Sunday, 13 March 2016

#YALIYOJIRI>>>Katibu Mtendaji NACTE Ajiuzulu....Ni Kutokana na Tuhuma za Kughushi Vyeti.Fahamu zaidi hapa.

Aliyekuwa Katibu Mtendaji wa NACTE Dokta Primus D Nkwera (kulia) akifafanua jambo
 
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la  Elimu ya Vyuo vya Ufundi( NACTE),Dr. Primus Nkwera amejiuzulu nafasi yake.

Uamuzi wa kujiuzulu  kwa  Dr. Nkwera ulitangazwa katika ofisi  kuu  za Baraza  hilo  zilizopo  Mikocheni  Dar es Salaam juzi na Mwenyekiti  wa  Bodi,Mhandisi Steven Mlote na kusababisha  baadhi  ya  wafanyakazi  kuangua  kilio.

Akizungumza katika kikao cha dharura cha wafanyakazi wote wa baraza hilo,Mlote alisema Dr. Nkwera amejiuzulu  ili  kulinda  hadhi  ya Nacte kutokana  na  habari iliyoandikwa na Gazeti la Dira ikimtuhumu mambo mbalimbali.

Gazeti  hilo la Dira la Jumatatu tarehe 07/03/2016 toleo no.405 lilimtuhumu Katibu Mtendaji wa NACTE, Dr.Primus Nkwera  kughushi vyeti vya shahada ya uzamivu  baada ya kusomeshwa na serikali Afrika Kusini na kufeli.

Mlote alisema kwa mujibu wa Dr. Nkwera, nafasi hiyo haipaswi kushikwa na mtu mwenye tuhuma  ya  aina  yoyote, na ametafakari na kuona ajiweke kando na uongozi wa Nacte ili uchunguzi ufanyike akiwa pembeni.

"Tumetumia muda mwingi kutafakari hoja  ya  Dr. Nkwera na hatimaye tumekubali kujiuzulu kwake kwa shingo upande," alisema Mlote na kuongeza:

"Kazi kubwa iliyofanywa na Dr. Nkwera akiwa kiongozi wa Nacte inafahamika na kila mmoja, vilio na machozi ya wafanyakazi wenzake yanadhihirisha kuwa kujiuzulu kwake kunaacha simanzi kubwa.

"Najua mmepata mshtuko mkubwa, lakini Dr Nkwera hajafa, yuko hai na huyu bado ni mtumishi wa serikali. Alichofanya ni kuamua kuachana na ukatibu utendaji.

"Tutaendelea kumtumia itakapobidi kwa ushauri.Wakati mwingine lazima mkubaliane  na  hali  hii, lakini pia  endeleen kuchapakazi kwa ufanisi kama  kawaida kana kwamba bado mko na Dr. Nkwera."

Kutokana  na  kujiuzulu  kwake, Mlote alisema bodi imemteua Mkurugenzi wa Mitaala wa Nacte, Dr Adolf Rutayunga kukaimu nafasi hiyo  wakati taratibu nyingine zikiendelea.

Akizungumza na wafanyakazi hao, Dr. Rutayunga alisema viatu alivyoviacha Dr. Nkwera ni vikubwa kwake, lakini  akaahidi kuendeleza yote  aliyoyaacha.

0 comments:

Post a Comment