MARA
kadhaa, nimewahi kumzungumzia kinda Farid Mussa, kwamba ni kati ya
nyota ambao Tanzania imewapata na anapaswa kutupiwa jicho.
Nilieleza
kuwa sina hofu hata kidogo na Farid kupiga hatua hadi kucheza Ulaya.
Tena nikasisitiza muda wake ni sasa kwa kuwa wachezaji wengi kutoka hapa
nyumbani wamefeli kutokana na umri na wengi hukumbuka kwenda kucheza
nje, umri ukiwa umewatupa mkono.
Klabu ya Azam ilifanya juhudi na kufanikiwa kumpeleka Hispania kwa ajili ya majaribio, akafanikiwa, yaani amefuzu.
Sasa
ni zaidi ya miezi miwili, kijana huyo hajui la kufanya kwa kuwa
Uhamisho wake wa Kimataifa (ITC) umetumwa Hispania katika klabu ya
Daraja la Kwanza ya Tenerife, lakini hawezi kuichezea kwa kuwa
tumeelezwa tatizo ni visa.
Azam
FC imeeleza kwamba ishu ya Farid imekwama kwa kuwa hajapewa visa, hivyo
kuomba asaidiwe lakini mimi nilianza kuingia hofu mapema kwamba kuna
tatizo ndani ya suala hilo. Nikiwa Hispania katika mambo yangu, niliamua
kufunga safari hadi Tenerife hata bila ya kuwa na mwenyeji.
Nilifanikiwa
kuiona Tenerife ikicheza mechi moja ambayo ilimalizika kwa sare ya bao
1-1. Nilivyowaona wachezaji wenzake na Farid, hakika sikuwa na hofu hata
kidogo kuwa wakimpa nafasi atafanya vizuri na hakuna wa kumzuia hata
chembe.
Nikaanza
kufanya uchunguzi kutaka kujua ni kwa nini Farid anaendelea kubaki Dar
es Salaam. Kulikuwa na ugumu kwa kuwa viongozi walionekana kuwa na hofu
kunijibu na hakika ilionekana suala lenyewe, ndani yake kama kuna figisu
hivi.
Mmoja
wa viongozi anayeshughulikia masuala ya soka katika eneo la Tenerife,
alinieleza kuwa Farid ana tatizo la ndani ya Tenerife. Kwamba kuna
mgogoro ambao unafanya akwame kwenda na inaonekana katikati katika
usajili wake, kulikosekana uaminifu.
Hakutaka
kufafanua zaidi kuhusiana na uaminifu huo. Nilianza kupata harufu ya
shida na ndiyo maana mchezaji huyo anaendelea kubaki nje ya uwanja.
Niliporejea
hapa, niligundua Farid alichoka na kuacha mazoezi na Azam FC, akaamua
kwenda Morogoro kwa masuala yake ya kifamilia. Jambo jingine ambalo
niliona halikuwa sahihi kwake.
Kweli
kachoka kufanya tu mazoezi bila ya kucheza mechi za mashindano, si
jambo zuri kwa mchezaji yeyote yule anayetaka maendeleo, ni hatari zaidi
kwa mchezaji kukaa nje bila ya mazoezi kabisa hasa chini ya wasimamizi
wanaofanya mambo kitaalamu.
Ninajua
ndani ya suala hilo kutakuwa na figisu, namna wale viongozi wa Tenerife
walivyokwepa kulizungumzia, hakuna shaka ndani yake kuna shida ambayo
wanapaswa kuifanyia kazi.
Huenda
Tenerife wanaweza wasiwe na shida sana, lakini Azam FC wanatakiwa
kufanya kazi ya ziada ili kuepuka kumpoteza Farid kwani si wao peke yao,
ni kijana wa taifa zima.
Farid
ni hazina ya taifa, kama kuna jambo kati ya Tenerife na Azam FC, au
kuna kitu kimesababisha hali ya kutoelewana, basi kifanyiwe kazi na
Farid arejee uwanjani na kuendelea kupambana. Kwani hata akikosa
Tenerife, bado ana nafasi ya kuendelea zaidi na kucheza kwingineko
Ulaya.
Lazima
tukubali, Tanzania inahitaji wachezaji wengi kucheza nje ya Afrika na
hasa Ulaya ili kuwa na mabadiliko kwenye timu ya taifa. Farid anaweza
kuwa sehemu ya mabadiliko kama ataendelea kucheza.
Kuendelea
kubaki nje ya uwanja kama ilivyo sasa, tena saikolojia yake ikiendelea
kuathirika na mbaya zaidi kama hakuna anayekaa karibu naye. Mwisho
atakata tamaa na kudondoka katika mbio za mapambano kukimbilia
mafanikio.
Kinda
huyu kuendelea kukaa nje, si sawa hata kidogo. Suala hilo Azam FC
wanapaswa kuliangalia kwa upana wa utaifa na maendeleo ya kinda huyo.
Vizuri
iwe sasa kabla hajakata tamaa, inawezekana kweli Azam FC wana mambo yao
mengi muhimu ya kufanya, lakini Farid wanaweza kumuweka sehemu ya mambo
muhimu na kulimaliza suala lake ili wamsaidie aendelee. Tafadhali,
asipotee wakati uwezo wa kumuendeleza upo. Kuacha aishe au amalizike, ni
kujimaliza wenyewe.
0 comments:
Post a Comment