Mamlaka
ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) imetangaza kuanzishwa kwa
mfumo mpya wa ukataji wa tiketi za mabasi na daladala kwa njia ya
kielektroniki.
Hatua
hiyo ina lengo la kurahisisha upatikanaji wa mapato halali ya serikali
pamoja na kuwafanya madereva na makondakta, kuajiriwa rasmi na wamiliki
wa vyombo hivyo vya usafiri.
Pia
mamlaka hiyo imezindua kampeni ya usafi kwa wafanyakazi wa daladala,
ambayo inawataka kubadilisha sare za madereva na makondata, ambazo
walishonewa na matajiri wao.
Sasa wafanyakazi hao watashona sare zao wao wenyewe ili wawe na uhalali wa kuzimiliki na kuzifanyia usafiri wa mara kwa mara.
Mkurugenzi
wa Barabara wa Sumatra, Johansen Kahatano alisema jana kuwa mfumo huo
wa tiketi za daladala kwa njia ya elektroniki, utaanza kutumika Januari
mwakani.
Lakini, aliongeza kuwa kuanzia Desemba mwaka huu, watafanya mpango huo kwa majaribio kwa mabasi yaendayo mikoani.
“Kwa
sasa tumeanza mpango huo kwa majaribio kwa daladala za kampuni ya
Christian, Desemba tutaenda kwa mabasi ya mikoani na Januari mwaka
kesho, mfumo huo utaanza kwa mabasi na daladala zote,” alisema Kahatano.
Alitangaza
mfumo huo jana wakati wa uzinduzi wa kampeni ya usafi kwa madereva,
ambayo inahusisha usafi wa mwili, mavazi na mabasi uliofanyika katika
stendi ya Makumbusho, Dar es Salaam. Katika kampeni hiyo, madereva na
makondakta watajishonea wenyewe sare zao na sio wamiliki wa magari.
Kahatano
alisema chini ya mfumo wa ukataji wa tiketi kwa njia ya kielektroniki,
utamfanya mmiliki wa basi kujua mapato yake halisi kwa siku na hivyo
atawalipa wafanyakazi wake mshahara na Serikali itapata kiwango sahihi
cha kodi. Kwa sasa ukataji wa tiketi za mabasi na ule wa daladala,
unafanywa kwa tiketi zilizochapishwa.
Alisema kutokana na mfumo huo mpya, dereva haruhusiwi kumlipa mmiliki hesabu ya kila siku kama wanavyofanya sasa.
Badala
yake, mmiliki ndiye atatakiwa kumlipa dereva na kondakta wa gari lake
mshahara kila mwisho wa mwezi. Alisema ili malipo hayo yaweze kufanyika
ni lazima madereva waajiriwe rasmi na walipwe chini ya mfumo wa ajira.
“Kwa
hiyo dereva na mmiliki wataingia mkataba wa ajira tofauti na sasa hivi
hakuna mkataba wowote kati ya tajiri na wafanyakazi wake, badala yake
wanakubaliana tu kwamba hesabu ya siku ni kiasi fulani cha fedha na
dereva anahangaika kukitafuta,” alisema Kahatano.
Kuhusu
sare za madereva, alisema kwamba ndani ya wiki mbili madereva wa wilaya
ya Kinondoni, wote wanatakiwa wawe wamebadili sare zao na kushona
ambazo wamekubaliana na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi
(VETA).
Mkuu
wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Awadhi
Haji, alisema wao kama wasimamizi wa sheria, watahakikisha ndani ya
wiki mbili madereva wote wa daladala wa wilaya ya Kinondoni, wanashona
sare hizo mpya ambazo zimepitishwa na Sumatra.
Alisema
kutokana na agizo hilo, hategemei kuwaona tena makondakta na madereva
wachafu kwa kuwa watakuwa na sare zao binafsi ambazo watazitunza kuliko
ilivyokuwa awali.
“Wale ambao watakaidi tutawakamata na kuwafikisha mahakamani.”
0 comments:
Post a Comment