Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Charles Kitwanga na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela wametofautiana juu ya taarifa za kuwapo kwa tawi la kundi la kigaidi la Islamic State (IS) jijini Tanga
Juzi,
Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC Swahili) lilitangaza uwepo wa
watu waliojitambulisha kuwa wawakilishi wa kundi hilo wanaoendesha
operesheni kwa nchi za Afrika Mashariki.
Shirika hilo lilieleza
kuwa kundi hilo limetuma ujumbe na kujitambulisha kwa kutumia video ya
dakika moja waliyoituma kwenye mtandao wa Twitter na kuzungumza na
Waziri Kitwanga ambaye alithibitisha kuwa na taarifa hizo.
“Tumezisikia na tumechukua hatua. Askari wetu wanafanya operesheni,” alikaririwa Waziri Kitwanga.
Hata
hivyo, jana Mkuu wa Mkoa wa
Tanga, Martin Shigela aliwaambia waandishi wa habari, kuwa mauaji na
matukio ya ujambazi wa kutumia silaha yaliyotokea mfululizo katika
maeneo mbalimbali jijini hapa siku za karibuni hayahusiani na ugaidi.
Alifafanua kuwa wahalifu waliopo huko wamegundulika kuwa wahamiaji
haramu kutoka Ethiopia, ambao wanaingia nchini kwa kutumia vichochoro
vilivyoko kwenye mapori ya mpaka wa Kenya na Tanzania, wakielekea nchi
jirani. Wamekuwa wakiingia nchini kupitia baadhi ya maeneo ya wilaya ya
Mkinga.
Wahalifu hao hutumia mapango hayo, kujificha kwa muda wakati
wakisubiri kuendelea na safari yao kuelekea nchi za Kusini mwa Afrika.
“Napenda kuwajulisha wakazi wa Tanga na taifa kwa ujumla kwamba hapa
mkoani hatuna vita dhidi ya kundi lolote la ugaidi wala kikosi cha
Al-Shabaab, isipokuwa kuna operesheni maalumu ya kikosi kazi chetu cha
ulinzi na usalama, kinachopambana na mambo makuu matatu; kubwa ni
matukio ya uhalifu unaofanywa na wahamiaji haramu,” alisema Mkuu wa
Mkoa.
Alisema kamati ya ulinzi na usalama mkoa, baada ya kutafakari
mwenendo wa kiusalama kutokana na matukio ya uhalifu wa hapa na pale,
imeunda kikosi kazi kukomesha vitendo hivyo, vinavyofanya mkoa kutumiwa
kama uchochoro.
Shigela ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, aliyataja mambo
yanayoshughulikiwa na kikosi kazi hicho ni kudhibiti uingizaji wa dawa
za kulevya, magendo ya bidhaa zisizoruhusiwa au kuingizwa bila kufuata
utaratibu pamoja na wahamiaji haramu.
“Wahamiaji haramu ndilo jambo hatarishi sana hapa kwa sasa, kwa
sababu hao watu wakishaingia nchini kwa njia za panya na kufanikiwa
kujificha, basi wanaposikia njaa hulazimika kujitokeza mitaani kutafuta
chakula kwa kuvamia maduka, kama walivyofanya katika duka kuu la Central
Bakery mwishoni mwa mwezi uliopita”, alisema.
Akizungumzia wakazi wa Kata ya Amboni yaliko mapango na mapori
husika, aliwataka kuchukua tahadhari, hasa wale wanaofanya shughuli za
kilimo jirani, kwa kuacha kuwenda kwa muda maeneo hayo, hasa kipindi
hiki ambacho kikosi kazi kinaendeleza operesheni.
0 comments:
Post a Comment