Naibu
wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt.
Hamisi Kigwangalla ameagiza kufungwa mara moja Chumba cha upasuaji cha
hospitali ya Sanitas ya Mikocheni Jijini Dar es Salaam baada ya kubaini
kuwa na kasoro mbalimbali ikiwemo mfumo na ramani yake kimefungwa kwa
kutokidhi vigezo vya kimataifa vya namna chumba hicho kinavyotakiwa
kuwa.
Dk.
Kigwangalla ametoa agizo hilo mapema jana Februari 29.2016, alipofanya
ziara ya kushtukiza kwenye hospitali hiyo majira ya saa nane na nusu
mchana ambapo baada ya kutembelea hospitali nzima na kushuhudia namna
ya utolewaji wa huduma, hakuridhishwa na hali aliyokutana nayo kwenye
chumba hicho na kutoa maagizo kwa Msajili wa Hospitali Binafsi, Dkt.
Pamela Sawa kufunga chumba hicho mpaka uongozi wa hospitali hiyo
utakapofanya marekebisho ya mapungufu yaliyopo.
“Chumba
cha upasuaji hakiko sawa, siwezi kuvumilia kuacha chumba hiki kiko
chini ya kiwango cha kimataifa. Rekebisheni chumba hiki kwa kutumia
mfumo wa ramani wa wizara,” alieleza Dkt. Kigwangalla wakati wa kutoa
maagizo kwa mmoja wa Ofisa wa Hospitali hiyo.
Aidha
uongozi wa hospitali hiyo umepewa siku saba wawe wamewasilisha maelezo
ya kutowalipa mishahara kwa kipindi cha miezi minne watumishi wake
pamoja na jinsi wanavyoteketeza taka hatarishi za hospitali hiyo.
Katika
ziara hiyo Naibu Waziri huyo alipata malalamiko kutoka kwa watumishi
hao ambao wamelalamikia kukatwa kwa makato ya mafao pasipo kupelekwa
mahali husika kwa zaidi ya miaka mitatu na nusu.
Dkt.
Kigwangalla alivitaja viwango vya chumba cha upasuaji kuwa kinatakiwa
chumba cha kubadilishia mavazi,kunawa mikono,sehemu ya alama maalum
zenye rangi nyekundu, meza ya upasuaji, ukanda wa usafi, chumba cha
mapunziko baada ya kutoka kwenye upasuaji na chumba cha kusafishia vifaa
vya upasuaji na kuna mashine maalum kwa kuwa kila upasuaji una idadi ya
vifaa vinavyotumika.
Aliongeza kuwa viwango hivi vinawekwa ili kuepuka maambukizi.
Kwa
upande wake Meneja Uendeshaji wa hospitali hiyo, Bi. Gean Cabral
alisema watarekebisha mapungufu yaliyobainika pamoja na kufanya yale
yote waliyoagiziwa baada ya tukio hilo.
0 comments:
Post a Comment