WAKATI gumzo nchi nzima likiwa ni wizi mkubwa ambao haujawahi kufanyika wa zaidi ya shilingi bilioni 300 kutoka akaunti iliyofunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya Tegeta Escrow, imeelezwa kuwa baadhi ya wabunge walikuwa wakihatarisha maisha yao na wengine wamepoteza ubunge kwa sababu ya kupinga ufisadi huo.
Vinara wa kufichua sakata hilo, aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, David Kafulila na Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe ndiyo waliofichua mambo hayo kwa nyakati tofauti.
Kafulila aliyehojiwa na gazeti hili wiki iliyopita alisema kundi lao la kupiga vita ufisadi huo lilikuwa hatarini kwa sababu kuna fedha zilikuwa zinatumika ili kuzima wizi huo.
Marehemu Deo Filikunjombe (ushoto), Davidi Kafulila, Zitto Kabwe pamoja na David Silinde.
“Hata wenzetu wabunge walikuwa wakitupinga na kwa kweli tulikuwa katika wakati mgumu, hata hivyo, hatukuacha kupigania jasho la umma ambalo lilikuwa limeliwa na watu wachache,” alisema Kafulila.
Alisema kuna wabunge ambao walikuwa wakiunga mkono vita hiyo nao walikuwa hatarini lakini kuna wengine ambao walikuwa upande wa mafisadi.
“Nashukuru kuna baadhi ya wabunge walikuwa wakiunga mkono vita dhidi ya ufisadi wa Escrow lakini baadhi walikuwa upande wa mafisadi. Ilikuwa hatari kwa sababu fedha zilikuwa zikitumika kuhujumu mpango mzima,” alisema Kafulila.
ZITTO ANENA
Naye Zitto katika andiko lake maalum amesema ili kuepuka kuuawa hasa kwa sumu, aliyekuwa Mbunge wa Ludewa ambaye likuwa makamu wake kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (PAC), Deo Filikunjombe alimleta dada yake (Zitto) mjini Dodoma ili awapikie chakula kwa ajili ya usalama wao.
Zitto alisema katika uchunguzi wao juu ya wizi huo alikutana na wengi akiwemo aliyekuwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh.
Siku niliyokutana naye nilimwambia: “Nimetoka kuonana na (namtajia jina na cheo – kwa sasa nalitunza si vema kumtaja), amenipa nyaraka zote za fedha zilizotunzwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow na kutolewa kulipwa PAP kama mmiliki wa IPTL. Sisi PAC tunataka sasa ufanye ukaguzi maalumu wa suala hili.”
BADE NA DK. HOSEA
Alisema kiongozi huyo na aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rashide Bade pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takururu), Dk. Edward Hosea walitoa ushirikiano mkubwa kufanikisha kazi yao.
“Tulipata msaada pia wa aliyekuwa Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, alitoa msaada mkubwa sana kwa kamati. Naye akatukanwa kuwa hakuwa msomi na alipata ziro akiwa kidato cha sita. Vyombo vya habari vilishangilia sana vioja hivi vya waziri kutaja matokeo ya shule ya mbunge bungeni ili kumvunjia heshima mbele ya jamii,” alisema Zitto.
Akaongeza kufafanua: “Ili kujenga umoja ndani ya Bunge nilimwomba spika (Anne Makinda) kuniongezea wajumbe kwenye kamati, ombi ambalo lilikubaIiwa. Tuliongezewa wajumbe kadhaa, akiwemo ndugu Kangi Lugola, Suleiman Zedi na Dkt. Hamis Kigwangalla.
“Hawa walikuwa ni viongozi wa Kamati nyingine. Lengo letu lilikuwa ni kuongeza nguvu kwenye Kamati ya Uongozi na pia sauti zenye uelewa. Tulitaka kuwe na taswira kubwa ya Kamati, isiwe tu ni PAC, iwe ni ya vyama vyote na yenye taswira ya kitaifa. Jambo hili lilitusaidia sana.
“Wakwapuaji nao walijipanga kwenye fedha. Walikuwa wanagawa fedha kwa kila mbunge anayechangia. Sisi tuliamua kuwachezea mchezo wa kupanga wachangiaji wetu wazuri siku ya mwisho na wao wakajaa kuchangia siku ya pili ya uwasilishaji wa taarifa bungeni, Alhamisi Deo Filikunjombe alifanya kazi hiyo ya mkakati.
“Spika Makinda na kabla yake Naibu Spika Ndugai walitupa ushirikiano mkubwa.
Ndugai alituambia wakati wa kukabidhiwa ripoti, namnukuu “Waelezeni Watanzania ukweli. Nipo nanyi.” Kweli alikuwa nasi na ili kutupunguza nguvu akapewa safari ya ghafla ya kwenda Paris.”
KUSHINDWA KWA WABUNGE
Habari za ndani zinasema baadhi ya wabunge waliokuwa wakipinga ufisadi huo walifuatwa majimboni mwao na mafisadi ili kuhakikisha hawarudi tena bungeni.
Baadhi ya wabunge hao na majimbo yao kwenye mabano ni Christopher Ole Sendeka (Simanjiro), Anna Kilango Malecela (Same Mashariki), David Kafulila (Kigoma Kaskazini) na James Lembeli (Kahama Mjini), Suleiman Zedi (Bukene), huku wengine wakiponea chupuchupu akiwemo Zitto, Kangi Lugora, Dk. Khamisi Kigwangalla na Spika Job Ndugai
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment