Ramani inayoonesha Mpango wa upanuzi wa mfumo wa uondoaji wa majitaka katika jiji la Dar es salaam utakaotekelezwa na Serikali kwa lengo la kuondoa wastani wa uondoaji wa majitaka kutoka asilimia 10 hadi asilimia 30 ifikapo mwaka 2017.
Mtambo mpya wa kusafishia maji katika chanzo cha maji Ruvu chini mara baada ya kukamilika.Mtambo huo sasa unazalisha maji lita milioni 270 kwa siku.
Taswira ya Mtambo wa Ruvu Juu mara baada ya upanuzi.
Na.Aron Msigwa- MAELEZO.
Serikali
imesema kuwa katika mwaka wa fedha 2016/2017 itatekeleza mradi wa
ujenzi wa mfumo mpya wa uondoaji na usafishaji wa majitaka
yanayozalishwa katika jiji la Dar es salaam ili kuliweka jiji hilo
katika hali ya usafi na kuongeza wastani wa huduma hiyo kutoka asilimia
10 ya sasa hadi asilimia 30 ifikapo mwaka 2017.
Waziri wa
Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge amesema mradi huo
utatekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Korea ya Kusini na Serikali
ya Tanzania kwa gharama ya Dola za Kimarekani milioni 89.
Amesema
mradi huo utahusisha upanuzi wa miundombinu ya maji taka kwenye maeneo
ya katikati ya jiji, ujenzi wa miundombinu mipya ya kupitishia maji hayo
katika maeneo ya Ilala, Magomeni hadi Ubungo pamoja na maeneo ya Sinza,
Kinondoni , Mwananyamala, Oysterbay na Masaki.
Maeneo
mengine yatakayoguswa na mradi huo jijini Dar es salaam ni Msasani,
Kawe, Mbezi Beach, Kurasini,Keko, Chang'ombe, Temeke, Hananasif,
Tandale, Kijitonyama, Makumbusho, Mabibo, Ubungo, Manzese, Sandali,
Tandika na Miburani.Mhandisi
Lwenge amesema mradi huo wa kipekee utahusisha ujenzi wa mitambo mitatu
ya kisasa ya kusafisha majitaka katika maeneo ya Jangwani, Kurasini na
Mbezi Beach.
Aidha,
Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Korea ya Kusini na Benki ya
Dunia itatekeleza mradi wa huduma ya uondoaji wa majitaka na ujenzi wa
miundombinu ya uondoaji wa maji ya mvua katika jiji la Dar es salaam
ambayo yamekuwa kero kwenye miundombinu ya jiji hilo.
"Serikali
tumeanza kutekeleza mpango wa kupanua mfumo wa uondoaji na usafishaji
wa majitaka yanayozalishwa na watumiaji maji , usanifu wa awali wa
miradi mipya ya majitaka umekamilika,kazi inayoendelea ni usanifu wa
kina ili kuweza kupata vitabu vya zabuni na michoro itakayotumika
kumpata mkandarasi wa ujenzi" Amesisitiza Mhandisi Lwenge.
Amesema
kuwa kupitia mpango huo bomba linalomwaga majitaka baharini litaacha
kutumika na badala yake maji hayo yatapelekwa katika mtambo mpya wa
kisasa wa kusafisha majitaka utakaojengwa maeneo ya Jangwani ambao pia
utasafisha majitaka kutoka maeneo yote ya katikati ya jiji Dar es salaam
yaliyo jirani ambapo maji hayo ambayo yatakua yamesafishwa yatauzwa na
kutumiwa katika shughuli mbalimbali za upozaji wa mitambo na
umwagiliaji.
Amebainisha
kuwa katika kulishughulikia tatizo la majitaka jijini Dar es salaam
Serikali itajenga mitambo mingine miwili eneo la Kurasini na Mbezi Beach
itakayotumika kuzalisha gesi asilia kwa ajili ya kuendeshea mitambo ya
kusafishia maji hayo hivyo kupunguza matumizi na gharama za umeme.
Katika
hatua nyingine Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge
amesema katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali itafanya ukarabati na
upanuzi wa mfumo wa kusambazia maji safi katika jiji la Dar es salaam.
Ujenzi
wa mfumo huo unalenga kuongeza idadi ya wananchi wapya
watakaounganishwa na mtandao wa mabomba ya maji safi kutoka Mradi wa
Ruvu Juu na ule wa Ruvu Chini ulioigharimu Serikali bilioni 141 ambao
sasa maji yake yanaingia katika matanki ya maji yaliyoko Chuo Kikuu
Ardhi jijini Dar es salaam.
Amesema
kukamilika kwa mradi wa Ruvu Chini na Ruvu Juu mpaka sasa kumeyawezesha
baadhi ya maeneo ya jiji hilo yakiwemo ya Segerea, Kimara, Kibangu na
Kinyerezi ambayo yalikua na mabomba ya maji maarufu kama mabomba ya
mchina kuanza kupata huduma ya majisafi.
Aidha,
kupitia miradi hiyo mikubwa Serikali inaendelea kuishughulikia kero ya
uhaba wa maji katika maeneo ya Bunju,Mabwepande, Boko,Tegeta,Kunduchi,
Mbezi Beach, Mbezi Juu, Salasala, Kawe, Makongo, Mikocheni, Msasani,
Masaki, Mwananyamala, Kinondoni, Magomeni, Sinza, Manzese, Ubungo,
Mabibo, Kigogo, Buguruni na maeneo yote ya katikati ya jiji hilo.
Mhandisi
Lwenge amefafanua kuwa Kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 32.93
kimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa mfumo wa
kusambaza majisafi katika jiji hilo na kuongeza kuwa wananchi wasiopata
huduma ya maji kutoka mtandao wa maji wa DAWASCO wataendelea kuhudumiwa
na mradi wa visima vilivyochimbwa.
"
Hadi mwezi Machi, 2016 tumechimba visima 52 na kati ya hivyo visima 32
vinatumika kutoa huduma ya majisafi katika maeneo mbalimbali ya jiji la
Dar es salaam" Amesema Mhandisi Lwenge.
Wakazi wa
jiji la Dar es salaam wapatao milioni 4.5 wamekuwa wakipata huduma ya
majisafi kutoka chanzo cha Ruvu Chini ambacho kwa siku kinazalisha mita
za ujazo 270,000 kwa siku, Mtambo wa Ruvu Juu unaozalisha mita za ujazo
182,000, Mtambo wa mtoni 9000 na Visima Virefu 27,000 na kufanya jumla
ya mita za ujazo zinazozalishwa kwa siku kufikia 502,000 kutoka 300,000
za awali.
0 comments:
Post a Comment