Serikali imejitoa katika Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi (Open Government Partnership-OGP) hatua ambayo inazua wasiwasi kuhusu utekelezaji wa sera ya uwazi iliyoasisiwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Hatua hiyo ya kujitoa kwa Tanzania ilitarajiwa kutangazwa wakati wowote na Kamati ya Uongozi ya mpango huo inayokutana katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kinachoendelea New York, Marekani.
Tanzania ilijiunga na mpango huo mwaka 2011 na hivyo kuwa nchi ya pili barani Afrika ikitanguliwa na Afrika Kusini ambayo ilikuwa ya kwanza kusaini makubaliano hayo yanayotaka nchi kuondokana na kasumba ya kuendesha mambo kwa usiri kati yake na wananchi.
Zaidi ya nchi 70 duniani zimesaini mpango huo unaohimiza dhana ya uwazi na ukweli. Rais mstaafu Kikwete alikuwa mstari wa mbele kuunga mkono mpango huo na alifanikisha mkutano wake uliofanyika kwa mara ya kwanza nchini 2015 ikiwa miezi michache kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu.
Wakuu wa mpango huo wanakutana New York wakijadiliana mambo mbalimbali ikiwamo ajenda inayoangazia kuongezeka kwa hali ya kutoaminiana kati ya Serikali na wafanyabiashara. Pia, wanaangalia njia zinazopaswa kuchukuliwa ili pande hizo ziweze kurejea katika hali yake ya kawaida.
Hata hivyo, Serikali ya Tanzania bado haijaweka hadharani juu ya hatua yake iliyochukua ya kujitoa kwenye mpango huo. Pia, haikuweza kufahamika mara moja kama maofisa wake walioko mjini New York watapeleka ujumbe uliochukuliwa nyumbani na Serikali.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kikanda, Augustine Mahiga yuko New York akimwakilisha Rais John Magufuli mkutano wa Umoja wa Mataifa.
Alipoulizwa kuhusiana na hatua hiyo iliyochukuliwa na Serikali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki alikataa kueleza lolote lakini akasema kuwa Serikali itatoa ufafanuzi wake muda utakapowadia.
“Nisikilize, sisi (Serikali) tutalieleza hilo tutakapoona inafaa,” alisema Waziri Kairuki ambaye hakukanusha wala kukiri lolote.
Lakini, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Aziz Mlima alikiri kuhusu Tanzania kujiondoa katika mpango huo.
“ Ndiyo ni kweli lakini ni kwa muda tu kwa sababu Serikali inataka kuutathmini mpango huo kama unaendana na masilahi ya Taifa,” alisema.
“ Kuna mambo tunahitaji kwanza kuyatekeleza kabla ya kutekeleza mpango huu,” alisema. Hata hivyo, vyanzo vya kuaminika vimelidokeza gazeti hili kuwa utawala wa Rais Magufuli unapenda kujikita zaidi katika utekelezaji wa Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora barani Afrika (APRM).
Kabla ya kujitoa katika mpango huo wa OGP, Tanzania ilikuwa tayari imepitia hatua mbili za utekelezaji na sasa ilikuwa ikijiandaa kutekeleza mpango mkakati wa tatu uliokuwa uanze 2016/17-2017/18.
Katika mipango hiyo, Tanzania ilikuwa imeainisha maeneo saba ya kuweka mkazo ikiwamo Sheria ya Kupata Habari, Bajeti ya Uwazi, Uwazi katika ardhi na madini.
Akizungumzia mpango huo mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Faraja Kristomus alisema wengi waliitazama OGP kama mpango wa nje zaidi na kukosa uungwaji mkono katika taasisi za kiserikali.
Katika makala zake zilizochapishwa na gazeti la Citizen, Kristomus ameandika kuwa wizara iliutazama mpango huo kama chombo chenye urasimu na haukusaidia kukaribisha mageuzi.
Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema hatua ya Tanzania kujiondoa katika mpango huo ni ishara nyingine ya kuanguka kwa demokrasia na uwazi serikalini. “Kitendo cha kujiondoa ni kuiambia dunia kuwa hatuko tayari kwa uwazi,” alisema.
Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alisema uwazi kwa serikali ilikuwa silaha tosha ya kukabiliana na rushwa.
“Tanzania ilikuwa haitekelezi kikamilifu mahitaji yote ya OGP. Lakini naamini kuwa angalau ilikuwa njia sahihi ya mwelekeo wetu. Hatua ya kujiondoa ilikuwa siyo wazo nzuri. Tunarudi nyuma katika eneo la utawala bora,” alisema.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment