Rais Dkt John Pombe Magufuli, akilakiwa na Mwenyeji wake, Rais wa Kenya, Mh. Uhuru Kenyatta alipokaribishwa Ikulu, Nairobi nchini Kenya leo. Rais Magufuli yupo nchini Kenya kwa ziara ya kikazi ya siku mbili
Rais Dkt John Pombe Magufuli, akilakiwa na Mwenyeji wake, Rais wa Kenya, Mh. Uhuru Kenyatta alipokaribishwa Ikulu, Nairobi nchini Kenya leo. Rais Magufuli yupo nchini Kenya kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.
Rais Dkt John Pombe Magufuli akikagua gwaride la Jeshi la Kenya, alipowasili Ikulu jijini Nairobi leo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na ujumbe wake katika mazungumzo na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta pamoja na ujumbe wake katika Ikulu ya Nairobi.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema Kenya ni nchi inayoongoza
kwa uwekezaji nchini Tanzania ikilinganishwa na nchi nyingine za Bara la
Afrika.
Rais Magufuli
amesema hayo leo tarehe 31 Oktoba, 2016 katika mkutano na waandishi wa habari
uliofanyika katika Ikulu ya Nairobi nchini Kenya ambako ameanza ziara ya
Kiserikali ya siku mbili kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru
Kenyatta.
Rais Magufuli
ambaye kabla ya Mkutano huo na waandishi wa habari amepokelewa rasmi kwa
kupigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa kwa heshima yake na
baadaye kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta, amesema
takwimu za kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC) zinaonesha kuwa Kenya ina jumla
ya kampuni 529 zinazoendesha shughuli zake nchini Tanzania ambapo zimewekeza
Dola za Marekani Bilioni 1.7 na zimeajiri watu 56,260.
Pia, Rais Magufuli
amebainisha kuwa biashara kati ya Tanzania na Kenya imeongezeka kutoka Shilingi
za Kitanzania Bilioni 652.9 hadi Shilingi za Kitanzania Trilioni 2.044.
"Naomba
niwahakikishie kuwa uhusiano na ushirikiano wetu ni mzuri na utaendelea kuwa
mzuri zaidi, na kwetu sisi Tanzania, Kenya ndio nchi ya kwanza kwa uwekezaji
kuliko nchi zote za Afrika.
"Tunashirikiana
vizuri katika uchumi, watu wetu wanafanya kazi pamoja, yapo makabila yetu
ambayo yanaingiliana kwa shughuli zao za kila siku na hata wanyamapori wetu
wanazunguka katika nchi zote mbili bila kujali mipaka"
amesema Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli
amesisitiza kuwa Serikali yake itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na
Kenya ulioasisiwa na Rais wa Kwanza wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere na Rais wa Kwanza wa Kenya Hayati Mzee Jomo Kenyatta na amewakaribisha
wafanyabiashara wengi zaidi wa Kenya kuwekeza nchini Tanzania.
"Kabla ya
kuja hapa nimekwenda kutoa heshima katika kaburi la Mzee Jomo Kenyatta, kwa kweli
nimeguswa sana na kazi kubwa iliyofanywa na wazee wetu, naomba niwahakikishie
kuwa tunawathamini sana ndugu zetu Wakenya na tutaendelea kufanya hivyo"
amesisitiza Dkt. Magufuli.
Kwa upande wake
Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta amemshukuru Rais Magufuli kwa
kukubali mwaliko wake na amemhakikishia kuwa Kenya itaendeleza na kuimarisha
zaidi uhusiano na ushirikiano na Tanzania."Kwetu sisi
Tanzania ni ndugu zetu, ni kaka na dada zetu tunao ushirikiano wa siku nyingi
na wa kidugu na tutahakikisha tunauendeleza ushirikiano na uhusiano huu mzuri
ulioasisiwa na wazee wetu" amesema Mhe.
Kenyatta.
Rais Kenyatta amesema
Tanzania na Kenya ni nchi zinazofanana kwa mambo mengi muhimu ikiwemo
kubadilishana uongozi wa Serikali kwa njia ya amani na ameongeza kuwa katika
mazungumzo yao wamekubaliana kuwa nchi hizi zitaendelea kuzisaidia nchi
nyingine za Afrika Mashariki zinazokabiliwa na matatizo mbalimbali.
Aidha, Rais
Kenyatta amesema Kenya itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza
miradi ya ushirikiano ikiwemo ujenzi wa miundombinu kama vile barabara ya
Bagamoyo (Tanzania) hadi Malindi (Kenya) pamoja na mambo mengine ambayo Tume
ya pamoja ya ushirikiano kati ya nchi hizi mbili (Joint Commission Cooperation) itayaainisha.
Baadaye leo, Rais
Magufuli anatarajiwa kuhudhuria dhifa ya kitaifa katika Ikulu ya Nairobi
aliyoandaliwa na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta na Kesho anatarajiwa
kutembelea kiwanda cha maziwa cha
Eldoville kilichopo
Karen Jijini Nairobi, na kuzindua barabara
mchepuko ya Southern By-pass iliyopo
Jijini Nairobi.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Nairobi
31 Oktoba,
2016
0 comments:
Post a Comment