Na Baraka Mbolembole
SIMBA SC ipo katika hatua za mwisho kumsaini mkufunzi, Milovan Curkovic ambaye aliifundisha timu hiyo kwa vipindi viwili (lakini si zaidi ya miaka miwili.) Kwa mara ya kwanza, Mserbia huyo alijiunga na Simba kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa ligi kuu Tanzania Bara msimu wa 2007/08.
Milovan alishuhudia timu hiyo ikimaliza katika nafasi ya tatu nyuma ya Yanga SC waliotwaa taji na Tanzania Prisons ilimaliza katika nafasi ya pili.
Baada ya kurejea nyumbani kwao Serbia kwa mapumziko, Milovan aliyekuwa na mkataba wa muda mfupi hakurejea tena kuinoa timu hiyo licha ya kwamba tayari mkataba mpya ulikuwa umeandaliwa na uongozi wa Mzee Hassan Dalali.
Siasa za Simba na Yanga zilitajwa kama sababu ya mwalimu huyo kutorejea huku Mserbia mwenzake, Dusan Kondic aliyekuwa kocha wa Yanga akitajwa kama ‘mshawishi aliyemkataza’ Milovan kurejea kuinoa timu iliyokuwa na ‘msuguano wa viongozi’.
Dalali na aliyekuwa katibu wake Mwina Kaduguda walikuwa na tofauti za mara kwa mara ambazo ziliwafa, Neidor Dos Santos na Nelson Elias raia wa Brazil kushindwa kufanya nao kazi.
Milovan si kocha mbaya, lakini anarudi Simba kufanya nini? Anapenda kufundisha mpira wa chini na wa kupasiana. Simba wanatamaduni ya kiuchezaji ambayo makocha watatu tu kati ya 16 waliopita ndani ya miaka 16 hii waliimudu kiasi cha kupendwa sana mashabiki.
Mkenya, James Siang’a alikuwa na miaka minne ya kupendeza sana kati ya mwaka 2000 hadi 2004. Vipindi viwili tofauti vya Mzambia, Patrick Phiri viliambatana na mchezo wa kuvutia kwa ‘Wekundu wa Msimbazi’ na Milovan anakumbukwa kwa msimu wa 2011/12 ambao Simba ilitwaa taji lake la mwisho la ligi kuu huku pia wakiwachapa 5-0 mahasimu wao Yanga (kipigo cha kihistoria katika karne mpya.)
Lakini yatakuwa ni makosa kumrejesha Milovan kwa maana mwalimu huyo si mtu makini wa kusimamia nidhamu katika timu.
Rejea sehemu ya MAKALA HAYA ambayo niliyaandika Novemba, 2012 baada ya Simba kushindwa kupata ushindi dhidi ya Polisi Moro FC na Mtibwa Sugar. Makala haya yalitumika na uongozi wa Ismail Aden Rage kumuondoa mwalimu huyo ambaye alirejea kwa mara ya pili klabuni hapo Novemba, 2011 kuchukua nafasi ya Mganda, Moses Basena.
Tuesday, November 6, 2012
SIKU SITA ZA SIMBA MORO NA POINTI YAO MOJA: NA KOCHA MILOVAN
Simba ilifikia katika, Hotel ya Usambara, ambayo humilikiwa na Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Mzee Yusuph Makamba. Kuna wachezaji waliolala katika vyumba vya gharama ya 20,000 na wapo waliolala katika vile vya gharama ya 25, 000.
Kocha Milovan Curkovic, yeye aliandaliwa chumba cha gharama ya 50, 000. Vikaanza vioja. Kocha akakataa kufikia Hotel isiyo na huduma ya Internet. Viongozi kwa kushirikiana na Meneja wa Hotel hiyo wakamtafutia Kompyuta yenye huduma ya Internet, lakini, Milovan, akakataa na kusema kwa kiswahili kizuri.
“Nataka yenye wireless” viongozi wachache tena wa ngazi ya chini, wakashindwa na kuingia katika mtego wa Milovan, ambaye tangu awali alionesha kutotaka kukaa katika Hotel ile. Kocha wa makipa wa timu hiyo akasema.
“Hana lolote, hakuna cha Internet wala nini anataka Mwanamke tu huyo kocha hamna kitu na sasa anaongea hadi Kiswahili…”, alikuwa akiongea mbele ya wachezaji wachache.
Milovan, akahamishiwa katika hotel yenye hadhi zaidi na gharama ya chumba ni zaidi ya 60, 000. Hakwenda pamoja na timu akitokea hotelini. Simba walitoka zao kivyao kutokea, Usambara, Milovan, akatokea ARC Hotel. Wakapata pointi moja mbele ya Polisi Moro.
…………………..
Milovan anarudi tena Simba akiwa na mafanikio gani kiufundishaji tangu alipoondoka Desemba, 2012? Alipoondolewa alimsema sana Geofrey Nyange ‘Kaburu’ kwamba ni ‘kiongozi anayependa kuingilia majukumu ya kocha katika upangaji wa timu.’
Je, ataweza kufanya kazi na Zacharia Hans Poppe? Ni kujidanganya wenyewe, kuamini Milovan anaweza kuirejesha juu Simba. Ndani ya wachezaji wenyewe timu imekosa kiongozi, ndani ya uongozi kuna utofauti mkubwa. Milovan anaweza kufanya kazi hivi sasa na Kaburu kwa maana kwa mwaka sasa amejiondoa katika ‘mtindo wake wa kuingilia majukumu ya kiufundi’.
Lakini mtu tishio zaidi kwake ni Poppe na Milovan mwenyewe ni mtu wa kuzurura hovyo na kujijali binafsi kuliko nidhamu yake mbele ya wachezaji, na kuheshimiana kati ya wachezaji kwa wachezaji.
Simba ingeongeza nguvu kumpata Mscotland, Bobby Williamsons na kuachana na makocha wa dola 6000. Bobby ni ghali lakini Simba imekuwa ikimtamani. Amerejesha nidhamu na uwajibikaji katika timu ya Taifa ya Kenya na aliweza kufanikiwa zaidi katika hilo katika miaka yake mitano akiwa kocha wa timu ya Taifa ya Uganda.
Kocha mwingine mzuri ambaye labda Simba inapaswa kumtazama kwa ‘macho-maangavu’ ni Mserbia, Goran Kopunovic ambaye Januari hadi June, 2015 alikuwa kocha wa mpito klabuni hapo. Goran alisimamia vizuri nidhamu yake, na jambo hilo likasambaa kwa wachezaji lakini alitaka kulipwa si chini ya milion 26 kwa mwezi ili asaini mkataba mpya.
Kazi yake katika mzunguko wa pili wa ligi kuu msimu wa 2014/15 ilikuwa nzuri sana kwani si tu aliweza kushinda kikombe cha Mapinduzi Cup, bali akiwatumia wachezaji wengi vijana Simba ilikuwa ikiweka mpira chini. Alishinda dhidi ya Yanga na Azam FC na kazi yake haina shaka, aliweza kuijenga ‘timu iliyokuwa goigoi’ na kuipa nguvu ya kupigania ‘TOP2.’
Sababu za kimaslai ziliwafanya Simba kushindwa kuendelea kuwa naye. Alikuwa na thamani ya zaidi ya waliyotaka kumpa Simba.
Alipoondolewa Mcroatia, Z.Logarusic na nafasi yake kuchukuliwa na Mzambia, Patrick Phiri, Agosti, 2014 niliuliza, Phiri amerejeshwa kwa mafanikio gani aliyopata tangu alipoondoka Simba mwaka 2011? Nilisema sababu zilizile zilizomuondoa 2005 na 2011 kama zisingerekebishwa ndizo zingemuondoa kwa mara ya tatu ‘bila kuaga.’
Phiri hakupenda kupangiwa timu yake na viongozi wa klabu, na mara zote alizorejeshwa aliahidiwa kutokuwapo tena kwa kadhia hiyo. Ila alidanganywa kwa maana Poppe baada ya sare ya 1-1 dhidi ya Prisons katika uwanja wa Sokoine alisikika akiponda mbinu za Phiri katika moja ya vituo vikubwa vya radio nchini, pia bila hofu alisema namna alivyotaka yeye kuona Simba ikicheza.
Milovan amekuwa akiitaka sana Simba, kwa kuwa anapendwa na mashabiki, pia aliipa taji la mwisho la VPL lilioambatana na kuwachapa 5-0 ‘Watani wao wa Jadi’ katika game ya kufunga msimu. Lakini, je, nani amejibadilisha na kupiga hatua mbele za kiutendaji kati ya watendji wa klabu na Milovan? Yetu macho, tusubiri na tuone.
Tangu 2000 hadi sasa
Mkenya, James Siang’a (2000-2004-Nilimuelewa sana Tu)
Trott Moloto-Sauz (2005-Sikumuelewa)
Patrick Phiri- Zambia (2005)
Neidor dos Santos-Brazil (2006 aliwapa nafasi yosso)
Nelson Elias-Brazil (2006 Siku kadhaa)
Talib Hilal & Julio (2007)
Milovan Curkovic-Serbia (Nov.2007-April 2008)
Patrick Phiri-Zambia (2009-2011)
Moses Basena-Uganda (June 2011-Novemba)
Milovan Curkovic-Serbia (Novemba 2011-Novemba 2012)
Patrick Liewig-Ufaransa (Desemba 2012-Mei 2013)
Abdallah ‘King’ Kibadeni (June 2013-Novemba)
Z.Logarusic-Croatia (Desemba 2013-June 2014)
Patrick Phiri (Agosti 2014-Novemba 2014)
Goran Kopunovic-Serbia (Disemba 2014 -June 2015)
Dylan Kerr-Malta (Julai 2015- 2016 Januari)
Jackson Mayanja (Januari 2016 –Mei)
0 comments:
Post a Comment