Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad jana aliitikisa Zanzibar pale alipoanza ziara yake ya siku sita katika Wilaya ya Kaskazini A na kusababisha polisi kuwatawanya wafuasi wake kwa mabomu na risasi huku baadhi wakijeruhiwa.
Wakati wa ziara hiyo, shughuli za biashara
zilisimama kwa muda ili kupisha ziara ya Maalim Seif na mamia ya
wananchi wake kwa waume walimpokea na kumfuata kila alipoelekea.
Ulinzi
uliimarishwa katika maeneo yote ya Mkoa wa Kaskazini Unguja, wakati
wote wa ziara hiyo na vikosi vya ulinzi na usalama vilionekana vikipiga
doria kila mahali.
Akiwa Kinyasini, Jimbo la Chaani ambako
alifanya kikao cha ndani, wakazi wa eneo la Kivunge kwa mamia walianza
kujikusanya katika maeneo ambako Maalim Seif alitarajiwa kutembelea huku
wakijipanga barabarani kumsubiri kiongozi huyo. Hata hivyo, askari
wenye silaha waliwatawanya.
Katika kuwatawanya, polisi walitumia
mabomu ya machozi na risasi hali iliyosababisha kizaazaa kwa takriban
dakika 30 katika eneo la Kivunge kabla ya kurudi hali ya kawaida.
Baada ya hapo baadhi ya askari waliokuwa na silaha waliwazuia waandishi kusogelea eneo hilo wala kuwapiga picha majeruhi.
Mkazi
wa Kivunge ambaye alidai ni miongoni mwa watu waliopatwa na mkasa huo,
Omari Makame (32) alisema, “Sisi tumejipanga kwa heshima zote kumsubiri
kiongozi wetu kipenzi cha Wazanzibari, tukiimba kwa furaha lakini ghafla
tumepata kipigo na mabomu ya machozi, nini hiki kama siyo chuki na
choyo kibaya.”
Mkazi mwingine, Haji Omar (27) alisema hata baada
ya kuwajeruhi wenzao, polisi wali wakatalia kuwapa fomu za kwenda
kupata matibabu na hata walipopelekwa hospitali ya Kivunge, polisi
walifika na kuwachukua kwa nguvu.
“Wamekataa ushauri wa
madaktari wa hapa kwamba wawapeleke Hospitali ya Rufaa ya Mnazi mmoja,
lakini wamewachukua kwa nguvu wamekwenda nao Kituo cha Polisi
Mkokotoni,” alisema Omar.
Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa
Makosa ya Jinai Zanzibar, Salum Msangi alikiri kuwapo kwa tukio hilo
akibainisha kuwa yote hayo yanatokea kwa sababu kuna watu hawataki
kufuata sheria, lakini akasema Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini
Unguja, Hassina Tawfik ndiye mwenye nafasi ya kufafanua zaidi.
Juhudi
za kumpata Tawfik hazikufanikiwa ikielezwa na baadhi ya watendaji wa
ofisi yake kuwa bosi wao hapatikani na hawakuwa na mawasiliano na yeye.
Mkurugenzi
wa Haki za Binaadamu wa CUF, Pavu Juma Abdalla alifika katika Makao
Makuu ya Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja na kushuhudia majeruhi hao
wakiwa mikononi mwa polisi.
Waliojeruhiwa ni Makame Abdalla Makame (28), mkazi wa Kivunge Bondeni na Shaame Juma Haji (45) mkazi wa Tumbatu Chwaka.
“Tunapigwa
kwa sababu ya umma kuonyesha mapenzi kwa Maalim Seif, wangelikuja watu
wa vyama vingine wasingelipigwa lakini ipo siku hawa jamaa wataheshimu
haki zetu,” alisema mtu aliyejitambulisha kwa jina moja la Haji akisema
baadhi ya majeruhi ni ndugu zake.
Mkurugenzi wa Habari wa CUF, Salim Bimani ambaye alifika hospitali kuwaona majeruhi alisema:“Wenye
mabomu na risasi wamewahujumu watu bure kwa sababu za chuki lakini yote
hayo yana mwisho.”.
Bimani alisema Chama chake kinalaani kwa nguvu zote
uonevu na hujuma hizo walizo tendewa wananchi wasiokuwa na hatia.
“Tunatumia pia kumbukumbu za hujuma hizi za leo kuongeza ushahidi wa kesi yetu tutakaouwasilisha ICC,” alisema Bimani.
Ziara
yenyewe
Maalim Seif alianza ziara hiyo ya kwanza Unguja tangu
kumalizika kwa uchaguzi wa marudio aliosusa kushiriki katika eneo la
Kinyasini, Chaani na kupokewa na mamia ya wafuasi wake ambao walikuwa
wakiimba “rais! rais! rais!
Aliambatana na viongozi na watendaji
wa CUF, akiwamo Naibu Katibu Mkuu, Nassor Ahmed Mazrui; Bimani; Pavu
Abdalla na Mkurugenzi wa Mipango na Chaguzi, Omar Ali Shehe.
Aliondoka
Kinyansini kuelekea Gamba, Mkwajuni ambako mamia ya wananchi waliokuwa
wakimshangilia walijipanga barabarani na walionekana kuongezeka kadri
alivyoelekea Kaskazini na kukaribia Jimbo la Mkwajuni.
Baadaye
Maalim Seif aliwahutubia wajumbe wa kamati mbalimbali za wilaya na
majimbo akieleza kile alichosema ni mwelekeo wa kisiasa wa chama chake,
Zanzibar na Tanzania kwa jumla.
Alisema dunia ilishuhudia
ukiukwaji mkubwa wa haki na demokrasia visiwani humo, akidai kwamba
pamoja na maonyo ya jamii mbalimbali za kitaifa na kimataifa, watawala
waliamua kupora uamuzi wa mamlaka halali ya wananchi kupitia masanduku
ya kura ya Oktoba 25, 2015.
“Angalieni watu hawa walivyokosa
aibu, umma uliwakataa, mataifa yaliwakataa hata kuwanyima misaada lakini
bado hawakuonyesha dalili za kujali kutokana na dhulma waliyotenda.
“Nasema
hali hii haitupeleki pema sisi na Taifa kwa ujumla maana iliyoporwa ni
haki ya umma na haiwezekani kuisamehe dhambi hii, hivyo mwishowe si
mwema na dhuluma haiwezi kudumu kwa muda mrefu asilani, sasa kusema
hivyo kuna ubaya gani?”
Hata hivyo, Mwangalizi Mkuu wa Ujumbe wa
Waangalizi wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya (EU – EOM) kwa Tanzania,
Judith Sargentini amesema atawasilisha ripoti kamili na mapendekezo ya
umoja huo, kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana Alhamisi ijayo.
Maalim Seif aliwataka wananchi wote, kama walivyoikataa CCM
kabla ya uchaguzi, wakati na baada ya kupiga kura Oktoba mwaka jana,
kuunga mkono juhudi na mikakati ya CUF, ili kuhakikisha haki
inapatikana, uamuzi wao unaheshimiwa, kwa masilahi ya nchi na Taifa kwa
jumla.
Viongozi wa chama hicho Wilaya ya Kaskazini A,
walimhakikishia Maalim Seif; “sisi tuko tayari kwa lolote, na naona siyo
sisi pekee, kwa sasa kila mtu anaisoma namba, tutakuwa bega kwa bega
mpaka haki yetu ipatikane,” alisema Makame Bakari, mmoja wa makatibu wa
CUF.
0 comments:
Post a Comment