Thursday, 29 June 2017

Dawa Mpya ya UKIMWI Yaanza Kutumika Kenya.

Hatimaye Kenya imekuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuanza kutumia vidonge vya ugonjwa wa Ukimwi ambavyo vinaweza kuboresha afya na kurefusha maisha ya maelfu ya watu wanaosumbuliwa na magonjwa nyemelezi na ambayo hayakubali tiba nyingine.

Jina la dawa hiyo kitaalamu ni Dolutegravir (DTG), lakini itajulikana kama Tivicay, na inazalishwa na ViiV Healthcare, kampuni ambayo sehemu kubwa ya hisa zake inamilikiwa na GlaxoSmithKline.

DTG imekuwa dawa ambayo ni chaguo la kwanza la watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa miaka miwili iliyopita katika nchi za watu wenye kipato kikubwa kwa kuwa ina athari chache, ni rahisi kutumia kuliko dawa za ARV zinazotumika sasa (yaani kidonge kimoja kidogo kila siku).

Kwa kutumia dawa hiyo, kuna uwezekano mdogo kwa wagonjwa kutengeneza usugu, kwa mujibu wa tovuti ya unitaid.eu.

Mwaka 2015, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilipendekeza DTG iwe chaguo la kwanza kwa watu wazima na vijana, lakini hadi siku za karibuni watu wanaoishi na VVU katika nchi kama Kenya walikuwa hawawezi kupata dawa hizo.

Vidonge hivyo, ambavyo vilipitishwa kutumika nchini Marekani mwaka 2013, sasa vinagawiwa kwa wagonjwa 20,000 nchini Kenya kabla ya kupelekwa Nigeria na baadaye Uganda, kwa kusaidiwa na Unitaid, ambao ni wakala wa afya.

DTG ni dawa ambayo inatumiwa na watu wenye VVU ambao hawakuwahi kutumia dawa za kufubaza makali ya Ukimwi ya ARV.

“Nilikuwa na tatizo la mara kwa mara la kutokuwa na hamu ya kula,” alisema mkazi wa Nairobi, Doughtiest Ogutu alipozungumza na taasisi ya Reuters Foundation.

Ogutu alianza kutumia dawa hizo mwaka huu kwa sababu tiba nyingine hazikuwa zinamfaa.

“Hamu yangu ya kula imerejea, mwili wangu unafanya kazi vizuri.”

Ogutu, ambaye ameishi na VVU kwa miaka 15, alisema kiwango cha VVU mwilini mwake kimepungua kwa kiasi kikubwa kutoka virusi 450,000 hadi 40,000 tangu aanze kutumia DTG.

Nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara zimekuwa zikiathiriwa sana na Virusi vya Ukimwi kwa miongo kadhaa na karibu robo tatu ya wakazi wake wana Virusi vya Ukimwi na Ukimwi.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Ukimwi (UNAIDS) linalenga kuwa asilimia 90 ya watu watakaogundulika kuwa na VVU wawe wamepata dawa hiyo ifikapo mwaka 2020.

Karibu asilimia 15 ya wagonjwa wa VVU hawawezi kutibiwa kwa kuwa dawa hazifanyi kazi mwilini mwao, alisema Sylvia Ojoo, mkurugenzi wa Shule ya Afya ya Chuo Kikuu cha Maryland nchini Kenya, ambaye anasimamia dawa hizo.


Download  Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa

                            Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
                       Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
                       Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa

0 comments:

Post a Comment