Vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge vitaanza tarehe 17 Oktoba hadi
tarehe 30 Oktoba 2016, Mjini Dodoma kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Tano
wa Bunge uliopangwa kuanza tarehe 1 Novemba 2016. Kufuatia Ratiba hiyo
ya shughuli za Kamati, Waheshimiwa Wabunge wote wanapaswa kuwa
wamewasili Mjini Dodoma ifikapo Jumapili tarehe 16 Oktoba, 2016 kwa
ajili ya kushiriki vikao hivyo.
Katika Vikao hivyo, shughuli zilizopangwa kutekelezwa na Kamati ni kama ifuatavyo:
- a) KUPOKEA MAONI YA WADAU WA MISWADA MBALIMBALI
Kamati mbili (2) za Kisekta zitajadili Miswada miwili ya Sheria
ambapo Kamati ya Katiba na Sheria itajadili Muswada wa Sheria ya
Marekebisho ya Sheria Mbalimbali, Na. 3 wa Mwaka 2016 [The Written Laws (Miscellaneous Amendments) Bill, 2016] na itakuwa na vikao vya kupokea maoni ya wadau kuhusu Muswada huo siku ya tarehe 21 Oktoba, 2016 katika Ukumbi wa Serengeti, Ofisi ya Hazina Mjini Dodoma kuanzia saa tano (5:00) Asubuhi ambapo Sheria hiyo ina jumla ya Sheria 9 zitakazofanyiwa marekebisho na Muswada huu.
Kamati nyingine ni Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ambayo itajadili Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa Mwaka 2016 [The Media Services Bill, 2016] na itakuwa na vikao vya kupokea maoni ya wadau kuhusu Muswada huo siku ya tarehe 19 Oktoba, 2016 Katika ukumbi ulipo katikaJengo la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Mjini Dodoma kuanzia saa tatu kamili (3:00) asubuhi hadi saa Tisa(9:000) Alasiri.
Pamoja
na kamati hizo mbili za kisekta, pia Kamati ya Sekta Mtambuka ambayo ni
Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo nayo imepanga kufanya mikutano ya
kusikiliza maoni ya wadau (Public Hearing)kuhusiana na Sheria
Ndogo zilizowasilishwa na Serikali katika Mkutano wa Nne wa Bunge.
Mikutano hiyo inatarajiwa kufanyika kati ya Jumanne tarehe 18 Oktoba, 2016 na Alhamisi tarehe 27 Oktoba, 2016 katika Jengo la Hazina (Treasury Square) Mjini Dodoma.
Wadau wote katika Miswada tajwa hapo juu wanakaribishwa kufika mbele ya Kamati kutoa maoni yao katika tarehe na muda uliotajwa.
- b) KUPOKEA TAARIFA ZA KIUTENDAJI WA WIZARA
Kamati tisa (9) za kisekta zitapokea Taarifa za utendaji wa
Wizara zinazosimamiwa na Kamati hizo kwa mujibu wa Kifungu cha 7 (1) (c)
na (d) cha Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo
Januari, 2016.
- i) Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama itapokea na kujadili Taarifa za wawakilishi wa Bunge katika SADC – PF, ACP – EU na CPA kwa mujibu wa Kifungu cha 7 (2) (iii) na (iv) cha Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016.
- ii) Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa itafanya ziara mbili Mkoani Dodoma kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya Wizara inazozisimamia kwa mujibu wa Kifungu cha 7 (1) (d) cha Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge
iii) Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) itapokea na
kujadili Taarifa za Uwekezaji unaofanywa na Mashirika/Taasisi za Umma
tisa (9).
- c) UCHAMBUZI WA TAARIFA KUHUSU HESABU ZILIZOKAGULIWA
Kamati mbili za usimamzi wa Fedha za Umma zitafanya uchambuzi wa
taarifa kuhusu Hesabu zilizokaguliwa kwa Mwaka unaoishia tarehe 30
Juni, 2015 ambapo Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) itachambua taarifa
kuhusu Hesabu zilizokaguliwa kwa Mwaka unaoishia tarehe 30 Juni, 2015.
Katika kipindi hicho, jumla ya Mashirika/Taasisi tisa (9) na Maafisa
Masuuli wa Mafungu (Votes) tatu (3) watakutana na Kamati kwa madhumuni
hayo.
Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) itachambua
Hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha
unaoishia tarehe 30 Juni, 2015, na Katika kipindi hicho, Hesabu za
Halmashauri kumi na sita (16) zitajadiliwa.
Ratiba zote za
Shughuli za Kamati za Bunge pamoja na Miswada itakayoshughulikiwa na
Kamati katika kipindi hiki inapatikana kupitia tovuti hii ya Bunge.
0 comments:
Post a Comment