Chadema imesema haitabadili msimamo wake wa kutaka wataalamu kutoka nje kuchunguza shambulio dhidi ya mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Juzi, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba alisema hakuna haja ya kuhangaika kutafuta wachunguzi kutoka nje kwa kuwa mazingira watakayofanyia kazi ni yaleyale na hivyo kuitaka Chadema kuviamini vyombo vya ndani vya uchunguzi.
Lakini jana, Chadema imeeleza kuwa haioni kinachoendelea na hata kama ni mazingira yaleyale, wachunguzi kutoka nje ndiyo muafaka.
Lissu, mmoja wa wabunge wa upinzani asiye na woga wa kusema anachokiamini, alishambuliwa kwa risasi mchana wa Septemba 7 akiwa katika gari nje ya makazi yake mjini Dodoma akitokea bungeni.
Pamoja na washambuliaji kufyatua risasi zipatazo 32, Lissu alinusurika kifo na kupelekwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na baadaye alipelekwa Nairobi, Kenya kwa matibabu zaidi, safari ambayo iligubikwa na mabishano baina ya Chadema, uongozi wa Bunge na Serikali, iliyotaka ahamishiwe Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Chadema imekuwa ikihusisha shambulio hilo na tofauti za kisiasa na hivi karibuni ilisema pamoja na kuwa na imani na vyombo vya usalama, inataka wachunguzi kutoka nje kwa kuwa vyombo vya dola vimetuhumiwa.
Mkurugenzi wa itikadi na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema aliiambia Mwananchi jana kuwa ikiwa Serikali haina hofu, iruhusu wachunguzi hao ili yapatikane majibu ya nani alihusika.
Mrema alisema hakuna haja ya kuzuia wachunguzi hao kwa kuwa wana uwezo wa ziada.
“Kwa nini Serikali haitaki wachunguzi huru? Ni kweli kwamba wakija watafanya kazi kwa mujibu wa sheria za nchi, lakini hii haibadili msimamo wetu, hawa wana vifaa na wanaweza kusaidia kupata majibu,” alisema Mrema.
Alisema tangu kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto alipotoa taarifa za awali za tukio hilo, hakuna taarifa nyingine zozote zilizopatikana, jambo ambalo alisema linaendelea kuwatia hofu.
Mrema alisema yapo mauaji mengi kama ya Kibiti ambayo wananchi hawajui matokeo ya uchunguzi wala hakuna waliofikishwa mahakamani.
Kiongozi huyo wa Chadema alisema hata suala la mauaji ya Kibiti halijatolewa taarifa wala watuhumiwa kufikishwa mahakamani, huku kada wa chama hicho, Ben Saanane akiwa hajulikani alipo na mauaji ya mwenyekiti wa Chadema mkoani Geita, Alphonce Mawazo yakiwa hayajatolewa ripoti.
Alisema wataalamu hao kutoka nje wapo tayari kuja kufanya kazi ya kuchunguza tukio hilo na kwamba kitendo cha kuwakataa kinaongeza shaka kwao.
“Tunakaribia mwezi hatujui chochote,” alisema Mrema.
“Kwa hiyo muafaka ni wachunguzi huru. Mtu hawezi kupigwa risasi mchana kweupe tena Dodoma Mjini...” alisema.
Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa alisema kuzuia wachunguzi hao kunawafanya wafikirie kuwa kuna watu ambao hawataki kuumbuka na kuongeza kuwa kama nia ipo, iwaruhusu.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment