WATANZANIA wametakiwa kuwa wazalendo na kuacha kutumia tamaduni za nje, ambazo zinachangia mmomonyoko wa maadili.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa, Paul
Makonda alipotembelewa ofisini kwake na wanafunzi wanaosoma shule za
Feza kutoka nchi 15 waliokuja nchini kutangaza utamaduni wao.
Alisema Watanzania wengi wamekuwa
wakiiga tamaduni za kigeni na kusahau utamaduni wao, ambao ungeweza
kuwatambulisha katika nchi nyingi na kuijenga sifa ya nchi.
Aliongeza kuwa ni jambo la kushangaza,
kuona watu kutoka nchi mbalimbali wakija Tanzania kutangaza utamaduni
wao ; na Watanzania wakikaa na kuishia kuiga tamaduni za watu na kuacha
tamaduni zao kupotea.
“Utamaduni mkubwa ambao tunaweza
kuutangaza ni lugha ya Kiswahili ambayo ndiyo pekee, inaweza kuitangaza
nchi yetu duniani kote na ikajenga heshima ya nchi kuliko kufuata
tamaduni ambazo haziwajengi Watanzania zaidi ya kuwaharibu,” alisema
Makonda.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Feza
Tanzania, Kadik Dakicek, ambao ndio waandaaji wa tamasha hilo,
wakishirikiana na International Festival Language and Culture, alisema
madhumuni makubwa ya ujio wa wanafunzi hao ni kutangaza tamaduni zao na
Tanzania ndio mwenyeji wa shughuli hiyo kwa mwaka huu.
“Tumewahi kufanya tamasha kama hizi za
kutangaza utamaduni katika nchi mbalimbali na mwaka huu tunafuraha kuona
Tanzania inakuwa mwenyeji wa tamasha hili, tunaamini kupitia tamasha
hili, nchi itajifunza mambo mbambali ambayo yatawasaidia kutangaza
utamaduni,” alisema Dakicek.
0 comments:
Post a Comment