WAKATI
fulani, kiungo nyota wa Yanga mwanzoni mwa miaka ya 2000, Waziri
Mahadhi, alibandikwa jina la Gaizka Mendieta. Hii ilitokana na umahiri
wake na ufanyaji mambo kwa uhakika katika safu ya kiungo.
Mahadhi,
alibandikwa jina hilo kutokana na umahiri wa kiungo nyota wa Valencia
wakati huo. Huyo ni Gaizka Mendieta Zabala ambaye alikuwa akiichezea
Valencia.
Baadaye
Mendieta alijiunga na Lazio mwaka 2001 ambako alidumu kwa msimu mmoja
akicheza mechi 20 na wao wakaamua kumtoa kwa mkopo FC Barcelona ambako
alicheza mechi 33 na kufunga mabao manne.
Akiwa Hispania, sehemu aliyopata mafanikio makubwa ni wakati yuko na kikosi cha Valencia ambako alizoa makombe lukuki.
Alibeba
Copa del Rey, Super Cup ya Hispania, Uefa Intertoto, na Uefa Champions
League mara mbili akaingia fainali ingawa mara zote hakufanikiwa kubeba
ubingwa.
Alipokwenda
England alijiunga na Middlesbrough ambako alifanikiwa kubeba Kombe la
Ligi, yeye ndiye akiwa kiungo mchezeshaji tegemeo.
Kazi
anayofanya ni kazi ya muziki. Sasa yeye ni Disco Joker, maarufu kama DJ
au mchezesha muziki. Kazi ambayo amekuwa akiwashagaza wengi kwa kuwa
sasa ni DJ wa kimataifa.
Mendieta
ni mchezaji mkubwa ambaye hata katika kikosi cha Hispania ambacho si
kazi rahisi kupata namba na hasa katika nafasi ya kiungo, Mendieta
alipata nafasi ya kucheza mechi 40 na kufunga mabao nane. Hii pekee
inatosha kumtambusha kama mmoja wa wachezaji wa kiwango cha juu duniani.
Mendieta
ni jina linaloheshimika katika soka la Hispania, lakini heshima yake
iko juu duniani kote kutokana na heshima aliyoipata wakati anacheza.
Kwa
sasa amestaafu na ukitaka kumuona ni wakati anaichezea timu ya wakongwe
wa Barcelona kama ambavyo wiki chache zilizopita alipopiga chenga na
kufunga bao la pili na kufanya mechi yao dhidi ya Manchester United
kwisha kwa sare ya mabao 2-2.
Pamoja na heshima kubwa katika mpira, Mendieta sasa anafanya mambo mawili tu, kwanza ni biashara na pili ni kazi.
Amekuwa
ni DJ wa kimataifa kwa kuwa anaalikwa katika matamasha mbalimbali
makubwa ili kuchezesha muziki na sasa amekuwa mmoja wa MaDJ wanaolipwa
vizuri zaidi duniani.
Udj
imekuwa ni kazi anayoifanya kwa ufasaha mkubwa na sasa heshima yake
imepanda kwa kuwa anaalikwa mara kadhaa katika matamasha makubwa ambayo
hualikwa wale wanaoaminika au wazoefu hasa.
Mendieta anasema, kazi hiyo si rahisi na wakati anaanza wengi walidhani atakata tamaa.
“Niliipenda sana hii kazi tangu nikiwa mwanasoka na kazi yangu muda wote na wengi walidhani natania lakini nilijua sitaacha.
“Kwangu
Udj imekuwa kama soka tu, maana ni kazi yangu, pia ni burudani yangu.
Hivyo nafanya kazi hii huku nikiwa naifurahia maana inaniburudisha hata
kabla ya kipato.
“Kweli
soka ni namba moja wakati huo, sasa muziki ni namba moja kwangu maana
ni burudani na kazi na ninaendelea kujifunza vizuri vingi ingawa wengine
wananiita ni wa kimataifa. Lakini nitaendelea kujifunza zaidi,”
anasema.
Pamoja
na kazi hiyo ya muziki, Mendieta ameamua kuwa mfanyabiashara na vitu
vingi vinasimamiwa na mkewe ambaye ni “mwanamke wa chuma.”
Mara
nyingine, Mendieta anakuwa na mkewe na wanafanya kazi ya kuendesha
migahawa mbalimbali ya kisasa katika maeneo mbalimbali ya Ulaya.
Sehemu
mojawapo ambayo wanamiliki mgahawa wa kisasa ni jijini London, England.
Lakini wanayo migahawa kwenye nchi nyingine kadhaa na imekuwa
ikiwaingizia fedha za kutosha kuendesha maisha yao pamoja na familia
yao.
Kuonyesha
kweli yuko makini na kazi zake, pamoja na kufanikiwa kufungua migahawa
zaidi ya minne, Mendieta ameonekana ni mwenye juhudi kubwa anayetaka
mafanikio zaidi ya hayo.
“Mimi
umri unakwenda, lazima nihudumie familia yangu. Kwanza nataka kuachana
na dhana kuwa mchezaji akistaafu basi au mchezaji anatakiwa ategemee
mambo ya soka tu,” anasema.
Tayari
Mendieta ni fundi wa kulicharaza gitaa la besi na anataka kujifunza
zaidi aina nyingine za magitaa ili kuujua muziki zaidi kwa kuwa hatanii.
“Niko makini na hili, nafanya ninachokipenda lakini naona ni sehemu itakayonibadilisha kabisa.”
Mendieta
ni kati ya watu wataratibu kabisa kama utakutana naye. Hapendi
kuzungumza sana lakini pia ni mtu anayependa kujumuika na watu hasa
rafiki zake wa zamani.
Anasema
mara nyingi asingependa sana kukumbuka mambo ya zamani yanayohusiana na
mpira na hasa kipindi ambacho anaamini mambo yalikuwa magumu.
“Nilifanikiwa kweli, kulikuwa na changamoto nyingi lakini mpira umenifunza kuwa imara na ninayetaka kupambana kama ilivyo leo.
“Lakini sipendi kuuzungumzia mpira kila mara na wakati mwingine ningependa kuzungumzia kazi yangu ya sasa na kujifunza zaidi.
“Timu
nilizopita mfano Valencia, mimi na wenzangu tulifanya vizuri kweli. FC
Barcelona, Lazio na Middlesbrough. Kila sehemu ina jambo ambalo
sitalisahau katika maisha yangu na kila moja limetofautiana.”
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment