao makuu Dodoma kabla ya kumalizika kwa mkutano wa Bunge watakutana na wabunge wa mkoa huo na wizara kujadiliana namna bora ya kuondoa changamoto hiyo.

#YALIYOJIRI>>>>GARI LA DAWASCO LAPARAMIA KITUO CHA MABASI NA KUJERUHI WATATU.Fahamu zaidi hapa.

Gari lenye namba za usajili T 369 BUZ linalomilikiwa na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) likiwa limeparamia kituo cha mabasi baada ya gari hilo kukosa mwelekeo na kugonga kituo hicho na kujeruhi abiria watatu waliokua kituoni hapo majira ya Saa 2 usiku jana eneo la Mbuyuni, Barabara ya Bagamoyo Dar es Salaam

#MICHEZO>>>PICHA:ZA TAIFA STARS KATIKA MCHEZO WA KIRAFIKI DHIDI YA KENYA ZIKO HAPA.

 Kikosi cha kwanza cha timu ya Soka ya Tanzania -Taifa Stars kilichoanza dhidi ya Harambee Stars ya Kenya hapo jana Jumapili.
 Mshambuliaji wa Taifa Stars, Elias Maguli (Kulia) akichuana na David Odhiambo wakati wa mchezo wa kirafiki wa Kimataifa uliofanyika Uwanja wa Moi Kasarani, Nairobi Kenya hapo jana. timu hizo zilitosahana nguvu kwa kutoka sare ya 1-1.
Winga wa Taifa Stars, Shiza Ramadhani akichuana na beki Joakins Atudo wa Harambee Stars katika mchezo huo.

#Breaking News>>> Upinzani wasusia kikao cha Bunge asubuhi ya leo.Fahamu zaidi hapa.

Wabunge wa Kambi ya upinzani wakitoka kwenye ukumbi wa Bunge wakipinga kushiriki tukio la kuapishwa kwa wabunge kupitia Baraza la Wawakilishi, mjini Dodoma, leo asubuhi.

#YALIYOJIRI>>> JIJI LA DAR ES SALAAM KUJENGEWA MFUMO WA KISASA WA UONDOAJI NA USAFISHAJI WA MAJITAKA PAMOJA NA MIUNDOMBINU MIPYA YA KUSAMBAZIA MAJISAFI MAENEO YASIYO NA MTANDAO WA MABOMBA.Fahamu zaidi hapa.

 Ramani inayoonesha Mpango wa upanuzi wa mfumo wa uondoaji wa majitaka katika jiji la Dar es salaam utakaotekelezwa na Serikali kwa lengo la kuondoa wastani wa uondoaji wa majitaka kutoka asilimia 10 hadi asilimia 30 ifikapo mwaka 2017.
 Mtambo mpya wa kusafishia maji katika chanzo cha maji Ruvu chini mara baada ya kukamilika.Mtambo huo sasa unazalisha maji lita milioni 270 kwa siku.
Taswira ya Mtambo wa Ruvu Juu mara baada ya upanuzi.

Na.Aron Msigwa- MAELEZO.

Serikali imesema kuwa katika mwaka wa fedha 2016/2017 itatekeleza mradi wa ujenzi wa mfumo mpya wa uondoaji na usafishaji wa majitaka yanayozalishwa katika jiji la Dar es salaam ili kuliweka jiji hilo katika hali ya usafi na kuongeza wastani wa huduma hiyo kutoka asilimia 10 ya sasa hadi asilimia 30 ifikapo mwaka 2017.

Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge amesema mradi huo utatekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Korea ya Kusini na Serikali ya Tanzania kwa gharama ya Dola za Kimarekani milioni 89.

Amesema mradi huo utahusisha upanuzi wa miundombinu ya maji taka kwenye maeneo ya katikati ya jiji, ujenzi wa miundombinu mipya ya kupitishia maji hayo katika maeneo ya Ilala, Magomeni hadi Ubungo pamoja na maeneo ya Sinza, Kinondoni , Mwananyamala, Oysterbay na Masaki.

Maeneo mengine yatakayoguswa na mradi huo jijini Dar es salaam ni Msasani, Kawe, Mbezi Beach, Kurasini,Keko, Chang'ombe, Temeke, Hananasif, Tandale, Kijitonyama, Makumbusho, Mabibo, Ubungo, Manzese, Sandali, Tandika na Miburani.Mhandisi Lwenge amesema mradi huo wa kipekee utahusisha ujenzi wa mitambo mitatu ya kisasa ya kusafisha majitaka katika maeneo ya Jangwani, Kurasini na Mbezi Beach.

Aidha, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Korea ya Kusini na Benki ya Dunia itatekeleza mradi wa huduma ya uondoaji wa majitaka na ujenzi wa miundombinu ya uondoaji wa maji ya mvua katika jiji la Dar es salaam ambayo yamekuwa kero kwenye miundombinu ya jiji hilo.

"Serikali tumeanza kutekeleza mpango wa kupanua mfumo wa uondoaji na usafishaji wa majitaka yanayozalishwa na watumiaji maji , usanifu wa awali wa miradi mipya ya majitaka umekamilika,kazi inayoendelea ni usanifu wa kina ili kuweza kupata vitabu vya zabuni na michoro itakayotumika kumpata mkandarasi wa ujenzi" Amesisitiza Mhandisi Lwenge.

Amesema kuwa kupitia mpango huo bomba linalomwaga majitaka baharini litaacha kutumika na badala yake maji hayo yatapelekwa katika mtambo mpya wa kisasa wa kusafisha majitaka utakaojengwa maeneo ya Jangwani ambao pia utasafisha majitaka kutoka maeneo yote ya katikati ya jiji Dar es salaam yaliyo jirani ambapo maji hayo ambayo yatakua yamesafishwa yatauzwa na kutumiwa katika shughuli mbalimbali za upozaji wa mitambo na umwagiliaji.

Amebainisha kuwa katika kulishughulikia tatizo la majitaka jijini Dar es salaam Serikali itajenga mitambo mingine miwili eneo la Kurasini na Mbezi Beach itakayotumika kuzalisha gesi asilia kwa ajili ya kuendeshea mitambo ya kusafishia maji hayo hivyo kupunguza matumizi na gharama za umeme.

Katika hatua nyingine Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge amesema katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali itafanya ukarabati na upanuzi wa mfumo wa kusambazia maji safi katika jiji la Dar es salaam.

Ujenzi wa mfumo huo unalenga kuongeza idadi ya wananchi wapya watakaounganishwa na mtandao wa mabomba ya maji safi kutoka Mradi wa Ruvu Juu na ule wa Ruvu Chini ulioigharimu Serikali bilioni 141 ambao sasa maji yake yanaingia katika matanki ya maji yaliyoko Chuo Kikuu Ardhi jijini Dar es salaam.

Amesema kukamilika kwa mradi wa Ruvu Chini na Ruvu Juu mpaka sasa kumeyawezesha baadhi ya maeneo ya jiji hilo yakiwemo ya Segerea, Kimara, Kibangu na Kinyerezi ambayo yalikua na mabomba ya maji maarufu kama mabomba ya mchina kuanza kupata huduma ya majisafi.

Aidha, kupitia miradi hiyo mikubwa Serikali inaendelea kuishughulikia kero ya uhaba wa maji katika maeneo ya Bunju,Mabwepande, Boko,Tegeta,Kunduchi, Mbezi Beach, Mbezi Juu, Salasala, Kawe, Makongo, Mikocheni, Msasani, Masaki, Mwananyamala, Kinondoni, Magomeni, Sinza, Manzese, Ubungo, Mabibo, Kigogo, Buguruni na maeneo yote ya katikati ya jiji hilo.

Mhandisi Lwenge amefafanua kuwa Kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 32.93 kimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa mfumo wa kusambaza majisafi katika jiji hilo na kuongeza kuwa wananchi wasiopata huduma ya maji kutoka mtandao wa maji wa DAWASCO wataendelea kuhudumiwa na mradi wa visima vilivyochimbwa.

" Hadi mwezi Machi, 2016 tumechimba visima 52 na kati ya hivyo visima 32 vinatumika kutoa huduma ya majisafi katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam" Amesema Mhandisi Lwenge.

Wakazi wa jiji la Dar es salaam wapatao milioni 4.5 wamekuwa wakipata huduma ya majisafi kutoka chanzo cha Ruvu Chini ambacho kwa siku kinazalisha mita za ujazo 270,000 kwa siku, Mtambo wa Ruvu Juu unaozalisha mita za ujazo 182,000, Mtambo wa mtoni 9000 na Visima Virefu 27,000 na kufanya jumla ya mita za ujazo zinazozalishwa kwa siku kufikia 502,000 kutoka 300,000 za awali.

#YALIYOJIRI>>>>>Serikali Yapiga Marufuku Pombe Ya Viroba ya Kwenye Mifuko Ya Plastiki.Fahamu zaidi hapa.

Mifuko ya plastiki inayofungasha pombe maarufu kama ‘viroba’ imepigwa marufuku na Serikali kuanzia mwakani. 
Sambamba na hilo Serikali pia, imepiga marufuku moja kwa moja utengenezaji, usambazaji, uingizaji nchini wa mifuko ya plastiki kuanzia mwaka huo.

Waziri wa Nchi , Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba aliwaambia wanahabari jana sehemu kubwa ya mifuko hiyo inayotolewa bure imekuwa ikichangia uchafuzi wa mazingira kwa kiasi kikubwa.

Wakati Makamba akiyasema hayo, Februari mwaka huu Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Luhaga Mpina aliondoa zuio la matumizi ya mifuko ya plastiki akisema kuwa itaziweka rehani ajira za Watanzania wanaofanya kazi kwenye viwanda vinavyotengeneza mifuko hiyo.

Pia, Mpina alisema itapunguza kasi ya uwekezaji wa viwanda vilivyowekeza katika bidhaa hiyo.

Akizungumza katika siku ya Mazingira Afrika, Mkurugenzi wa Mazingira, Dk Julius Ningu alisema maamuzi hayo yamelenga kulinda viwanda vilivyoajiri mamia ya Watanzania, tofauti na nchi nyingine zinazotegemea wazalishaji wa nje ya nchi.

Makamba akizungumzia uamuzi mpya wa kuzuia mifuko ya plastiki, alisema matumizi ya mifuko inayofungashia vileo na inayotumika katika matumizi mengine husambaa na kuchafua mazingira. Alisema mifuko ya plastiki inatajwa kuziba mifereji na kusababisha mafuriko na athari nyingine za mazingira.

“Leo (Jana), tumeamua kutangaza ili kuwaanda wahusika wasiendelee kuwekeza katika mifuko hii badala yake wasubiri utaratibu mwingine utakaowekwa na Serikali,” alisema Makamba na kuongeza kuwa:

 “Asilimia kubwa ya uchafu kwenye nyanzo vya maji, mito, maziwa na fukwe za bahari ni mifuko ya plastiki.” 
Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli, alisema Serikali inakamilisha majadiliano ya ndani na baadaye itawahusisha wadau kuhusu dhamira ya kupiga marufuku ya moja kwa moja mifuko hiyo.

Alifafanua kwamba Serikali itatoa muda kwa walioajiriwa, kujiajiri na kuwekeza kwenye biashara ya mifuko hiyo ili kujiandaa kuacha shughuli hizo na badala yake itawezesha mazingira ya utengenezaji na upatikanaji wa vifungashio mbadala.

“Kwa wanaotengeza mifuko hii na kuiuza katika soko la nje hatuna tatizo nao waendelee. Ila kwa soko la ndani hawataruhusiwa kufanya hivyo.Zuio hili litakuwa la kisheria siyo kwa maneno,” alisisitiza Makamba. 
Aliongeza kuwa katika kuonyesha Serikali imedhamiria kupambana na hali hiyo wizara yake imeamua kutuma timu ya watu watano kwenda Rwanda kujifunza namna bora ya kudhibiti matumizi na kuzuia mifuko hiyo tangu mwaka 2008.

Waziri huyo alitoa wito kwa watengenezaji, wasambazaji na waagizaji wa mifuko hiyo kujiandaa na zuio hilo na katika siku zijazo Serikali itatoa utaratibu na maelekezo ya tarehe ya kuanza zuio huku taratibu nyingine za kina zikifuata ili kuondoa mkanganyiko.

 Katika hatua nyingine, Makamba alisema maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo hufanyika Juni 5 kila mwaka hayatafanyika kitaifa badala yake wizara imewaelekeza wakuu wa mikoa kufanya maadhimisho katika maeneo yao.

 “Tumewapa miongozo kuhusu utekezezaji wa shughuli hizo za maadhimisho zinazolenga kutoa hamasa ya hifadhi ya mazingira hususan nyanzo ya maji amabayo ni muhimu kwa viumbe hai,” alisema Makamba.

Kwa mujibu wa Makamba, kauli mbiu ya mwaka huu kitaifa juu ya maadhimisho hayo ni ‘ tuhifadhi vyanzo vya maji kwa uhai wa taifa letu’aliwashauri na kuwataka Watanzania kutumia siku hiyo kupanda miti, kudhibiti uchomaji wa misitu 
Ofisa Mwandamizi Mazingira wa Nemc, Arnold Kisagala alisema nusu ya mifuko ya plastiki nchini inazalishwa na kuingizwa kutoka nchi jirani ya Kenya.

Alisema agizo la Waziri Makamba litawezekana, lakini linahitaji ushirikiano kutoka kwenye sekta zingine kwa kuwa viwanda vingi vya mifuko ya plastiki vipo Kenya.

"NEMC tayari tulishaanza mazungumzo na wazalishaji kuhusu mifuko ya plastiki,” alisema.