Zikiwa ni takribani wiki mbili tangu Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mkoa wa Arusha, Alexander Mnyeti kuwaweka ndani madiwani wanne wa Chadema kwa madai ya kumkwamisha kutekeleza kazi zake, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Zephania Chaula naye amewasweka mahabusu madiwani wawili wa CCM.
Chaula
amewaweka ndani madiwani hao akiwamo wa Kata ya Emboreet, Christopher
Ole Kuya na wa Viti Maalumu, Diana Kuluo kwa madai ya kuvunja ofisi ya
Kijiji cha Emboreet na kushinikiza wananchi kuandamana ili kumpinga
mwenyekiti wa kijiji hicho.
Chaula alitoa amri ya kukamatwa kwa madiwani hao baada ya kuona wanaongoza kuharibu usalama kwenye eneo hilo.
Alisema madiwani hao waliwaongoza baadhi ya wanakijiji kuvunja ofisi ili kumshinikiza mwenyekiti wa kijiji hicho, John Olendikoni kujiuzulu na kusababisha waandamane kumpinga.
Alisema madiwani hao waliwaongoza baadhi ya wanakijiji kuvunja ofisi ili kumshinikiza mwenyekiti wa kijiji hicho, John Olendikoni kujiuzulu na kusababisha waandamane kumpinga.
Mkuu
huyo wa wilaya alisema alichukua hatua hiyo baada ya vyombo vya ulinzi
na usalama kumpa taarifa kuwa madiwani hao wanaongoza harakati za
kumng’oa madarakani mwenyekiti wa kijiji bila kufuata taratibu na
sheria.
“Sitakubali
kuona kiongozi yeyote hata kama ni kupitia CCM anafanya makosa, kisha
nikamuacha kwani suala la kumtaka mwenyekiti wa kijiji ajiuzulu lina
taratibu zake siyo kumwambia atoke kwenye kiti,” alisema Chaula.
Alisema,
awali aliwaeleza wahusika kuvuta subira juu ya suala hilo na kufuata
taratibu kupitia vikao, ili kubaini tatizo lililopo kwa madai kwamba
siasa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 vimeingizwa kwenye suala hilo.
“Nimeshawaagiza
watengeneze mlango na vyombo vyote vilivyoharibika kwenye ofisi hiyo
walipovunja na nimewapa taarifa kuwa nitawachukulia hatua wananchi
wakiandamana tena,” alisema mkuu huyo wa wilaya.
Alisema
amewaambia madiwani hao mchakato na taratibu za kumtoa mwenyekiti wa
kijiji zinaanzia halmashauri ya kijiji, mkutano mkuu wa kijiji, taarifa
kwa mkuu wa wilaya na mkuu wa mkoa.
“Tunafanya
kazi kwa utaratibu siyo shinikizo na nimewapa angalizo wawe viongozi wa
kuwapo kwa amani katika eneo hilo na yakizuka mengine nitawaweka ndani
tena kisha mahakamani,” alisema.
Akizungumza
baada ya kuachiwa kwenye Kituo cha Polisi Orkesumet, Ole Kuya alisema
hawakuwashinikiza wananchi kuandamana ili kumkataa mwenyekiti na kuvunja
ofisi ya kijiji.
“Sisi
hatuhusiki kwenye kuongoza harakati hizo, ila ni wananchi wenyewe
wameamua kupambana kwa ajili ya kudai haki zao baada ya kuona uongozi wa
kijiji unafanya mambo ambayo hawaridhiki nayo,” alisema Ole Kuya.
Kifungu
cha 15(1) cha Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997 kinawapa mamlaka
mkuu wa mikoa na wilaya kumuweka ndani mtu kwa saa 48 pale anapobaini
mhusika ametenda kosa.
0 comments:
Post a Comment