TIMU ya Azam FC yaonesha nia ya kuchukua kombe la ligi kuu Vodacom
Tanzania Bara baada ya kuendeleza mfululizo wa kushinda michezo yake ya ligi kuu Vodacom
Tanzania Bara imekaa kileleni kwa mara ya kwanza msimu huu baada ya
kuichapa JKT Ruvu mabao 4-2 kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania uliofanyika Uwanja wa Karume jioni ya leo.
Azam FC inakaa kileleni baada ya kufikisha jumla ya pointi 22 na
kuishusha Yanga yenye pointi 20 baada ya jana kuambulia sare ya mabao
2-2 dhidi ya Mwadui.
Kocha wa Azam FC, Stewart Hall, alifanya marekebisho kwenye eneo la
ushambuliaji la timu yake katika mchezo wa leo, akimuanzisha kwa mara ya
kwanza mshambuliaji Didier Kavumbagu raia wa Burundi.
Kavumbagu aliitumia vema nafasi hiyo aliyopewa baada ya kuifungia bao
la uongozi Azam FC katika dakika ya 4 akitumia vema pasi safi ya
Michael Bolou na kupiga shuti la kiufundi lililomshinda kipa wa JKT,
Shabani Dihile.
Dakika mbili baadaye nahodha wa Azam FC, John Bocco, aliitumia vema
krosi safi ya beki wa kulia Shomari Kapombe na kupiga shuti safi
lililomshinda kipa wa JKT.
Winga msumbufu wa JKT Ruvu, Najim Magulu, aliipatia timu yake bao la
kwanza dakika ya 31 kwa shuti akiwa ndani ya eneo la 18 akiunasa mpira
wa adhabu ndogo uliopigwa na mshambuliaji Saady Kipanga na kuwababatiza
mabeki wa Azam FC.
Hadi dakika 45 za kwanza zinamalizika, Azam iliondoka kifua mbele kwa
mabao 2-1, ambapo kipindi cha pili kilianza kwa Hall kumtoa kiungo
Michael Bolou na kuingia Himid Mao, JKT Ruvu nayo ilimtoa mshambuliaji
Gaudence Mwaikimba na kuingia Samwel Kamuntu.
Mwamuzi wa mchezo wa leo, Israel Nkongo kutoka Dar es Salaam aliamuru
penalti ipigwe langoni mwa JKT Ruvu dakika ya 63 baada ya beki wa timu
hiyo Paul Mhidze, kumkwatua beki wa Azam FC, Shomari Kapombe.
Bocco aliihakikishia Azam FC ushindi kwa kufunga vema penalti hiyo
dakika ya 64 kwa kuandika bao la tatu kwa timu na la tatu kwake msimu
huu kwenye ligi hiyo, JKT Ruvu ilirejea mchezoni baada ya kupata bao la
pili dakika 69 lililofungwa na Emmanuel Pius.
Hall alifanya tena mabadiliko dakika ya 77 kwa kumtoa Bocco na
kuingia Kipre Tchetche, ambaye aliifungia bao la nne Azam FC dakika ya
90 akipiga shuti la kiufundi la juu baada ya kuwahadaa mabeki wa JKT
Ruvu pembeni ya uwanja na kupiga shuti hilo lililomshinda kipa wa JKT.
0 comments:
Post a Comment