Saturday, 24 June 2017

LEMA na Meya wa Arusha Wafunguka 'Tumechoshwa na Udhalimu na Uonevu Unaofanywa na DOLA Kwa Maagizo ya Viongozi" .

MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Meya wa Jiji Kalist Lazaro na naibu wake, Viola Likindikoki, wamesema wamechoshwa na kile walichokiita udhalimu na uovu wanaofanyiwa na vyombo vya dola kwa maagizo ya viongozi mkoani hapa.

Kutokana na kufanyiwa vitendo hivyo, wamesema wameamua kwenda kuwashtaki viongozi hao kwa Rais John Magufuli.

Walisema hayo katika tamko la pamoja jijini hapa jana ikiwa siku mmoja tu baada ya polisi kumkamata na kumshikilia Naibu Meya Viola kwa tuhuma za kurekodi na kutoa nje siri za vikao vya kamati na vya Baraza la Madiwani.

Meya Lazaro alisema: “Nalaani kwa nguvu zote udhalilishaji dhidi ya viongozi wa upinzani kwa kisingizio cha amri tunazoambiwa zinatoka juu.
“Yaani viongozi wa serikali wanashindana kufanya uovu kwa kunyanyasa wapinzani.”

Alisema kwa mfano, Meya wa Ubungo alikamatwa kwa amri ya aina hiyo ikaonekana Arusha hawajafanya hivyo siku nyingi, ndiyo wakamkamata Naibu Meya. “Sasa tumechoka”.

Kwa upande wake, Lema alisema: “Tunasema tumechoka.” “Sisi ni binadamu, tuna nyama, tuna damu, tuna familia, tuna ndugu na jamaa.”
Alisema anajua hatakubaliwa na kuruhusiwa kuonana na Rais Magufuli ili kumweleza kilio chao cha kuonewa na viongozi hao, hasa vijana aliowateua.

“Tumeamua Mstahiki Meya ambaye ni Katibu wa Chama Mkoa aandike barua na aombe kukutana na Rais kumweleza kilio chetu,” alisema Lema.

Akizungumzia tukio la jana, Meya Lazaro alisema kitendo kilichofanywa na polisi kumkamata naibu wake kwa kosa ambalo kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji wa Serikali za Mitaa lilipaswa kushughulikiwa na Kamati ya Maadili ya Baraza la Madiwani ni kulidhalilisha jeshi hilo.

“Polisi na hususani ofisi ya RCO (Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa) kitengo cha uchunguzi wa makosa ya mtandao hakihusiki na suala analotuhumiwa Naibu Meya kama kweli alitenda kosa hilo.

“Lakini hivi kwa akili ya kawaida Naibu Meya ni kiongozi wa vikao vya Baraza kama Meya hayupo, anasoma makabrasha hata yale yaliyopigwa mihuri ya siri, halafu anawezaje kuvujisha siri,” alihoji na kuongeza, “huku ni kujidhalilisha na kudhalilisha Jeshi la Polisi.”

Alisema kwa kuwa viongozi hawa wamezoea kukurupuka, Naibu Meya amemwandikia barua kumwomba aende akaonane na Rais Magufuli ili awachukulie hatua viongozi hawa ambao wengi historia zao zinafahamika kwa kukosa maadili.

Alidai hali hiyo inatokana na Baraza la Madiwani kuziba mianya yote ya ulaji kama vile kumpa mafuta ya gari Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya.

“Huko nyuma Halmashauri ya Jiji la Arusha lilikuwa shamba la bibi. Leo tumefanikiwa kupata hati safi, tumefanya vizuri kwenye sekta zote,” alisema.

Akizungumzia sababu za kukamatwa na kushikiliwa katika kituo kikuu cha polisi Arusha, Viola alisema pamoja na kushikiliwa kwa muda mrefu hakukuwa na mlalamikaji hadi polisi ilipompigia simu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Athumani Kihamia, ambaye alitoa maelezo kama mlalamikaji.

“Hawa polisi na wale waliowatuma wamefanya mchezo wa aibu. Yaani mimi niko chini ya ulinzi wa polisi nawauliza kosa langu wanadai nimetoa siri za vikao. Nikauliza mlalamikaji ni nani na wao hawajui wanasema ni amri kutoka juu. Hii ni kweli?” alisema.

Aidha alisema atalishtaki mahakamani Jeshi la Polisi kwa kupoteza baadhi ya vitu vyake ikiwamo simu ya mkononi wakati wakitekeleza amri ya kumkamata.

“Tunajua hofu ya wakubwa hawa ni kwa sababu ya maovu waliyofanya, sasa tunawaambia vitisho vyao hatuviogopi na ni vya kawaida,” alisema.

Naibu Meya alikamatwa na kushikiliwa kwa muda pamoja na madiwani wawili wa viti maalumu, Sabina Peter na Happyness Chale kwa tuhuma za kutoa siri za vikao vya baraza la madiwani wa Jiji la Arusha.


Download  Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa

                            Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
                       Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
                       Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa

0 comments:

Post a Comment